Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 23 Septemba 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 23 Septemba 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Sayansi Itumike Kukuza na Kudumisha Utu, Heshima na Ubinadamu!

Papa tarehe 23 Septemba 2024 amekutana na wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi. Amekazia: Sayansi, kimsingi inapaswa kutumia ujuzi na maarifa kukuza na kudumisha utu, heshima na ubinadamu katika ujumla wake. Teknolojia ya akili mnemba inaweza kuwa na manufaa makubwa katika sekta ya afya; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na kuwezesha matumizi endelevu ya rasilimali za dunia kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, mnamo tarehe 11 Februari 1994, katika Barua binafsi “Motu proprio” ya “Vitae mysterium” yaani “Fumbo la maisha anasema, lengo la taasisi hii ni kusimama kidete kulinda na kutetea thamani ya maisha na utu wa binadamu mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Taasisi hii ina dhamana ya kutafiti, ili hatimaye, kuunda utamaduni wa maisha dhidi ya utamaduni wa kifo na kuhabarisha wadau mbalimbali changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai duniani! Taasisi hii ina dhamana na wajibu wa kufanya tafiti za kitaaluma na kisayansi, ili kusaidia kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha maisha ya binadamu. Ina kazi maalum ya kusaidia kuwafunda waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika utamaduni wa maisha mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Ni wajibu wa taasisi katika hali ya uwazi na kwa haraka, inapaswa kuwajulisha viongozi wa Kanisa, taasisi za elimu maumbile na sayansi ya biolojia ya binadamu; taasisi za kiafya; vyombo vya mawasiliano ya jamii na jumuiya za kiraia kuhusu shughuli na tafiti zake kama sehemu ya mchakato wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Sayansi itumike kukuza utu, heshima na ubinadamu katika ujumla wake
Sayansi itumike kukuza utu, heshima na ubinadamu katika ujumla wake

Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii inawajibika kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu, utu na heshima yake, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu pamoja na kudumisha heshima kati ya vizazi. Wasiwasi mkubwa umetanda juu ya uso wa nchi kutokana na athari kubwa ya binadamu kwa asili na mifumo ya kiikolojia. Mwanasayansi Paul Crutzen, katika kuelezea athari hii katika kazi ya uumbaji wametajwa kwa pamoja kama wanaounda “Enzi ya Anthropocene.”Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 23 Septemba 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi. Katika hotuba yake amesema: Sayansi, kimsingi inapaswa kutumia ujuzi na maarifa kukuza na kudumisha utu, heshima na ubinadamu katika ujumla wake. Teknolojia ya akili mnemba inaweza kuwa na manufaa makubwa katika sekta ya afya; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na kuwezesha matumizi endelevu ya rasilimali za dunia kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi. Baadhi ya wajumbe wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii walikuwa ni miongoni mwa wataalamu wa kwanza kubainisha athari za shughuli za binadamu zinazoendelea kuongezeka katika kazi ya Uumbaji kwa kusoma hatari na matatizo yanayoambatana nazo.

Kuna athari kubwa ya binadamu katika mifumo ya kiikolojia
Kuna athari kubwa ya binadamu katika mifumo ya kiikolojia

“Anthropocene” kwa kweli inafichua na matokeo yake yanayozidi kuwa makubwa kwa asili na wanadamu, haswa katika athari za mabadiliko ya tabianchi na upotezaji wa bioanuwai. Taasisi hii ya Kipapa inaendelea kujikita katika masuala kama haya, hasa kwa kuzingatia umuhimu wake kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Sayansi, kimsingi inapaswa kutumia ujuzi na maarifa kukuza na kudumisha utu, heshima na ubinadamu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, dunia inakabiliwa na changamoto kubwa za kijamii, kisiasa na kimazingira, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, katika majadiliano ya hadhara vipengele vyote vya maisha ya kijamii vijumuishwe, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: maskini na waliotengwa, pamoja na kuwashirikisha wazawa na busara zao katika mijadala hii. Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii katika Mkutano wake wa mwaka 2024 unazingatia maarifa na ubunifu mpya unaoibuka pamoja na fursa zinazohusiana na sayari hii pamoja na ubora wake. Nafasi ya binadamu katika maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba lazima yapewe kipaumbele cha kwanza, ili maendeleo haya yaweze kuleta usawa, ustawi na maendeleo ya kijamii.

Matumizi ya teknolojia ya akili mnemba
Matumizi ya teknolojia ya akili mnemba

Teknolojia ya akili mnemba ni chombo chenye nguvu sana, kinachopaswa kutumika kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema! Teknolojia ya akili mnemba inaweza kuwa na manufaa makubwa katika sekta ya afya; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na kuwezesha matumizi endelevu ya rasilimali za dunia kwa kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa. Lakini teknolojia ya akili mnemba inaweza kuwa na madhara yake makubwa kwa watu, kumbe, kuna haja ya kuwa makini kwa kutambua athari za matumizi ya tekanolojia ya akili mnemba, katika kukuza na kudumisha demokrasia hasa nyakati za michakato ya uchaguzi. Kumbe, kanuni maadili na utu wema ni mambo yanayopewa kipaumbele cha kwanza kama msingi wa maendeleo ya teknolojia mpya kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya maisha ya watu, kwa kusimama kidete katika usawa na suluhu, kama sehemu ya maendeleo ya kweli ya binadamu. Matumizi ya teknolojia ya akili mnemba lazima yaangalie athari kwa watu binafsi na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwa makini zaidi katika tafiti zake. Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii iko mstari wa mbele kupendekeza sheria ili kuzuia hatari na kukuza faida katika uwanja wenye utata! Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, vita na vitisho kwa usalama wa Jumuiya ya Kimataifa vinaonekana kutawala, lakini mchango wa wataalamu ni muhimu katika mchakato wa kuendeleza ujuzi na maarifa katika huduma ya familia ya binadamu, ili kukuza na kudumisha amani, umoja na ushirikiano wa Kimataifa.

Taasisi ya Kipapa
23 September 2024, 15:27