Jumuiya ya Mtakatifu Egidio iliandaa "Mkutano wa Amani' huko Paris nchini Ufaransa  kuanzia 22-24 Septemba 2024. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio iliandaa "Mkutano wa Amani' huko Paris nchini Ufaransa kuanzia 22-24 Septemba 2024. 

Papa kwa Washiriki wa Mkutano wa amani:tuko katikati ya mabadiliko ya nyakati!

Papa aliwatumia washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa amani uliofanyika jijini Paris 22-24 Septemba 2024:“Matukio mengi yameathiri ulimwengu wetu tangu 1986:kuanguka kwa Ukuta wa Berlin,mwanzo wa Milenia ya Tatu,kuenea kwa itikadi kali,kuzuka kwa migogoro na athari za kimataifa,changamoto za mabadiliko ya tabianchi,ujio wa teknolojia zinazoibuka na kubadilika na magonjwa ya milipuko yaliyoathiri ubinadamu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko aliwatumia Washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Amani ulioandaliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kwa kushirikiana na Jimbo Kuu la Paris, nchini Ufaransa, ulioanza tangu tarehe 22 hadi 24 Septemba 2024. Baba Mtakatifu katika ujumbe huo alianza kuonesha furaha ya kuwasalimia kaka na dada wote wapendwa, wawakilishi wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo na za dini kuu za ulimwengu, pamoja na mamlaka ya kiraia waliokuwapo. Alishukuru Jumuiya ya Mtakatifu 'Egidio kwa ari na ubunifu ambao kwayo wanaendelea kuweka ari hai ya Assisi. Miaka thelathini na minane imepita tangu mwaka 1986, wakati Mkutano wa kwanza wa Amani ulipofanyika. Baba Mtakatifu Francisko alikazia kuwa “Matukio mengi yameathiri ulimwengu wetu tangu wakati huo kuanzia na kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, mwanzo wa Milenia ya Tatu, kuenea kwa itikadi kali na kuzuka kwa migogoro na athari za kimataifa, bila kusema chochote juu ya changamoto zinazoletwa na mabadiliko ya tabianchi, ujio wa teknolojia zinazoibuka na zinazobadilika, na magonjwa ya milipuko ambayo yameathiri ubinadamu. Kiukweli, tuko katikati ya “mabadiliko ya nyakati,” bila kuwa na... kwa sasa, na wazo wazi la wapi yatatuongoza.” Papa aliongeza: “Hata hivyo, kila mwaka, kama wawakilishi wa dini kuu za ulimwengu na wanaume na wanawake wenye mapenzi mema, mmesafiri kama mahujaji kwenye majiji mbalimbali katika Ulaya na ulimwenguni pote, ili kudumisha uhai wa roho ya Assisi.”

Uhusiano wa ndani kati ya dini na wema wa amani ni dhahiri

Baba Mtakatifu amebainisha kwamba: “Kwa kufanya hivyo, tukumbushwa changamoto ambayo mtangulizi wangu, Mtakatifu Yohane Paulo II, alirejea katika maneno yake mwishoni wa siku hiyo ya kukumbukwa. “Labda zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika historia,” yeye akadokeza, “uhusiano wa ndani kati ya mtazamo wa kidini wa kweli na wema mkuu wa amani umekuwa dhahiri kwa wote... Kwa pamoja tumejaza mitazamo yetu maono ya amani: yanaachilia nguvu kwa lugha mpya ya amani, kwa ishara mpya za amani, ishara ambazo zitavunja minyororo mbaya ya migawanyiko iliyorithiriwa kutoka katika historia au iliyosababishwa na itikadi za kisasa. Amani inawangoja wajenzi wake”. Roho ya Assisi ni baraka kwa ulimwengu wetu huu, ambao bado umekumbwa na vita na vitendo vingi vya jeuri. "Roho" ya Assisi lazima ivume kwa nguvu zaidi katika matanga ya mazungumzo na urafiki kati ya watu.

Acheni vita! Sasa tunaharibu dunia!

Papa Francisko amesema kwamba mwaka huu wamekutana mjini Paris, ambapo na jioni  ya tarehe 24 Septemba 2024  walikusanyika mbele ya Kanisa Kuu ambalo, baada ya moto wa kutisha, linakaribia kufunguliwa tena milango yake kwa sala. Papa ameongeza: “Ni jinsi tunavyohitaji kuomba kwa ajili ya amani!” Hatari kwamba migogoro mingi katika ulimwengu wetu, badala ya kukoma, inaenea kwa hatari na ni ya kweli sana." Kwa njia hiyo: “Ninaungana na sauti yangu kwa ombi lenu na la waathiriwa wote wa vita, katika kuwasihi viongozi wa kisiasa: “Acheni vita! Acheni vita!” Sasa tunaharibu dunia! Wacha tusimame wakati bado!”

