Tafuta

Papa huko Jakarta akutana na walemavu na wagonjwa

Baba Mtakatifu,katika makao makuu mapya ya Baraza la Maaskofu wa Indonesia,alikutana na wagonjwa karibu mia,watu wenye ulemavu na maskini wanaosaidiwa na mashirika mbalimbali ya upendo akiwafafanua kama nyota ndogo angavu angani ya visiwa hivyo.Shuhuda za mtu aliyepoteza uwezo wa kuona na kijana mwenye usonji mdogo zilisikika.

Na Alessandro Di Bussolo na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, kwa utamu na ukaribu, aliwasalimia wagonjwa mia moja, watu wenye ulemavu na maskini wanaosaidiwa na mashirika ya Upando  ya Kanisa la Indonesia,  wakati wa kukutana nao mwishoni mwa asubuhi ya pili huko Jakarta, kwenye makao makuu mapya ya Baraza la Maaskofu Indonesia. Papa aliwaeleza kuwa “"Nyinyi ni nyota ndogo angavu angani ya visiwa hivi, washiriki wa thamani sana wa Kanisa hili. Alimpongeza Mikahil, kijana aliye na usonji mdogo ambaye alichaguliwa katika kikosi cha Jakarta Mashariki kwa Michezo ya Kuogelea ya Walemavu na ameomba apigiwe makofi kwa kila mtu, “kwa sababu sote tumeitwa pamoja kuwa mabingwa wa upendo katika Olimpiki kubwa ya maisha.”

Mahitaji mahalia

Muda mfupi wa mkutano uliochukua chini ya saa moja, baada ya Mkutano wa Kidini katika  msikiti, Papa anawasili saa 4.45 asubuhi masaa ya Jakarta (saa 11.45 nchini Italia), akikaribishwa na rais wa Baraza la Maaskofu wa Indonesia, Askofu Antonius Franciskus Subianto Bunyamin, wa Jimbo la Bandung, na Kardinali Ignatius Suharyo. Katika makao makuu mapya, katikati mwa jiji la Jakarta, yaliyozinduliwa na kubarikiwa mnamo tarehe 15 Mei 2024, Papa Francisko alisindikizwa hadi ghorofa ya nane, katika Ukumbi wa Henry Soetio. Hapo Askofu  Subianto alimsalimia, akikumbuka kwamba “maisha na kazi yake inadhihirisha huruma ya Yesu kwetu, hasa kwa kuwatunza ndugu zetu maskini, wanyonge, waliotengwa na wanaoteseka.” Na kwamba kuadhimisha miaka mia moja ya Baraza la Maaskofu Katoliki Indonesia, Kanisa la mahali linazingatia mahitaji ya wale walio katika vitongoji.

Ushuhuda wa Mimi

Mimi Lusli, ambaye alipoteza uwezo wake wa kuona akiwa na umri wa miaka 17, alizungumza karibu na askofu huyo na kusema alipata faraja katika Njia ya Msalaba, ambako alikutana na Yesu, ambaye “hakuniacha, bali alinifundisha kuendesha maisha bila kuona kimwili.” Anakiita “kinara chetu cha matumaini” na alisema ana uhakika kwamba “Mungu aliumba wanadamu wenye uwezo wa kipekee ili kuimarisha utofauti wa ulimwengu wetu, na ulemavu ni mojawapo tu ya vipengele hivi vya kipekee.” Alisisitiza kwamba jukumu la Kanisa “ni muhimu katika kuhakikisha utu wa binadamu na kwa sababu hiyo, kama Wakatoliki, lazima tuwajibike na kuunga mkono kikamilifu haki za watu wenye ulemavu. Lakini uwepo wa Papa na huruma, alihitimisha, unatuhakikishia kwamba hatutasahaulika kamwe.”

