Baa la Njaa Duniani Linasigina Utu, Heshima na Haki Msingi Za Binadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maji ni sehemu ya msingi ya mifumo ya chakula na kilimo lakini inakabiliwa na changamoto zinazoongezeka kila kukicha. Uhaba wa maji na ukame, mafuriko, na uchafuzi wa vyanzo vya maji vyote hivi vinadhoofisha juhudi za Kimataifa za kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yaani: Uzalishaji bora, lishe bora, mazingira bora na maisha bora, bila kumwacha mtu yoyote nyuma. Kuna zaidi ya watu bilioni tatu wanaoishi katika maeneo ya kilimo yenye viwango vya juu kabisa vya uhaba wa maji. Wakati ambapo takribani watu bilioni 1.2 wanaishi katika maeneno yenye ukame mkubwa. Baa la njaa duniani linasigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baa la njaa linazidi kuongezeka kila kukicha kutokana na vita, kinzani na misigano ya kijamii; athari za mabadiliko ya tabianchi bila kusahau majanga asilia. Na matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Katika kipindi cha miaka mitatu baa la njaa na utapia mlo wa kutisha vimeongezeka, kiasi cha kwamba, watu zaidi ya milioni 733 wanateseka kwa baa la njaa na sehemu kubwa ya waathirika ni kutoka Barani Afrika. Licha maboresho makubwa ya uzalishaji wa mazao ya chakula, lakini bado baa la njaa linaendelea kuwasakama watu ulimwenguni, kiasi cha kukosa uhakika wa usalama wa chakula. Asilimia 20% ya waathirika wa baa la njaa wako Barani Afrika na Barani Asia idadi ya watu wanao pekenywa na baa la njaa ni sawa na asilimia 8.1%, Amerika ya Kusini ni sawa na asilimia 6.2%. Kama hali ikiendelea, hadi kufikia mwaka 2030 idadi ya watu watakaosiginwa na baa la njaa itaweza kufikia watu milioni 582 na nusu ya waathirika wanatoka Barani Afrika.
Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, umaskini, ukosefu wa usawa, ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula; uhaba wa maji safi na salama; huduma bora za elimu, afya pamoja na makazi bora ni kati ya mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Lengo la Jumuiya ya Kimataifa la kutaka kufuta baa la njaa duniani ifikapo mwaka 2030 pengine lisifikiwe kutokana na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza kwa sasa duniani. Kumekuwepo na matumizi makubwa ya rasilimali za dunia kupita kiasi; athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na ukosefu wa usawa kati ya watu. Mbinu mkakati wa uhakika wa usalama wa chakula duniani ulishafikiwa takribani miaka thelathini iliyopita, lakini athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya changamoto mpya zinazotishia uhakika na usalama wa chakula duniani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuangalia mahitaji msingi ya watu mahalia; kwa kuheshimu na kuzingatia tofauti zao msingi kitamaduni ili kuondokana na dhana ya ukoloni wa kiitikadi. Kumbe, sera na mikakati ya kutokomeza baa la njaa duniani lazima izingatie mahitaji ya watu na jumuiya zao na wala watu mahalia wasitwishwe sera na mikakati kutoka juu, ambayo mara nyingi ni kwa ajili ya faida ya watunga sera hizi. Changamoto kubwa ya kutokomeza baa la njaa duniani, itaweza kufanikiwa ikiwa kama Jumuiya yote ya Kimataifa itashiriki kikamilifu, sanjari na kuondokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii.
Kumbe, FAO pamoja na Mashirika yake yote ya Kimataifa yanaweza kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kipaumbele cha kwanza, kikiwa ni maskini. Wadau mbalimbali hawana budi kuunganisha nguvu na rasilimali zao ili kupambana na baa la njaa duniani bila kumwacha mtu awaye yote nyumba. Vatican kwa upande wake, itaendelea kujizatiti kuchangia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, huku ikichota amana, utajiri, uzoefu na mang’amuzi yanayobubujika kutoka katika Kanisa Katoliki, ili duniani asiwe mtu anayekufa kwa baa la njaa; kwa kuendelea kulinda na kuhifadhi mazingira nyumba ya wote, ili dunia irejee tena kuwa ni bustani iliyotengenezwa kwa mikono ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao ya binadamu wote. Ni katika muktadha huu wa mapambano dhidi ya baa la njaa duniani, Umoja wa Mataifa unasema, takwimu zinaonesha kwamba, kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo, hali ya usalama wa chakula imendelea kuwa tete sana.