Waamini wagundue upya wito wa kukuza udugu kati ya watu

Papa alisisitiza kuwa “Mkutano huu uwahimize waamini wote kugundua tena wito wao wa kukuza udugu kati ya watu katika wakati wetu. Mara nyingi sana zamani, dini zilitumiwa kuchochea mizozo na vita. Hatari ya hii inaendelea, hata katika siku zetu wenyewe. Niruhusu nirudie tena imani niliyoieleza pamoja na Imamu Mkuu Ahmad Al-Tayyeb: “Dini kamwe zisichochee vita, mitazamo ya chuki, uadui na misimamo mikali, wala zisichochee vurugu au umwagaji wa damu. Mambo haya ya kutisha ni matokeo ya kupotoka kutoka katika mafundisho ya kidini.” Vita vinatokana na upotoshaji wa kisiasa wa dini na tafsiri zilizofanywa na vikundi vya kidini ambavyo, katika kipindi cha historia, vimechukua fursa ya hisia za kidini katika mioyo ya wanaume na wanawake”. Ni lazima tuzuie dini zisikubali jaribu la kuwa njia ya kuchochea aina za utaifa, ukabila na ushabiki. Vita vinazidi tu. Ole wao wanaojaribu kumvuta Mungu ili wajiunge na vita!

Kazi ya dharura ya dini ni kukuza maono ya amani

Baba Mtakatifu alibanisha kuwa “Kazi ya dharura ya dini ni kukuza maono ya amani, kama walivyoonesha siku hizo huko Paris. Kama wanaume na wanawake wa tamaduni tofauti na imani za kidini, wamepata uzoefu wa nguvu na uzuri wa udugu wa ulimwengu wote. Haya ndiyo maono ambayo ulimwengu wetu unahitaji leo. Papa kwa njia hiyo aliwahimiza wavumilie katika juhudi zao za kuwa mafundi wa amani. Ikiwa wengine wataendelea kufanya vita, pamoja tunaweza kufanya kazi kwa ajili ya  amani. Katika Waraka wa Kitume wa a Fratelli Tutti, Papa amesisitiza kuwa aliwahimiza waamini “kuchangia pakubwa katika kujenga udugu na kutetea haki katika jamii. Mazungumzo baina ya wafuasi wa dini mbalimbali hayafanyiki kwa ajili ya diplomasia tu, kuzingatia au kuvumiliana. Kwa maneno ya Maaskofu wa India, ‘lengo la mazungumzo ni kuanzisha urafiki, amani na maelewano, na kushirikishana tunu za kiroho na kimaadili na mang’amuzi katika roho ya ukweli na upendo.’” Ni kutokana na hali hii ambapo jina la Mkutano huo wa Paris  uliojikita na mada “Fikiria Amani” ni fasaha zaidi.” 

Mungu ametukabidhi sisi sote jukumu la kuwatia moyo washiriki wa familia

Tunahitaji kuendelea kukutana, kusuka vifungo vya udugu na kujiruhusu kuongozwa na maongozi ya kimungu yaliyo katika kila imani, ili kujiunga katika “kuwazia amani” kati ya watu wote. Tunahitaji “nyakati kama hizo kuzungumza sisi kwa sisi na kutenda pamoja kwa manufaa ya wote na hamasisha maskini.” Katika ulimwengu ulio katika hatari ya kugawanyika na migogoro na vita, juhudi zinazofanywa na waamini ni muhimu sana kwa ajili ya kuweka maono ya amani na kukuza udugu na amani kati ya watu kila mahali. Wawakilishi mashuhuri wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo na wa dini kuu za ulimwengu, wanaume na wanawake wenye mapenzi mema ambao walishiriki katika Mkutano huu, Papa alisema "Leo, hata zaidi ya hapo awali, jukumu kubwa la amani limewekwa mikononi mwenu. Hili linadai kwa upande wetu hekima, ujasiri, ukarimu na uamuzi. Mungu ameweka pia mikononi mwetu ndoto yake kwa ulimwengu: udugu kati ya watu wote. Katika Hati zote za Baba Mtakatifu  za: Laudato Sì na Fratelli Tutti, “niliwazia” mustakabali wa ulimwengu wetu huu: nyumba moja (sayari yetu) na familia moja (ile ya watu wote). Mungu ametukabidhi sisi sote jukumu la kuwatia moyo na kuwaongoza washiriki wa familia yetu ya kibinadamu kuishi pamoja kwa udugu na amani.

Ujumbe wa Papa kwa Mkutano wa amani huko Paris
25 September 2024, 15:38