Papa akisikiliza shuhuda
Papa akisikiliza shuhuda

Historia ya Mikail

Mikail Andrew Nathaniel, mwenye umri wa miaka 18 amegunduliwa kuwa na ugonjwa mdogo wa tawahudi na ulemavu mdogo wa kiakili. Alijaribu kuzungumza bila kusoma hotuba iliyoandaliwa, lakini kisha aliomba msaada kwa maelezo yaliyoandaliwa. Yeye alimwambia Papa Francisko kwamba “wazazi wangu wananipenda bila masharti na hunipa mtaalamu bora katika jiji.” Mikail anataka kuwa mtu wa kujitegemea, na hivyo pamoja na kuchaguliwa katika kikosi cha Jakarta Mashariki kwa Michezo ya kuogelea ya Walemavu, alisema anahudhuria kozi ya bar na masomo ya kupiga gitaa na ngoma.

Utajiri wa utofauti

Katika salamu zake, Papa Fransisko alisisitiza kwamba, “Ni jambo zuri sana kwamba Maaskofu wa Indonesia walichagua kuadhimisha miaka 100 ya Baraza lao la Kitaifa pamoja na wagonjwa, watu wenye ulemavu na maskini. Aidha Papa anakubaliana kabisa na kile alichosema Mimi kwamba: “Mungu aliumba wanadamu wakiwa na uwezo wa kipekee ili kutajirisha utofauti wa ulimwengu wetu.” Na yeye mwenyewe alitudhihirishia hilo kwa kusema nasi kwa njia ya ajabu kuhusu Yesu, “mwenye mwanga wa tumaini letu.” Na asante kwa hili. Kukabiliana na matatizo pamoja, sote tukifanya vyema tuwezavyo, kila mmoja  kutoa mchango wa kipekee, hututajirisha na hutusaidia kugundua siku baada ya siku jinsi kuwa kwetu pamoja, ulimwenguni, Kanisani, katika familia kunafaa."

Umuhimu wa kupendana

Sisi sote tunahitajiana, alihitimisha Baba Mtakatifu na hili si jambo baya: kiukweli, hutusaidia kuelewa vyema na vizuri zaidi kwamba upendo ni jambo muhimu zaidi katika maisha yetu, kutambua jinsi watu wengi wazuri wapo karibu nasi.” Na kisha alitukumbusha “jinsi gani Bwana anatupenda sisi sote, zaidi ya mipaka na magumu yoyote. Kila mmoja wetu ni wa kipekee machoni pake, machoni pa Bwana na Yeye kamwe hatusahau.” Kwa kuongeza Papa alisema:  “Hebu tukumbuke hili, kuweka tumaini letu hai na kujitolea, bila kuchoka kamwe, kufanya maisha yetu kuwa zawadi kwa wengine.”

Papa alikutana na walemavu na wagonjwa
Papa alikutana na walemavu na wagonjwa

Maombi ya ukweli wa upendo

Mkutano huo unamalizika kwa sala iliyosomwa na Askofu wa Wakarmeli Henricus Pidyarto, askofu anayesimamia tume ya kiliturujia. “Wape watu wako huruma isiyo na kikomo ili wakutambue kama Baba ambaye anatupenda bila masharti. Njooni kwa huruma kutusaidia, tunakuomba, ili, tukipokea kwa furaha kutoka kwenu furaha ya Injili, tuweze kuwatumikia kaka na dada zetu dhaifu, waliotengwa, wanaoteseka, walemavu, wagonjwa na walioachwa.

Zawadi za mwisho na salamu

Papa alitoa mchango kwa Baraza la Maaskofu wa Indonesia Picha kubwa ya Bikira wa Portaitissa, taswira maalum ya Bikira Maria ‘Odighitria’ ambayo kwa Kigiriki ina maana “Yeye anayeonesha njia” - na ambayo kwa jadi ni  Maria akiwa na Mtoto Yesu. katika mkono wake wa kushoto, akiuelekeza kwa mkono wa kulia. Na kabla ya kuondoka kwenye Jumba la Henry Soetio alitia saini bango la marumaru la Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu. Kisha yeye binafsi aliwasalimia na kuwabariki wote waliokuwapo. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko aliwabariki na kuwakumbatia waamini wengi kwa bendera za Vatican kwa tabasamu lake na Indonesia, ambao walisongamana kwenye korido ya kuingilia ya makao mapya uaskofu, iliyopambwa kwa misaada mikubwa.

Papa akutana na walemavu na wagonjwa
05 September 2024, 10:40