Tafuta

2024.09.20 Papa Francisko akutana na Harakati Maarufu nchini Italia(Movimenti Popolari). 2024.09.20 Papa Francisko akutana na Harakati Maarufu nchini Italia(Movimenti Popolari).  (Vatican Media)

Papa Francisko kwa Harakati Maarufu:Pambania haki za kijamii na kiuchumi!

Ijumaa tarehe 20 Septemba,Baba Mtakatifu akikutana na wawakilishi wa Harakati Maarufu zikiadhimisha miaka kumi ya mkutano wao wa kwanza mjini Vatican,aliwatia moyo katika vita vyao dhidi ya dhuluma za kijamii na akarudia pendekezo lake la Mapato Msingi kwa Wote na ushuru wa juu kwa mabilionea.

Na Tiziana Campisi na Angella Rwezaula -Vatican

Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 20 Septemba 2024 alitembelea Makao makuu ya Baraza la Kipapa kwa ajili ya Kuhamasisha Maendeleo Fungamani ya Binadamu kwa ajili ya tukio la “Kusimika Bendera Dhidi ya Udhalilishaji.” Waliomngojea walikuwa wawakilishi wa Harakati Maarufu, wakati wakiadhimisha kumbukumbu ya miaka kumi tangu walipofanya Mkutano wao wa Kwanza Ulimwenguni wa Haharakati Maarufu(WMPM) na Papa, ambao ulifanyika mjini Roma mnamo mwaka 2014. Huo ni Mkutano na nafasi ya udugu kati ya mashirika ya msingi kutoka mabara matano, unaohamasisha utamaduni wa kukutana katika kuunga mkono maneno matatu ya lugha ya kihispania(Techo, Tierra, Trabajo(T3) maana yake: (Nyumba, Ardhi, Kazi,) inayolenga kufanya mazungumzo na kutafakari juu ya safari ya tangu 2014 kushughulikia changamoto za leo  hii kwa ajili ya haki kijamii na amani katika nyumba yetu ya pamoja. Baba Mtakatifu Francisko alipofika, alikaa kati ya washiriki, huku akisikiliza mjadala wao juu ya kuhakikisha kwamba “hakuna familia isiyo na makazi, hakuna mkulima asiye na ardhi, hakuna mfanyakazi asiye na haki na hakuna mtu asiye na heshima inayotokana na kazi,” kama kauli mbiu ya Maharakati hayo (WMPM),isemavyo.

Papa katikati ya Harakati Maarufu mjini Vatican
Papa katikati ya Harakati Maarufu mjini Vatican

Kukuza udugu

Papa alitoa hotuba ndefu, iliyozungumzwa kwa lugha ya Kihispania na nyongeza ya kifungu, ambapo alizungumzia haki ya kijamii, akitaka huduma kwa walio hatarini zaidi hasa wazee, watoto na maskini na kusisitiza thamani ya huruma, ikimaanisha kuteseka pamoja na wengine, kuwa karibu nao na kuwa sauti ya wasio na sauti. Alitoa wito kwa matajiri kugawana rasilimali zao, huku akiwakumbusha kuwa: “Utajiri hufanywa kwa kugawanywa, kuunda na kukuza udugu.” Papa alisisitiza kwamba “bila upendo sisi si kitu na kwamba mahusiano yote yanapaswa kujengwa juu ya upendo huu, kwani haki lazima ifuatwe bila vurugu, kama inavyooneshwa na mjane katika Injili..

Uchoyo wa matajiri

Papa Francisko aliakisi aidha mada kuu kutoka katika Waraka wake wa Kitume wa Evangelii Gaudium, yaani Injili ya Furaha: "hitaji la kushughulikia shida za maskini kwa kukataa uhuru kamili wa soko na uvumi wa kifedha." Alionesha kwamba “sote tunawategemea maskini, hata matajiri.” Papa alikiri kwamba wengine wanamkosoa kwa kusema zaidi juu ya maskini kuliko watu wa tabaka la kati, lakini alisisitiza kwamba, Injili inawaweka maskini katikati. Alionya kwamba ikiwa hakuna sera za haki zinazohakikisha upatikanaji wa ardhi, nyumba,na mishahara ya haki, “mantiki ya uchafu wa nyenzo na wa kibinadamu itaenea, ikitayarisha njia ya jeuri na ukiwa. Papa alisisitiza kuwa: “Kwa bahati mbaya, mara nyingi ni matajiri zaidi ambao wanapinga utimilifu wa haki ya kijamii au ikolojia fungamani kutokana na uchoyo mtupu. Uchoyo huu mara nyingi umefunikwa na itikadi lakini", kulingana na Papa, "ni ubakhili uleule unaoshinikiza serikali kuunga mkono sera zenye madhara."

Kugawana Rasilimali

Papa alionesha matumaini kwamba watu binafsi wenye uwezo wa kiuchumi wangetoka katika kutengwa, kukataa usalama wa uwongo wa pesa na kukumbatia kugawana bidhaa, ambayo ni  hatima ya ulimwengu wote, inayotokana na Uumbaji wenyewe. Alisisitiza kwamba mali lazima igawiwe “si kama zawadi,” bali “kidugu.” Alizihimiza kwa hiyo Harakati hizo Maarufu kudai mabadiliko haya, akibainisha kuwa mtazamo potovu wa ukweli unainua mkusanyiko wa mali kama fadhila, wakati kiukweli ni tabia mbaya. “Kulimbikiza sio wema, bali kusambaza,  kwa sababu Yesu hakukusanya; badala yake alizidisha,” Papa alikumbusha hayo akirejea mafundisho ya Kristo juu ya kutoweka hazina duniani, bali mbinguni.

