Tafuta

Papa Francisko:Ni Makanisa ambayo hayaongoi watu bali yanakua kwa mvuto!

Papa akiwa katika Katekesi ya Septemba 18,amejikita juu ya ziara ya kitume hivi karibuni:Indonesia,Papua New Guinea,Timor ya Mashariki na Singapore.Amesisitizia kuwa Udugu ni siku zijazo.Ni jibu la kupinga ustaarabu wa njama za kishetani za chuki na vita.Hakuna ubinadamu mpya bila wanaume na wanawake wapya:Na ni Bwana pekee anayefanya haya.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 18 Septemba 2024, ametoa tafakari yake kwa mahujaji na waamini waliofika kutoka pande za Dunia wakiwa katika Uwanaja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, ambapo tafakari yake imehusu Ziara ya 45 ya  kitume ya kwenda nchini Indonesia, Papua, New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye Singapore kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024. Akianza Baba Mtakatifu alieelezea juu ya safari kiyo kuwa ilikuwa ni Ziara ya kitume ambayo haikuwa ya utalii bali kwenda kuepeleka Neno la Kristo na kushuhudia. Baadaye Papa aliendelea kueleza kuwa: “Leo nitazungumzia Ziara ya Kitume niliyoifanya huko Asia na Oceania. Paulo VI, mnamo mwaka wa 1970, alikuwa Papa wa kwanza kuruka kuelekea jua linakochomoza, akiwa na ziara ndefu katika Ufilipino na Australia, lakini alisimama pia katika nchi mbalimbali za Asia na katika Visiwa vya Samoa. Safari ya kukumbukwa!

Katekesi Papa, Septemba 18
Katekesi Papa, Septemba 18

Katika hili pia nilijaribu kufuata mfano wake lakini, kwa kuwa nilikuwa na umri mkubwa zaidi kuliko yeye kwa miaka michache, nilijiwekea mipaka kwa nchi nne: Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na Singapore. Ninamshukuru Bwana ambaye aliniruhusu kufanya kama Papa mzee kile ambacho ningependa kufanya nikiwa Mjesuit kijana! Baba Mtakatifu ameendelea akisema kwamba“ Tafakari ya kwanza ambayo huja kwa kawaida baada ya safari hii ni kwamba katika kulifikiria Kanisa, bado tuko katikati ya Ulaya, au kama wanasema, “magharibi.” Kiukweli, Kanisa ni kubwa zaidi na liko hai zaidi! Nilipitia haya kwa njia ya kusisimua kwa kukutana na jumuiya hizo, kusikiliza shuhuda za mapadre, watawa, walei na hasa makatekista. Makanisa ambayo hayaongoi watu, lakini yanakua kwa mvuto."

Nchini Indonesia:kuishi pamoja na huruma ni njia ya kutembea

Nchini Indonesia, takriban asilimia kumi ya watu ni Wakristo, na asilimia tatu ni Wakatoliki. Lakini nilichokutana nacho kilikuwa Kanisa changamfu, lenye nguvu, lenye uwezo wa kuishi na kueneza Injili katika nchi ambayo ina utamaduni wa hali ya juu sana, inayo mwelekeo wa kuoanisha utofauti, na wakati huohuo ina Waislamu wengi zaidi ulimwenguni.  Katika muktadha huo, nilipata uthibitisho kwamba huruma ndiyo njia ambayo Wakristo wanaweza na wanapaswa kutembea ili kushuhudia Kristo Mwokozi, na wakati huo huo kukutana na mila kuu ya kidini na kitamaduni. “Imani, udugu, huruma” ndiyo ilikuwa kauli mbiu ya ziara hiyo nchini Indonesia: katika msingi wa maneno haya, Injili inaingia kila siku katika maisha ya watu kwa namna halisi, ikiikaribisha na kuipa neema ya Yesu aliyekufa na kufufuka tena. Maneno haya ni kama daraja, kama njia ya chini inayounganisha Kanisa Kuu la Jakarta na Msikiti mkubwa zaidi barani Asia. Hapo, niliona kwamba udugu ni siku zijazo, ni jibu la kupinga ustaarabu, kwa njama za kishetani za chuki na vita.

