Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 31 Agosti 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa 86 wa Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko Wakapuchini “OFM.Cap. Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 31 Agosti 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa 86 wa Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko Wakapuchini “OFM.Cap.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko Wakapuchini: Udugu, Uwepo na Amani

Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 31 Agosti 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa 86 wa Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko Wakapuchini “OFM.Cap. Katika hotuba yake amewataka Wakapuchini kuwa ni wajumbe na vyombo vya haki na amani; wakijizatiti zaidi kuwa karibu na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Amekazia ujenzi wa udugu wa kibinadamu, uwepo katika huduma na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko Wakapuchini “OFM.Cap. lilianzishwa rasmi mnamo mwaka 1528. Hili ni tawi mojawapo la familia tatu za Shirika la kwanza la Mtakatifu Francisko wa Assisi. Watawa 173 kutoka katika nchi zaidi ya 100 wa Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko Wakapuchini kuanzia tarehe 25 Agosti hadi tarehe 15 Septemba 2024 wanashiriki katika Mkutano mkuu wa 86 wa Shirika; huku watawa wengine 45 wakitoa huduma mbalimbali kwenye Mkutano mkuu. Hii ni tafakari ya Wakapuchini katika kipindi cha miaka 6 ili kuangalia: matatizo, changamoto, fursa na matarajio yao kwa siku za usoni. Mkutano huu unanogeshwa na kauli mbiu “Bwana alinipatia ndugu, ili kwenda ulimwenguni.” Mikutano mikuu ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume inayoadhimishwa wakati huu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ni muhimu sana katika maisha na utume wa kila Shirika ili kulinda, kutunza na kuendeleza karama za waanzilishi wa Mashirika haya. Huu ni muda muafaka wa kujenga utamaduni wa kusikilizana; kuchunguza na kusoma ishara za nyakati na kuzifafanua katika mwanga wa Injili, ili kubaini masuala yenye uzito zaidi katika ulimwengu mamboleo. Rej, Gaudium et spes, 4. Ni wakati wa kufanya tafakari ya kina kuhusu: mang’amuzi, majiundo na Injili ya upendo. Huu ni muda uliokubalika kwa kila mwanashirika kujikita katika mchakato wa upyaisho wa maisha yake binafsi na ule wa kijumuiya, tayari kuzama katika maendeleo ya Shirika kwa sasa na kwa siku usoni. Tangu mwanzo wa Kanisa wamekuwepo watu kwa kutekeleza mashauri ya Injili walinuia kumfuasa Kristo Yesu kwa hiari zaidi na kumwiga kwa karibu, walienenda, kila mmoja kwa jinsi yake, katika maisha ya wakfu kwa Mungu ambao unapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo, na unaojitoa na kujisadaka kabisa kwa Mungu na kwa msukumo wa Roho Mtakatifu, wanaamua kumfuata Kristo Yesu kwa karibu zaidi kwa kujisadaka na kuonesha upendo kwa Mungu, anayepaswa kupendwa kuliko vitu vyote. Rej. Perfectae caritatis, 1 na KKK, 916.

Wakapuchini kipaumbele: haki na amani; maskini; uwepo katika huduma
Wakapuchini kipaumbele: haki na amani; maskini; uwepo katika huduma

Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni kipindi maalum cha watawa kukutana katika: Sala, tafakari na mang’amuzi ya kina mintarafu amana na utajiri wa mashirika na wanashirika wenyewe. Ni wakati muafaka kwa wanashirika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu maisha na utume wa mashirika yao, kwa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zilizopo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda baada ya mikutano yao mikuu. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, watawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake tayari kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 31 Agosti 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa 86 wa Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko Wakapuchini “OFM.Cap. Katika hotuba yake amewataka Wakapuchini kuwa ni wajumbe na vyombo vya haki na amani; wakijizatiti zaidi kuwa karibu na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Baba Mtakatifu anasema, Wakapuchini ni waungamishaji wazuri, wanaojitahidi ku mwilisha huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya waamini na kwamba, maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Shirika ni muda maalum kwa Shirika na Kanisa katika ujumla wake, kwani mkutano huu unawashirikisha Wakapuchini kutoka katika Mataifa, tamaduni na lugha mbalimbali, ili kusikilizana na hatimaye, kuzungumza lugha moja ya Roho Mtakatifu sanjari na kushirikishana mambo makuu ya Mungu katika maisha na utume wao. Rej. Zab 125:3.

