Papa amewasili Indonesia.Ziara ya 45 ya kitume inaanza!
Vatican News.
Papa Francisko amewasili nchini Indonesia saa 12.19 asubuhi kwa saa za Roma, ambapo ilikuwa ni saa 5.19 asubuhi kwa saa za ndani, kwa Ndege ya Shirika la Ita iliyoondoka tarehe 2 Septemba 2024 saa 11.32 jioni kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Fiumicino Roma na ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Soekarno-Hatta, Jakarta ambapo ilikuwa ni hatua ya kwanza ya safari ya Asia na Oceania, katika Ziara ya 45 ya Kitume Kimataifa na ndefu zaidi ya Upapa wake. Aliyemkaribisha Papa, chini ya ngazi za mbele, pamoja na wengine kulikuwa na Waziri wa Mambo ya Kidini na watoto wawili waliovalia mavazi ya kiutamaduni wakiwa na zawadi ya maua.
Baada ya salamu za wajumbe na Walinzi wa Heshima, Baba Mtakatifu alihamia Makao ya Ubalozi wa Vatican, ambako alikutana na kundi la wagonjwa, wahamiaji na wakimbizi wakisindikizwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio na Huduma ya Shirika la Wajesuit kwa ajili ya Wakimbizi.
Mipango inayofuata
Ziara rasimi na mipango ya Papa itakuwa hai kuanzia tarehe 4 Septemba, kwa sherehe ya kukaribishwa nje ya Ikulu ya Rais na kwa ziara ya heshima kwa Rais wa Jamhuri hiyo. Baadaye kutakuwa na mkutano wa kwanza wa hadhara, ule kwa mamlaka, pamoja na mashirika ya kiraia na mabalozi, ikifuatiwa na mkutano wa faragha na wanashirika wa Shirika la Yesu (Jesuit) katika Ubalozi wa Vatican nchini humo na kukutana na maaskofu, mapadre, mashemasi, wanaume na wanawake waliowekwa wakfu, waseminari na makatekista katika Kanisa Kuu la Mama yetu wa Kupalizwa, hadi kufunga siku ya mkutano na vijana wa Scholas Occurrentes katika ‘Grha Youth House Pemuda.’
Telegramu kwa nchi alizopitia kwa juu
Mbali na telegramu kwa mkuu wa Serikali ya Italia, Bwana Sergio Mattarella - ambamo Baba Mtakatifu Francisko alionesha umuhimu wa mikutano inayomngojea “katika mataifa yale tajiri kwa maadili ya kibinadamu na kiroho, kushirikishwa katika roho ya ushirika, mshikamano na mazungumzo hata katika nyakati na hali zenye majaribu,” Papa pia alituma ujumbe kwa marais na mamlaka ya nchi nyingine alizopitia kwa ndege Juu wakati wa safari ya kuelekea Indonesia: Kroatia, Bosnia na Herzegovina, Serbia au Montenegro, Bulgaria, Uturuki, Iran, Pakistan, India, Malaysia.
Papa Francisko kwa njia hiyo alitoa salamu zake kwa watu mbali mbali, anawahakikishia maombi yake ili waweze kuishi katika maelewano na ustawi wa kidugu, na kuwaombea baraka za kimungu za amani, ustawi na umoja juu ya mataifa.