Tafuta

Ziara ya Papa,Papua New Guinea:Mtindo wa Mungu wa ukaribu,huruma na upole

Papa Francisko amekutana na Maaskofu wa Papua New Guinea na visiwa vya Solomoni,mapadre,mashemasi,waliowekwa wakfu,waseminari na makatekista katika Madhabahu ya Maria Msaada wa Wakristo tarehe 7 Septemba 2024.Papa amefafanua juu ya ujasiri wa kuanza,uzuri wa kuwepo na matumaini ya kukua kama ushuhuda ulivyotolewa.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amekutana na Maaskofu wa Papua Guinea na visiwa vya Solomoni, mapadre, mashemasi, waliowekwa wakfu, waseminari na makatekista katika Madhabahu ya Maria Mwombezi, Jumamosi tarehe 7 Septemba 2024, akiwa katika Ziara yake ya 45 ya Kitume Barani  Asia na Oceania. Baba Mtakatifu akianza hotuba yake ametoa salamu ya upendo kwa wote hao huku akimshukuru Rais wa Baraza la Maaskofu kwa maneno yake, pamoja na James, Grace, Sr Lorena na Padre Emmanuel kwa ushuhuda wao. Ameonesha furaha sana kukutana nao katika Madhabahu hayo yaliyowekwa wakfu kwa Maria Msaada wa Wakristo, jina linalopendwa sana na Mtakatifu Yohane Bosco; au Maria Helpim wanapomwita hapo kwa upendo. Mnamo 1844, wakati Mama Yetu aliongoza Don Bosco kujenga Kanisa kwa heshima yake huko Torino, alimpatia ahadi hii: “Hapa ni nyumba yangu, kutoka hapa kuna utukufu wangu.” Maria alimuahidi kwamba ikiwa angekuwa na ujasiri wa kuanza ujenzi wa Kanisa, basi neema kubwa ingefuata. Na ndivyo ilivyokuwa: Kanisa lilijengwa - ni la ajabu - na limekuwa kituo cha kuruhusu Injili kutangazwa, kuunda vijana na kutekeleza kazi za upendo, mahali pa kumbukumbu kwa watu wengi.

Mkutano na Kanisa la Papua New Guinea
Mkutano na Kanisa la Papua New Guinea

Baba Mtakatifu amesema kuwa hekalu zuri waliojikuta ndani yake, ambalo limeongozwa na historia hiyo, linaweza kuwa ishara kwao pia kwa mambo matatu ya safari yetu ya Kikristo na ya kimisionari ambayo yaliangaziwa katika shuhuda walizosikia: ujasiri wa kuanza, uzuri wa kuwepo, na matumaini ya kukua. Kwanza, ujasiri wa kuanza. Wajenzi wa madhabahu hayo  walianza kazi yao kwa tendo kubwa la imani, ambalo limezaa matunda. Walakini iliwezekana tu kwa sababu ya mwanzo mwingine mwingi wa ujasiri na wale waliowatangulia. Wamisionari walifika katika nchi hiyo katikati ya karne ya kumi na tisa, na hatua za kwanza za huduma yao hazikuwa rahisi. Hakika baadhi ya majaribio yameshindwa. Hata hivyo, hawakukata tamaa; kwa imani kuu, ari ya kitume na sadaka nyingi, waliendelea kuhubiri Injili na kuwatumikia ndugu zao, wakianza tena mara nyingi kila waliposhindwa.

Zawadi
Zawadi

Madirisha ya vioo kwenye Madhabahu hiyo, Papa Francisko alisema yanakumbusha hilo. Mwanga wa jua unatabasamu kupitia nyuso za watakatifu na wenyeheri, wanawake na wanaume kutoka asili zote, waliounganishwa na historia ya jumuiya yao: Peter Chanel, John Mazzucconi na Peter To Rot, mashahidi wa New Guinea, na pia Teresa wa Calcutta, Yohane Paulo II, Mary McKillop, Maria Goretti, Laura Vicuña, Zeffirino Namuncurà, Francis wa Sales, Yohane  Bosco, Maria Domenica Mazzarello. Hawa ni kaka  na dada wote ambao, kwa njia tofauti na kwa nyakati tofauti walianza mipango na  hata njia potofu, walianza tena mara nyingi. Walichangia kuleta Injili kwao, pamoja na mali nyingi za karama zenye rangi nyingi zinazohuishwa na Roho yule yule na mapendo yale yale ya Kristo (rej. 1Kor 12:4-7; 2Kor 5:14).

Papa na maaskofu
Papa na maaskofu

Ni shukrani kwao, kwa kuanza kwao na na vile vile kuanza upya kwamba wako hapo  na kwamba licha ya changamoto za sasa, ambazo hazikosekani, wanaendelea kusonga mbele bila hofu, wakijua kwamba hawako peke yao. Ni Bwana anayetenda ndani yao na pamoja nao (taz. Gal 2:20), kwa kuwafanya wao kuwa kama vyombo vya neema yake (taz. 1Pet 4:10). Katika hilo na kwa kuzingatia yale yaliyosikika, Papa Francisko amependa kupendekeza mwelekeo muhimu kwa “kuanza” kwao wenyewe, yaani kando ya nchi hiyo. Amewafikiria watu walio katika sehemu zenye uhitaji mkubwa wa wakazi mijini, pamoja na wale wanaoishi katika maeneo ya mbali na yaliyotelekezwa, ambapo wakati mwingine mahitaji ya kimsingi yanakosekana. Amewafikiria “pia wale waliotengwa na kujeruhiwa, kiadili na kimwili, kwa ubaguzi na ushirikina, nyakati fulani hadi kufikia hatua ya kuhatarisha maisha yao, kama vile James na Sr Lorena walivyokumbusha. Kanisa linatamani hasa kuwa karibu na kaka na dada hawa, kwa sababu ndani yao Yesu yumo kwa namna ya pekee (rej. Mt 25:31-40). Na pale yeye, kichwa chetu, yupo, hapo ndipo sisi, viungo vyake, kwa kuwa sisi ni wa mwili mmoja, “tukiwa tumeunganishwa na kuunganishwa kwa kila kiungo" (Efe 4:16).