Wakapuchini dumisheni udugu wa kibinadamu, umoja na ushirika
Wakapuchini dumisheni udugu wa kibinadamu, umoja na ushirika

Mwenyezi Mungu anaendelea kutenda kazi zake kupitia kwa Watoto wa Mtakatifu Francisko, waliotawanyika sehemu mbalimbali za dunia. Huu ni wakati wa kumshukuru na kumtukuza Mungu kutokana na kukua na kupanuka kwa Shirika, hasa kwa kuwa na mvuto kwa vijana wa kizazi kipya. Hii ni changamoto na mwaliko wa kuendelea kutangaza na kushuhudia ujenzi wa Ufalme wa Mungu huku wakifuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake mintarafu mang’amuzi na utume wa kimisionari amekazia kuhusu: Ujenzi wa udugu wa kibinadamu; uwepo wao katika huduma na dhamana ya kutafuta na kudumisha amani. Mkutano huu unanogeshwa na kauli mbiu “Bwana alinipatia ndugu, ili kwenda ulimwenguni.” Hii ni tema inayokazia umuhimu wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ushirikiano na mshikamano wa dhati ili kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha na utume wao. Huu ni mwaliko wa kujikita katika Injili ya upendo, umoja na ushirika kwa kutambua kwamba, kila mmoja wao ni zawadi kwa mwingine. Umoja huu ni amana na utajiri wa Shirika zima na kwamba, wanapaswa kutambuana kuwa ni ndugu katika imani kwa kujikita katika malezi na majiundo makini ya Wakapuchini watakao kuwa na msimamo thabiti kwa siku za usoni. Kiini cha maisha na utume wao ni binadamu na haki zake msingi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na wokovu wa roho zao.

Wakapuchini vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho
Wakapuchini vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho

Ujenzi wa udugu wa kibinadamu ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na kwamba, huu nndio msingi wa maisha na utume wao. Ujenzi wa udugu wa kibinadamu unapaswa kusimikwa katika utayari wa kwenda mahali popote kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na hapa utayari huu unapaswa kusimikwa katika Injili ya upendo, imani na matumaini lakini lililo kuu ni upendo. Rej. 1Kor 13:13. Huu ni mwaliko wa kujenga Jumuiya ya Kimisionari, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kuwaheshimu na kuwathamini maskini sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Wakapuchini wawe tayari kutumwa mahali popote ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kukumbatia na kuambata ufukara wa Kiinjili. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Wakapuchini kujizatiti katika kutafuta, kujenga na kudumisha Injili ya haki na amani; wawe ni vyombo, mashuhuda na wajenzi wa amani na wapatanishi. Mt. 5:9. Watengeneze fursa za kuwakutanisha watu; kutafuta suluhu ya matatizo na changamoto zinazowakabili wale wanaowahudumia; wawe ni mashuhuda wa upatanisho hata katika mazingira ambazo ni magumu na hatarishi, kwa kutambua kwamba, wao ni wa Kristo Yesu na majirani wa wote Rej. Lk 10: 25-37 lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; watambulikane kama “mashuhuda wa amani.”

Wakapuchini Jengeni Jumuiya ya Kimisionari ili kutangaza Injili
Wakapuchini Jengeni Jumuiya ya Kimisionari ili kutangaza Injili

Mtakatifu Francisko wa Assisi aliweza kujikubali na kujipokea na katika hali yake ya ufukara akakutana na Kristo Yesu, Mkombozi wake! Akawa ni chombo cha upendo na upatanisho, kwa sababu upendo unabeba ndani mwake Injili ya upatanisho inayojenga na kudumisha ujirani mwema. Rej. Evangelii gaudium, 49. Hii ni hija inayokita mizizi yake katika imani na matumaini na kwamba, Bikira Maria awalinde na kuwasindikiza katika maisha na utume wao. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza Watawa wa Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko Wakapuchini “OFM.Cap. kwa mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa.

Wakapuchini 2024
03 September 2024, 13:32