Kilio cha waliotengwa

Baba Mtakatifu aidha alishutumu ushindani usiozuiliwa wa kupata mali kuwa “nguvu yenye uharibifu, inayoongoza kwenye upotevu akiita “kutowajibika, ukosefu wa adili, na usio na akili. Uchoyo huu, unagawanya ubinadamu na kuharibu uumbaji. Kwa njia hiyo aliwataka viongozi kuzingatia kilio cha waliotengwa, ambacho kina uwezo wa kuamsha dhamiri za viongozi wa kisiasa wenye jukumu la kutekeleza haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Haki hizi, alibainisha, zinatambuliwa na mataifa mengi na Umoja wa Mataifa, lakini bado hazijatimizwa katika hali halisi ya kijamii na kiuchumi. “Ushindani usiodhibitiwa wa utajiri ni nguvu ya uharibifu, inayoongoza kwenye upotevu.”

Papa akiwa na Harakati Maarufu
Papa akiwa na Harakati Maarufu

Huruma

Papa akiendelea alisisitiza kwamba “Haki, lazima iambatane na huruma, ambayo inamaanisha kuteseka pamoja na wengine, kushiriki hisia zao. Huruma sio kutoa hisani kutoka katika nafasi ya upendeleo bali kuwaendea wengine kwa huruma na mshikamano. Huruma ya kweli hujenga umoja na uzuri wa dunia,” Papa Francisko alikazia.

Hakuna anayepaswa kudharauliwa

Papa pia alilaani utamaduni wa washindani, ambao ni kipengele cha utamaduni wa upotevu. Kitendo hiki, ambacho mara nyingi kinategemea kunyonya watu au maumbile, au kufaidika na uvumi wa kifedha, ukwepaji wa ushuru, au uhalifu uliopangwa, huwaongoza wengine kudharau kwa kiburi wale wanaoitwa hasara.” Kwa maana hiyo Baba Mtakatifu  alionya kwamba “mtazamo huu wa kuwadharau wengine, kwa kutojali au dharau huchochea jeuri. Ukimya katika kukabiliana na dhuluma hufungua njia ya mgawanyiko wa kijamii, migawanyiko ya kijamii inafungua njia ya unyanyasaji wa maneno, unyanyasaji wa maneno hufungua njia ya unyanyasaji wa kimwili,na unyanyasaji wa kimwili hufikia hadi vita,” alisisitiza.

Wito kwa upendo

Baba Mtakatifu Francisko  alizidi kuthibitisha hitaji la upendo katika kila nyanja ya maisha. Alitaja ziara yake ya hivi karibuni katika shule ya watoto walemavu huko Dili, Timor ya Mashariki, akisema, “Bila upendo, hilo halingekuwa na maana.” Alikumbusha Harakati Maarufu zinazojulikana kwamba: ni “haki ya kijamii na ikolojia fungamani zinaweza kueleweka tu kupitia upendo.

Darwin ya kijamii

Kadhalika  Papa alionya kwamba harakati za ubinafsi na ubinafsi husababisha aina ya Mtindo wa Darwin ya kijamii, ambapo sheria ya wenye nguvu zaidi inahalalisha kutojali na ukatili. Alitaja hili kuwa linatoka kwa yule Mwovu, na kuzihimiza Harakati hizo Maarufu kupinga jaribio lolote la kufuta kumbukumbu au utambulisho wa kiutamaduni, unaoashiriwa na marejeo yake ya Mamba wanaotaka kula maadili ya jamii."

Papa Francisko katikati ya Wajumbe wa Harakati Maarufu
Papa Francisko katikati ya Wajumbe wa Harakati Maarufu

Janga la uhalifu uliopangwa

Papa Francisko alielezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa uhalifu wa kupangwa, ambao hustawi kwa umaskini na kutengwa. Alitoa wito wa kuendelea na mapambano dhidi ya uchumi wa uhalifu kupitia uchumi maarufu, akisisitiza kwamba hakuna mtoto au mtu anayepaswa kuwa bidhaa mikononi mwa wafanyabiashara wa kifo.

Mapato ya msingi kwa wote

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko alirejea wito wake wa Mapato ya Msingi kwa Wote ili kuhakikisha kwamba katika enzi ya mashine na Akili Mnemba, hakuna mtu anayenyimwa mahitaji ya kimsingi. Alisisitiza kwamba hiyo si huruma tu bali haki kali. Papa alionesha tumaini lake la kibinafsi kwa vizazi vijavyo kwamba : “Jinsi ninavyotamani kwamba vizazi vipya vipate ulimwengu bora zaidi kuliko ule ambao tumeupokea. Na akahitimisha kwa ujumbe wa tumaini kwamba: “Tumaini ndilo sifa dhaifu zaidi, lakini halikatishi tamaa kamwe.”

Papa na Harakati Maarufu kimataifa

 

20 September 2024, 17:32