Papa ahimiza Makardinali kurudisha dhamira ya mageuzi ya kiuchumi
Vatican News
Katika barua aliyoiandika kwa ajili ya Baraza la Makardinali, tarehe 16 Septemba 2024, Baba Mtakatifu Francisko alibainisha kwamba miaka kumi imepita tangu kuanza kwa mageuzi ya Curia Romana na akawakumbusha wajibu na nafasi yao katika suala hilo. "Katika jukumu lenu la kumsaidia Papa wa Kirumi katika kutawala Kanisa la ulimwengu wote, kazi ya kusindikiza na wale wanaohusika katika mchakato huu wa mabadiliko imeangukia juu yenu, ndugu Kardinali,"aliandika. Akitafakari juu ya maendeleo yaliyopatikana tangu kuanza kwa mageuzi hayo, kutokana na kuchapishwa kwa hati ya kitume ya Praedicate Evangelium, yaani hubirini Injili ambayo ni Katiba ya Kitume iliyopanga kwa upya Curia Romana na kuweka msingi wa juhudi za mageuzi katika taasisi zote za Vacan, Papa Francisko alibainisha kwamba kanuni ya Ecclesia semper reformanda, yaani “Kanisa lazima kurekebishwa daima”—kama roho inayoongoza nyuma ya mabadiliko. Akibainisha kwamba kuundwa upya kwa Curia Romana kunalenga kuhakikisha kunamsaidia Mrithi wa Petro katika kutekeleza utume wake mkuu wa kichungaji katika huduma kwa Kanisa zima na Makanisa mahalia, Papa alitambua juhudi na sadaka za wanaume na wanawake ambao wamejitolea kwa kuchukuliwa kwa utaratibu huu wa kufanywa upya na kusema, “Upya huu ni ushuhuda wa uhai na neema.”
Haja ya mageuzi ya kiuchumi
Baba Mtakatifu amesisitiza haja ya kuendelea kuzingatia mageuzi ya kiuchumi, mada ambayo imejadiliwa kwa mapana wakati wa Mkutano mkuu kabla ya uchanguzi wa mwaka 2013. "Miaka iliyopita imeonesha kwamba maombi ya mageuzi, ambayo wanachama wengi wa Baraza la Makardinali wamefanya hapo awali, yalikuwa ya kuona mbali," aliandika. Marekebisho haya, aliendelea, yamesaidia kukuza ufahamu kwamba "rasilimali za kiuchumi katika huduma ya utume ni ndogo na lazima zidhibitiwe kwa ukali na umakini." Kwa hivyo, Papa Francisko alitoa wito kwa juhudi mpya za kuondoa nakisi ya bajeti ya Vatican na kuzitaka taasisi za Vatican kufanya kazi ili kufikia "upungufu sufuri" kama lengo linalowezekana. Alisisitiza sera za kimaadili ambazo zimewekwa ili kuboresha utendaji wa kifedha, huku pia akihimiza kila taasisi kutafuta rasilimali kutoka nje ili kuunga mkono dhamira yao. Juhudi kama hizo, alisema, lazima ziwe mfano wa "usimamizi wa uwazi na uwajibikaji katika huduma ya Kanisa."
Mshikamano na kupunguza gharama
Katika barua yake, Papa Francisko pia alizungumzia umuhimu wa mshikamano kati ya vyombo vya Vatican. "Taasisi za Vatican zina mengi ya kujifunza kutokana na mshikamano wa familia nzuri," alisema, akiongeza kwamba "wale walio katika hali nzuri ya kifedha huwasaidia wale wanaohitaji." Aina hii ya ukarimu imejikita katika Injili, aliendelea, na ni msingi muhimu wa kuomba ukarimu kutoka kwa wengine nje ya Kanisa. Akitoa wito kwa hatua madhubuti za kupunguza gharama zisizo za lazima ndani ya Vatican, Papa alihimiza Curia Romana kukumbatia roho ya “umuhimu” katika utendaji wake, “kuepuka mambo ya kupita kiasi na kuchagua kwa uangalifu vipaumbele vyetu, kusitawisha ushirikiano na mshikamano wa pamoja.” "Lazima tufahamu kwamba leo tunakabiliwa na maamuzi ya kimkakati ya kufanywa kwa uwajibikaji mkubwa, kama tunavyoitwa kuhakikisha mustakabali wa Utume,” aliandika.
Ujasiri na ushirikiano
Katika kuhitimisha barua yake, Baba Mtakatifu Francisko aliwaalika Makardinali kuunga mkono mageuzi yanayoendelea kwa “ujasiri, moyo wa huduma, na ukarimu.” Aliwahimiza kuchangia ipasavyo katika mchakato huo kwa kushirikishana ujuzi na mang’amuzi yao, huku akisisitiza kwamba, kazi ya kila taasisi ni sehemu ya jumla kubwa zaidi, iliyounganishwa katika utume wa pamoja wa kulihudumia Kanisa. “Kila moja ya taasisi za Vatican zinaunda, pamoja na wengine wote, chombo kimoja,” Papa aliwakumbusha Makardinali, “Kwa hiyo, ushirikiano wa kweli na mshikamano kuelekea lengo moja la wema wa Kanisa ni hitaji muhimu la huduma yetu.”