Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 23 Septemba 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa Kipapa wa Utamaduni wa Elimu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 23 Septemba 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa Kipapa wa Utamaduni wa Elimu,   (Vatican Media)

Tamasha la Muziki wa Noeli Kwa Mwaka 2024: Utukufu Kwa Mungu Juu Na Amani Duniani

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 23 Septemba 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa Kipapa wa Utamaduni wa Elimu, kwa namna ya pekee kabisa amewapongeza na kuwashukuru vijana wa kizazi kipya wanaowekeza karama na mapaji yao kwa ajili ya nyimbo za Noeli, kama kielelezo cha ukuaji wa kiutu, changamoto kwa vijana kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa ajili ya utukufu na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa Kipapa wa Utamaduni wa Elimu “Fondazione Pontificia Gravissimum Educationis – Cultura per l’Educazione”, kwa mara nyingine tena umeandaa Tamasha la Noeli kwa mwaka 2024 linalohusisha nyimbo za zamani ambazo zimegeuzwa kuwa ni sehemu ya sala za waamini na ziliimbwa kwa kichwa! Hata katika ulimwengu mamboleo, zile nyimbo zinazopendwa sana na vijana wa kizazi kipya wanaziimba kwa kichwa; maneno yanayowekwa kwenye muziki yanaamsha hisia kali ya mambo msingi katika maisha. Inasadikiwa kwamba, Italia ni kati ya nchi ambazo zina utajiri na amana kubwa ya nyimbo za zamani za Noeli, zinazofahamika na kuimbwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu. Hizi ni nyimbo zenye utajiri na amana kubwa ya kitaalimungu na kwamba, Mtakatifu Alfonsi Maria de Liguori, ni kati ya watunzi mahiri sana wa nyimbo za Noeli. Nyimbo za Noeli zimeenea sehemu mbalimbali za dunia na zinapania kuwasilisha ujumbe wa kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu. Huu ni ujumbe unaomwilishwa katika lugha na tamaduni mbalimbali, kwa sababu Injili ya Noeli ni moja, lakini inamwilishwa katika lugha na tamaduni mbalimbali. Lakini kwa bahati mbaya mwelekeo wa sasa wa “kiteknokratiko” unakwenda kinyume chake kwa kutaka kufanya mambo yote kuwa sawa. Sanaa ya nyimbo za Noeli ni tofauti na nyimbo hizi ambazo zinapaswa kuimbwa kama zinazovububujika kutoka katika sakafu ya nyoyo za waamini na wasanii katika ujumla wao.

Fumbo la Umwilisho: Utukufu kwa Mungu na Amani Duniani
Fumbo la Umwilisho: Utukufu kwa Mungu na Amani Duniani

Kwa bahati mbaya, anasema Baba Mtakatifu Francisko Sherehe ya Noeli imetekwa na wafanyabiashara na hivyo kugeuzwa kuwa ni kipindi cha ulaji wa kupindukia. Kumbe, ni wajibu na dhamana ya wasanii, kulinda na kudumisha maana ya Sherehe ya Noeli kwa nyimbo zao. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 23 Septemba 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa Kipapa wa Utamaduni wa Elimu “Fondazione Pontificia Gravissimum Educationis – Cultura per l’Educazione.” Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kabisa amewapongeza na kuwashukuru vijana wa kizazi kipya wanaowekeza karama na mapaji yao kwa ajili ya nyimbo za Noeli, kama kielelezo cha ukuaji wa kiutu. Kuna umati wa vijana wa kizazi kipya wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kutangaza, kukuza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Lk 2:14.

Fumbo la Umwilisho limewakirimia wanadamu amani ya kweli
Fumbo la Umwilisho limewakirimia wanadamu amani ya kweli

Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu amewakirimia binadamu amani ya kweli, amani inayohitajika kwa hali na mali katika ulimwengu mamboleo. Hili ni Fumbo ambalo limewahamasisha watunzi na wasanii wengi kutoka katika lugha na tamaduni mbalimbali kuonesha ile njia ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu duniani. Baba Mtakatifu amewaambia wasanii hawa kwamba, hata wao ni sehemu ya kundi kubwa linaloshiriki kuonesha njia kwa kujikita katika asili, historia na sauti zao kielelezo cha upendo wa Mungu, uliomwilishwa kwa Kristo Yesu anayezungumza katika nyoyo zao. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza vijana wa kizazi kipya wanaoonesha utashi wa kutangaza wito wao katika safari ya Ukristo, katika njia mbalimbali kwa sababu wanavutwa na upendo wa Fumbo la Umwilisho unaosikika katika nyimbo na muziki.

Vijana wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za kiinjili.
Vijana wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za kiinjili.

Ni katika mantiki hii, wasanii hawa nao wanakuwa ni mashuhuda na vyombo vya hija ya matumaini, kwa wale wanaoteseka, waliovunjika na kupondeka moyo kutokana na: magonjwa, vita, uhamiaji wa kulazimishwa, matatizo na changamoto za maisha ya kifamilia, masomo au misigano na kinzani na marafiki. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, baadhi ya vijana hawa wataweza kuguswa na ushuhuda wao. Kwa hakika, ulimwengu unawahitaji vijana wa kizazi kipya waliokirimiwa karama na kipaji cha ubunifu wanaosukumwa nao si kwa kupenda fedha na mali, bali ni kutokana na uzuri na udugu na Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumpatia mwanadamu maana ya maisha!

Tamasha la Noeli 2024
23 September 2024, 15:01