Papa na Harakati ya Wanafunzi Katoliki Pax Romana:kuwa wahusika wakuu wa mapinduzi ya upendo na huduma
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Ijumaa tarehe 20 Septemba 2024, Baba Mtakatifu amekutana na washiriki wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wanafunzi Wakatoliki ‘Pax Romana’ na kuwapa salamu wote pamoja na marafiki na familia zao na kuwashukuru kwa uwepo wao. “Ninathamini sana kujitolea kwenu kukuza haki ya kijamii na maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuchochewa na imani yenu ya Kikatoliki na maono yake ya ulimwengu unaopatana zaidi na mpango wa upendo wa Mungu kwa ajili ya familia yetu ya kibinadamu.", alisema Papa Francisko. "Kufuatia tafakari ya Sinodi ya Kanisa kuhusu Vijana ya 2018, Papa ameongeza kusema “niliwahimiza vijana hasa kuwa “wahusika wakuu wa mapinduzi ya upendo na huduma” (Christus Vivit, 174). Uwepo wenu na shughuli zenu ziwe katika mazingira ya kitaaluma, mahali pa kazi au mitaa ya jiji, itumikie lengo hili kwa kufanya kazi ili kuchora ulimwengu wa huruma zaidi, usawa na wa kidugu."
Papa Francisko amefikiria "kwa mfano, kazi ya elimu na mafunzo ya uongozi iliyofanywa katika vituo vyao mbalimbali nchini Ufaransa, Thailand na Kenya, vyenye msingi katika ushuhuda wa Injili na kujitolea kwa mafundisho ya kijamii ya Kanisa. Kwa kukuza hisia za uraia wa kimataifa na hatua za kutia moyo katika ngazi mahalia, Harakati yao inawawezesha vijana sio tu kuongeza uelewa wao wa masuala muhimu ya kijamii ya wakati wetu, lakini pia kuwapa uwezo wa kukuza mabadiliko yenye matokeo ndani ya jumuiya zao, hivyo kufanya kazi kama chachu halisi ya Injili." Papa amesema kuwa "Katika siku hizi, tunaposonga mbele na Sinodi ya sasa ya Sinodi, amependa “kuwatia moyo, kama watu binafsi na kwa pamoja, kushiriki kikamilifu katika safari nzima ya sinodi ya Kanisa ya “kutembea pamoja”, kusikiliza, kushiriki na kujihusisha katika mazungumzo ya wazi na ya utambuzi, ili kuwa makini kwa sauti tulivu ya Roho Mtakatifu.”
Papa aidha amewahimiza “kukaribisha adhimisho lijalo la Mwaka Mtakatifu wa 2025 kama fursa adhimu ya kufanywa upya kibinafsi na kujitajirisha kiroho katika muungano na Kanisa zima. Alama fasaha ya Mlango Mtakatifu ambao waamini hupitia, hapa Roma na katika Makanisa yote mahalia, inatukumbusha kwamba sisi sote ni mahujaji tukiwa safarini, tunaitwa pamoja ili kuungana kwa undani zaidi na Bwana Yesu na kufunguka kwa uwezo wa Kristo, neema ya kubadilisha maisha yetu na ulimwengu tunamoishi.”
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba uwepo wao mjini Roma na mkutano wao hapo na Papa utakuwa chanzo cha msukumo mpya kwa juhudi zao za “kufanya kazi kwa ajili ya ukuaji wa amani, maelewano, haki, haki za binadamu na huruma, na hivyo upanuzi wa ufalme wa Mungu katika ulimwengu huu”(Christus Vivit, 168). Amewapongeza wote kwa sala za Maria, Malkia wa Amani,na Mwenyeheri Giorgio Frassati, ambaye amesema “ninatarajia kumwaandikisha miongoni mwa watakatifu katika Mwaka Mtakatifu ujao. Ninawaombea ninyi nyote baraka za Bwana za hekima, furaha na amani ya kudumu.” Papa Francisko amehitimisha.