Papa atuma ujumbe kwa vijana huko Tirana:Ninyi ni mstakabali wa Mediterania!

Baba Mtakatifu ametuma ujumbe kwa njia ya video kwa vijana washiriki wa Mkutano wa Mediterrane 2024 unaofanyika huko jiji la Tirana nchini Arbania, kuanzia 15-21 Septemba 2024 akiwatia moyo ili wawe walinzi wa amani,umoja na udugu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Jumanne tarehe 17 Septemba 2024, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia Ujumbe kwa njia ya video kwa washiriki wa Mkutano wa Mediterania (MED2024) unaoongozwa na mada Wanahija wa matumaini wajenzi wa amano huko jijini Tirana kuanzia tarehe 15 hadi 21 Septemba 2024. Katika ujumbe huo baba Mtakatifu anaanza kusema kuwa “Wapendwa Marafiki, vijana wapendwa kutoka Albania na kutoka eneo la Mediterania, ni furaha kubwa kwangu kujua kwamba mmekusanyika huko Tirana miaka kumi baada ya ziara yangu katika nchi yenu pendwa, mwaka wa 2014 - na ninawahakishia kwamba sisahau!  na ninakumbuka safari hiyo isiyosahaulika, nilipokutana na watu wenu, watu waliotajirishwa na nyuso kadhaa tofauti lakini waliounganishwa na ujasiri uleule. Kama nilivyowaambia vijana katika hafla hiyo: "Nyinyi ni kizazi kipya cha Albania", sasa nataka kuongeza, kwa ajili yenu vijana wapendwa kutoka pwani tano za Bahari ya Mediterania: "nyinyi, kizazi kipya, ninyi ni mustakabali wa eneo la Mediterania”.

Jifunzeni pamoja ili kujua alama za nyakati

Baba Mtakatifu akiendelea amesema “Sisi sote ni mahujaji wa matumaini, tunatembea katika kutafuta ukweli, kuishi imani yetu na kujenga amani - kwa sababu amani inahitaji kujengwa! Mungu anampenda kila mtu; Yeye hafanyi tofauti kati yetu. Udugu kati ya pwani tano za Mediterania ambazo mnatoka ndio jibu, kiukweli ni jibu! -, jibu bora tunaweza kutoa kwa migogoro na kutojali mbaya. Ninawaalika tujifunze pamoja ili kutambua alama za nyakati. Tafakarini tofauti ya mapokeo yenu kama utajiri, utajiri ambao Mungu anataka kuwa. Umoja sio usawa, na utofauti wa utambulisho wenu wa kitamaduni na kidini ni zawadi ya Mungu. Umoja katika utofauti. Hebu kuheshimiana kukue baina yenu kwa kufuata ushahidi wa baba zenu. Weka katikati sauti ya wale ambao hawazingatiwi, na hapa ninafikiria watu masikini zaidi, wale wote wanaoteseka kuzingatiwa kama mzigo au shida. Ninafikiria juu ya wale ambao wanalazimika kuondoka katika nchi zao, hata katika umri mdogo sana, kutafuta maisha bora ya baadaye.

Tunzeni kila mtu na sio idadi, ni watu na kila mtu ni mtakatifu

Papa Francisko amezidi kukazia kwamba “Tafadhali, mtunze kila mtu: sio idadi tu, lakini ni watu, na kila mtu ni mtakatifu. Tunazungumza juu ya nyuso za kibinafsi ambazo utu wake lazima uimarishwe na kulindwa. Tuachane na utamaduni wa kutojali, tufungue mlango wa kukubalika na urafiki. Kama katika Ziwa kubwa la Tiberia tu ambalo sasa limekabidhiwa uangalizi wenu, mnakaa katika ufukwe wa bahari hii inayokuunganisha - Mediterania inakuunganisha! Inawakusanya kama kwenye bustani nzuri tu mliyoitwa kuipalilia. Kisha mnahifadhi roho ya huduma katika kila hali, mkitunza kila kiumbe kilichokabidhiwa mikononi mwenu. Mnaweza kutembea kwa kufuata nyayo za mashahidi wenu. Ujasiri wao ni shahidi hai anayeweza kutia moyo kujitolea kwenu  katika kupinga vurugu zote zinazoharibu ubinadamu wetu, kama Mwenyeheri Maria Taci alivyofanya, alipokuwa na umri wa miaka 22 pekee.” Kadhalika Baba Mtakatifu amewakabidhi wote kwa Maria, Mama wa Shauri Njema”. Daima amekuwa mama mzazi  kwa upendo kama katika huzuni, kwenye matukio ya nchi yao. Wajifunze kutoka kwa Moyo wake Safi kuwa mahujaji wasiotulia wa matumaini na kufuata ishara za Mungu, ili eneo la Mediterania liweze kurejesha sifa yake bora zaidi: usemi wa udugu na amani, na lisingekuwa tena kaburi!

Ujumbe wa Papa kwa vijana wa Tirana (MED24)
17 September 2024, 09:49