Papa kwa vijana wa Pwani ya Amalfitana:Tuna silaha nzuri,maombi!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika fursa ya Mkutano wa Vijana wa Pwani ya Amalfitana huo Scala nchini Italia, unaongozwa na mada: “Vyombo vya amani,” Baba Mtakatifu Francisko aliwatumia ujumbe wake. Katika ujumbe huo, Papa anandika kuwa: “Wapendwa vijana wa Pwani ya Amalfitana ninayo furaha kuwahutubia ninyi mnaoshiriki katika mkutano wa "Vyombo vya Amani" katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Lorenzo huko Scala. Ninawasalimu, Askofu Mkuu wa Amalfi-Cava de' Tirreni, AskofuOrazio Soricelli, Mameya, Taasisi na Mamlaka zilizopo. Vijana wapendwa, mmechagua mada nzuri! Ni udharura tunao upata wakati wa vita na watu wengi wanaopoteza maisha kila siku, watoto, wazee, vijana, wanaume na wanawake. Yesu yu hai na anataka muwe hai! Bila amani hakuna maisha. Kuna kifo na uharibifu tu.”
Angazeni Ishara ya huduma, huruma na msamaha
Baba Mtakatifu katika ujumbe huo anabainisha kuwa: "Kuna njia tatu za uhakika za kuwa vyombo vya amani: kwanza “Kujaza siku kwa ishara za amani. Katika mji huu wa kale wa Scala mnaweza kuzama zaidi katika njia ya mshikamano na mazungumzo yaliyoanzishwa na Mwenyeheri Ndugu Gerardo Sasso, mwanzilishi na Mkuu wa kwanza wa Shirika la Kijeshi la Malta. Katika enzi ya migogoro ya vita aliunda hospitali ya kwanza ya kidini huko Yerusalem, karibu 1100 AD. Ninyi pia, mkifuata mfano wake, mnaweza kujenga madaraja ya urafiki na mshikamano wa pande zote. Angazeni kila saa ya siku zenu kwa kufanya ishara ya amani: ishara ya huduma, ya huruma, ya msamaha."
Ombeni kwa ajili ya amani
Pili Baba Mtakatifu Francikso anawashauri kwamba: “Ombeni kwa moyo wenu kwa ajili ya amani. Tunapohisi kutokuwa na uwezo katika kukabiliana na matukio ya ajabu ya ulimwengu, tukumbuke kwamba "Hakuna lisilowezekana kwa Mungu” (Lk 1:37). Tuna silaha nzuri sana ambayo ni maombi. Wacha tuitumie! Tuombe zaidi amani, ili ifike upesi.” Hebu tuombe kwa imani na uaminifu! Hebu tufanye ahadi ya kila siku kwa maombi ya kibinafsi ya amani. Tuwe pamoja ili kushiriki nyakati za kuabudu Ekaristi mbele ya Bwana, Mfalme wa amani."
Vita daima ni kushindwa kwa binadamu
Jambo la Tatu, ambalo Baba Mtakatifu anahimiza ni kuwa "waishi kama mahujaji wa matumaini." Kwa ujasiri, wasichoke kuota"amani na udugu tu, kwa sababu hii pia ni ndoto ya Baba: kwamba watoto wake wawe na umoja na furaha, wakitambua kuwa sisi sote ni kama ndugu." Papa amekazia kwamba Watazame zaidi ya usiku! kwa sababu "Wasikubali kuwa na mawazo kwamba vita "vinaweza kutatua matatizo na kuleta amani. Vita daima ni kushindwa, kujisalimisha kwa aibu mbele ya nguvu za uovu. Wacha tukumbuke waathiriwa wote, ambao hatupaswi kamwe kuwasahau na kumbukumbu hii itatufungua kwa hakika kutafuta njia ya kutoka kwa sasa kwenye njia ya upatanisho.” Na hatimaye Baba Mtakatifu ameandika kuwa “Nikiwakabidhi kwa maombezi ya mama Maria, Malkia wa Amani, ninawabariki na kuwaomba, tafadhali, mniombee.”