Wito Kwa Jumuiya ya Kimataifa Kurejesha Amani Nchini Lebanon
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Jumatano tarehe 25 Septemba 2024 amesema, amesikitishwa sana na taarifa za mashambulizi makali ya mabomu huko nchini Lebanon na hivyo kusababisha athari kubwa kwa watu na mali zao. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itafanya kila linalowezekana kukomesha mashambulizi haya yanayotishia usalama na maisha ya watu wasiokuwa na hatia.
Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wananchi wa Lebanoni wanaoendelea kuteseka kutokana na mashambulizi haya. Imekuwa pia ni fursa ya kusali na kuwaombea watu wanaoteseka kwa vita sehemu mbalimbali za dunia, hasa: Ukraine, Palestina, Israeli, Myanmar na Sudan. Baba Mtakatifu Francisko katika maeneo yote ya vita, anapenda kuwaombea amani ya kudumu.