Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 14 Septemba 2024 ameongoza Ibada ya Misa kwa ajili ya kumbuzi ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Mapadre  wa Theatines. Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 14 Septemba 2024 ameongoza Ibada ya Misa kwa ajili ya kumbuzi ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Mapadre wa Theatines.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kiteni Maisha Na Utume Wenu Katika: Upyaisho, Ushirika na Huduma

Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu alikazia mambo makuu matatu: Upyaisho wa maisha na utume wao; Ushirika na Huduma. Hili ni Shirika lililoanzishwa ili kujenga na kudumisha ushirika unaosimikwa katika maisha ya kijumuiya, huduma kwa Mungu na kwa jirani pamoja na kushiriki katika mchakato wa kupyaisha maisha na utume wa Kanisa mintarafu maisha ya waamini wa Kanisa la Mwanzo. Rej. Mk 3:13-15. Waiogope kubomoa kile ambacho hakifai kwa maisha na utume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Mapadre  wa Theatines “Ordo Clericorum Regularium Vulgo Theatinorum, CP.” lilianzishwa na Mtakatifu Gaetano Thiene na Giampietro Caraffa, Askofu wa Chieti na Brindisi ambaye baadaye alikuja kuchaguliwa kuwa Papa Paul IV, kunako tarehe 14 Septemba 1524, Mwaka 2024 wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 500 tangu kuanzishwa kwao. Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba tarehe 14 Septemba 2024, Wanashirika hawa walifanya hija ya maisha ya kiroho mjini Vatican na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican akaadhimisha Ibada ya Misa Misa Takatifu kwa nia hii, na baadaye wakakutana na Baba Mtakatifu Francisko. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu alikazia mambo makuu matatu: Upyaisho wa maisha na utume wao; Ushirika na Huduma. Hili ni Shirika lililoanzishwa ili kujenga na kudumisha ushirika unaosimikwa katika maisha ya kijumuiya, huduma kwa Mungu na kwa jirani pamoja na kushiriki katika mchakato wa kupyaisha maisha na utume wa Kanisa mintarafu maisha ya waamini wa Kanisa la Mwanzo. Rej. Mk 3:13-15.

Jubilei ya Miaka 500 tangu kuanzishwa Shirika la Theatines
Jubilei ya Miaka 500 tangu kuanzishwa Shirika la Theatines

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha kwamba, Mapadre wa kwanza wa Shirika lao, waliweka nadhari zao kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, kama lilivyokuwa kunako mwaka 1524, wakati huo, kulikuwa kunafanyika ukarabati mkubwa kwa kusoma alama za nyakati na ili kukidhi mahitaji ya watu wa Mungu kwa nyakati hizo. Ukarabati huu ulifanyika kwa kusuasua, kutokana na ukata wa fedha na wala hakukuwepo na uwazi katika utekelezaji wa mradi huu mkubwa. Hii ni changamoto kwa Mapadre hawa kuendelea kusimama kidete katika amana na utajiri wa Mapokeo yao; kwa kujikita katika ujasiri tayari kushiriki mchakato wa upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa. Wawe tayari kubomoa kile ambacho hakifai tena kwa maisha na utume wa Shirika lao. Rej. Lk 5: 36-39 kwani divai mpya sharti itiwe katika viriba vipya na huu ndio mchakato wa upyaisho wa maisha na utume wa Shirika hili ndani ya Kanisa.

Papa Francisko: Upyaishaji, Ushirika na Huduma kwa Mungu na Jirani
Papa Francisko: Upyaishaji, Ushirika na Huduma kwa Mungu na Jirani

Ukarabati wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ni kazi iliyofanywa na umati mkubwa wa watu waliochangia ujuzi, ufahamu na maarifa yao, katika hali ya unyenyekevu, upendo, umoja na mshikamano wa dhati na matokeo yake ni mwonekano wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwa sasa. Kumbe, huu ni mwaliko kwa Mapadre kushirikiana kikamilifu na watu wa Mungu katika Jumuiya kwa kuthamini mchango wa kila mtu, ili kukuza na kudumisha umoja na ushirika wa Kanisa. Rej. I Kor 12:7-11. Watambue kwamba, viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja na kwamba, kuna tofauti ya karama, lakini zote muasisi wake ni Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa unaosimikwa katika umoja na ushirika, pamoja na mambo mengine unapania kutoa huduma kwa watu wa Mungu. Hii ni huduma inayosimikwa katika unyenyekevu, utashi na moyo wa sadaka na majitoleo. Matendo ya huruma kiroho na kimwili, yaliyoasisiwa na Kristo Yesu, bado yako hai hadi leo hii. Kristo Yesu anasema, hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi. Rej. Mk 10:45. Shirika la Mapadre  wa Theatines “Ordo Clericorum Regularium Vulgo Theatinorum, CP.” lilianzishwa wakati wa Sikukuu ya Kutukuka Kwa Msalaba. Jengo la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ni alama, lakini muhimu ni waamini. Ni katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 tangu kuanzishwa kwa Shirika hili, bado linaendelea kuishi, alama wazi ya mawe hai, ambayo yametumika katika ujenzi wa Kanisa, Mchumba wa Kristo Yesu. Rej. 1 Pet 2: 4-5 na kwamba Kristo ndiye msingi wa Kanisa na wao wanawajibika kutoa dhabihu ya roho. Kanisa ni Shamba la Mungu, Yerusalemu ya juu, Mama yetu; Kanisa ni mwili wa Kristo Yesu; hili ni Kanisa linaloonekana na lile lisilo onekana. Hili ni Kanisa moja, takatifu, katoliki na la Mitume. Rej. LG 6-9.

Sanamu ya Mtakatifu Gaetano Thiene imerejeshwa tena mjini Vatican.
Sanamu ya Mtakatifu Gaetano Thiene imerejeshwa tena mjini Vatican.

Baba Mtakatifu amewakumbusha Mapadre hawa kwamba, baada ya karne tano zilizopita, sasa Shirika limewekwa mikononi mwao. Amewashukuru na kuwapongeza mapadre wote kwa sadaka na majitoleo yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo! Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 14 Septemba 2024 ameongoza Ibada ya Misa kwa ajili ya kumbuzi ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Mapadre  wa Theatines “Ordo Clericorum Regularium Vulgo Theatinorum, CP” kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Sanamu ya Mtakatifu Gaetano Thiene imerejeshwa tena kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hii ni Sanamu iliyochongwa na Msanii Carlo Damian na kukamilika kunako mwaka 1885, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 tangu kuanzishwa kwa kwa Shirika la Mapadre  wa Theatines “Ordo Clericorum Regularium Vulgo Theatinorum, CP.”

Jubilei Miaka 500
17 September 2024, 14:27