Papua New Guinea:Makabila na lugha zaidi ya 800

Niligundua tena uzuri wa Kanisa la wamisionari lililokuwa nje ya nchi katika Papua New Guinea, funguvisiwa linaloenea kuelekea kwenye ukubwa wa Bahari ya Pasifiki. Huko, makabila mbalimbali yanazungumza lugha zaidi ya mia nane: mazingira bora kwa Roho Mtakatifu, ambaye anapenda kufanya ujumbe wa upendo usikike katika ulinganifu wa lugha. Hapo, kwa namna fulani, wahusika wakuu wamekuwa na bado ni wamisionari na makatekista. Nilifurahi kuweza kukaa kwa muda na wamisionari na makatekista wa siku hizi; na nilisukumwa kusikiliza nyimbo na muziki wa vijana: ndani yao, niliona mustakabali mpya, bila vurugu za kikabila, bila utegemezi, bila ukoloni wa kiuchumi au kiitikadi; mustakabali wa udugu na utunzaji wa mazingira ya asili ya ajabu. Papua New Guinea inaweza kuwa “maabara” ya kielelezo hiki cha maendeleo shirikishi, kilichochochewa na “chachu” ya Injili. Kwa sababu hakuna ubinadamu mpya bila wanaume wapya na wanawake wapya, na ni Bwana pekee anayefanya haya.

Timor ya Mashariki:kukua kwa ubinadamu na kijamii

Nguvu ya ujumbe wa Kikristo wa ukuzaji wa kibinadamu na kijamii inaonekana dhahiri katika historia ya Timor ya mashariki. Huko, Kanisa limeshiriki mchakato wa uhuru na watu wote, daima likiongoza kuelekea amani na upatanisho. Si suala la itikadi ya imani, hapana; ni imani ambayo inakuwa utamaduni na wakati huo huo kuiangaza, kuitakasa, kuinua. Hii ndiyo sababu nilizindua upya uhusiano wenye kuzaa matunda kati ya imani na utamaduni, ambao Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ameuelekeza katika ziara yake. Lakini zaidi ya yote, nilivutiwa na uzuri wa watu: watu ambao wamevumilia mengi lakini wanafurahi, watu wenye hekima katika mateso. Idadi ya watu ambayo sio tu huzaa watoto wengi, lakini pia inawafundisha jinsi ya kutabasamu. Na hii ni dhamana kwa siku zijazo. Kwa ufupi, huko Timor ya Mashariki niliona ujana wa Kanisa: familia, watoto, vijana, waseminari wengi na wanaotamani maisha ya kuwekwa wakfu. Nilipumua "hewa ya majira ya kuchipua"!

Singapore:tofauti na nchi nyingine tatu,utajiri

Kituo cha mwisho katika safari hii kilikuwa Singapore. Nchi tofauti sana na nchi nyingine tatu: Jiji-Taifa, la kisasa sana, nguzo ya kiuchumi na kifedha kwa Asia na kwingineko. Hapo, Wakristo ni wachache, lakini hata hivyo wanaunda Kanisa hai, linalojishughulisha na kukuza maelewano na udugu kati ya makabila, tamaduni na dini mbalimbali. Hata katika Singapore tajiri kuna “wadogo”, ambao wanafuata Injili na kuwa chumvi na mwanga, mashahidi wa tumaini kubwa kuliko yale ambayo faida za kiuchumi zinaweza kuhakikisha. Namshukuru Mungu kwa zawadi ya safari hii! Na ninarudia shukrani zangu kwa mamlaka ya kiraia na Makanisa ya mahali, ambao walinikaribisha kwa shauku kubwa. Mungu awabariki watu niliokutana nao, na awaongoze katika njia ya amani na udugu!

Katekesi ya Papa 18 Septemba 2024
18 September 2024, 11:09