Papa akutana na watu wa Kanisa Katoliki
Papa akutana na watu wa Kanisa Katoliki

Katika hilo ndipo imepelekea  kwenye kipengele cha pili cha: uzuri wa kuwepo. Baba Mtakatifu Francisko amesisitiza kuwa “hiyo inawezekana kuifananisha  na magamba ya kina, ishara ya mafanikio ambayo yanapamba baraza kuu la Kanisa hilo. Ni kukumbusha kuwa “ sisi ni hazina nzuri zaidi machoni pa Baba. Karibu na Yesu na chini ya vazi la Maria, tumeunganishwa kiroho na kaka na dada zetu wote ambao Bwana ametukabidhi, na wale ambao hawawezi kuwa hapa, tukiwa na hamu ya kwamba ulimwengu wote upate kuijua Injili na kushiriki katika nguvu na mwanga wake. James aliuliza jinsi gani tunaweza kufikisha shauku ya utume wa kimisionari kwa vijana.  

Papa aliwasalimaia hata watu waliokusanyika nje ya Madhabahu ya Mama Yetu
Papa aliwasalimaia hata watu waliokusanyika nje ya Madhabahu ya Mama Yetu

Papa Francisko katika hilo amesema “Sidhani kama kuna mbinu za hiyo. Njia moja iliyothibitishwa, hata hivyo, ni kukuza na kushiriki nao furaha yetu ya kuwa Kanisa (taz. Benedikito  XVI, Mahubiri  katika Misa ya Kusimikwa kwa Mkutano Mkuu wa Tano wa Uaskofu wa Amerika ya Kusini na Carribien, Aparecida, 13 Mei 2007), nyumba ya ukaribishaji iliyofanyizwa kwa vito vilivyo hai, vilivyochaguliwa na vya thamani, vilivyowekwa na Bwana karibu na kila kimoja na kukimarishwa kwa upendo wake (rej. 1 Pet. 2:4-5). Papa Francisko amesema kuwa "Kama vile uzoefu wa Neema wa Sinodi unavyotukumbusha, kwa kuthaminiana na kuheshimiana na kujiweka katika huduma ya sisi kwa sisi, tunaweza kuonyesha kila mtu tunayekutana naye jinsi ilivyo nzuri kumfuata Yesu pamoja na kutangaza Injili yake. Uzuri wa kuwepo, basi, haupatikani sana katika matukio makubwa na wakati wa mafanikio, lakini katika uaminifu na upendo ambao tunajitahidi kukua pamoja kila siku. 

Papa akifurahi na Sr
Papa akifurahi na Sr

Papa Francisko akiendelea amefafanua kipengele cha tatu na cha mwisho: tumaini la kukua. Katika madhabahu hiyo  kuna Katekesi kwa njia ya picha za kuvutia zinazojumuisha kuvuka kwa Bahari ya Shamu, na hatua  za Ibrahimu, Isaka na Musa. Ni Mababa waliozaa matunda kwa njia ya imani, waliopokea karama ya uzao wengi kwa sababu waliamini (rej. Mw 15:5; 26:3-5; Kut 32:7-14). Hii ni ishara muhimu, kwa sababu inatutia moyo pia leo kuwa na imani katika kuzaa matunda ya utume wetu, tukiendelea kupanda mbegu ndogo za mema katika mifereji ya dunia. Inaweza kuonekana kuwa ndogo kama punje ya haradali, lakini tukiamini na tusipoacha kutawanya, kwa neema ya Mungu itachipuka na kutoa mavuno mengi (taz. Mt 13:3-9) na kuzaa miti yenye uwezo wa kuwakaribisha ndege wa angani (rej. Mk 4:30-32). Mtakatifu Paulo anatukumbusha kwamba kukua kwa kile tunachopanda si kazi yetu wenyewe, bali ni ya Bwana (rej. 1Kor 3:7).

Hotuba ya Papa
Hotuba ya Papa

Papa kwa kukazia amesema "Mama Kanisa Mtakatifu anafundisha jambo lile lile anaposisitiza kwamba hata kwa juhudi zetu wenyewe, Mungu ndiye “afanyaye ufalme wake kuja duniani” (reg Ad Gentes, 42). Kwa hiyo, Papa amewasihi kuendelea  kueneza injili kwa subira, bila kujiruhusu kukatishwa tamaa na matatizo au kutoelewana, hata yanapotokea mahali ambapo hasa hatutaki kukutana nayo: katika familia, kwa mfano, kama walivyosikia katika shuhuda. Papa Francisko amesema: “tumshukuru Bwana pamoja kwa jinsi Injili ilivyokita mizizi na kuendelea kuenea katika Papua New Guinea na Visiwa vya Solomon. Waendelee na utume wao kama mashahidi wa ujasiri, uzuri na matumaini! Amewashukuru kwa kile wanachofanya, amewabariki wote kutoka moyoni mwake. Na tafadhali, amewaomba wasimsahau katika sala zao. 

Maaskofu wakimsikiliza Papa
Maaskofu wakimsikiliza Papa
Hotuba ya Papa kwa maaskofu , mapadre na watu waliowekwa wakfu
07 September 2024, 12:38