Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia barua Makardinali wapya ishirini na moja, walioteuliwa hivi karibuni, ambao watasimikwa rasmi tarehe 7 Desemba 2024 na kuadhimisha Misa ya pamoja 8 Desemba 2024. Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia barua Makardinali wapya ishirini na moja, walioteuliwa hivi karibuni, ambao watasimikwa rasmi tarehe 7 Desemba 2024 na kuadhimisha Misa ya pamoja 8 Desemba 2024.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Barua ya Baba Mtakatifu Francisko Kwa Makardinali Wapya 2024

Baba Mtakatifu anawasihi Makardinali wote wapya kuhakikisha kwamba, wanainua macho yao; mikono yao iliyofungwa na miguu wazi. Hii kimsingi ni mitazamo mitatu inayopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Makardinali wapya kwa kuwa na: Macho yaliyoinuliwa ili kuweza kuona mbali na hivyo kupenda na kwa bidii zaidi. Huu ni mwaliko wa kuketi pamoja na Yohane wa Msalaba katika “Shule ya macho yake” ambayo ni upande wa Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia barua Makardinali wapya ishirini na moja, walioteuliwa hivi karibuni, na kuingizwa kwenye Baraza la Makardinali, wanakuwa pia na hadhi ya washirika wa Jimbo kuu la Roma. Ushirika huu ni kielelezo cha umoja wa kanisa na kifungo kinachounganisha Makanisa yote mahalia na Kanisa la Roma. Ni katika mukadha huu, Baba Mtakatifu anapenda kuwasihi Makardinali wote wapya kuhakikisha kwamba, wanainua macho yao; mikono yao iliyofungwa na miguu wazi. Hii kimsingi ni mitazamo mitatu inayopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Makardinali wapya. Wanapaswa kuwa na macho yaliyoinuliwa, kwa sababu huduma yao inawahitaji kupanua nyoyo zao, ili kuweza kuona mbali na hivyo kupenda na kwa bidii zaidi. Huu ni mwaliko wa kuketi pamoja na Yohane wa Msalaba katika “Shule ya macho yake” ambayo ni upande wa Kristo Yesu, unaoteseka.

Makardinali wawe ni watu wa sala
Makardinali wawe ni watu wa sala

Wawe na mikono iliyofungwa, kwa sababu kile ambacho Kanisa linahitaji zaidi ni pamoja na mahubiri ya kina kutoka katika Injili, Sala na maombi ili kuweza kuchunga vyema zaidi kundi la Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anasema kwamba, Sala ni sehemu ya utambuzi itakayowasaidia kutafuta na hatimaye, kugundua na hivyo kutekeleza mapenzi ya Mungu kwa watu wao. Miguu yao inapaswa kuwa wazi kwa sababu inagusa hali halisi mbaya ya sehemu mbalimbali za dunia zinazogubikwa na mateso na maumivu kutokana na: Vita, ubaguzi, nyanyaso, njaa pamoja na mifumo mbalimbali ya umaskini; mambo ambayo yatawadai Makardinali hawa wapya neema na rehema kubwa, ili kupambana nayo! Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru Makardinali wapya kwa moyo wao wa ukarimu na anapenda tangu sasa kuwahakikishia sala na maombi yake kwao na anapenda kuwakaribisha katika huduma kwa watu wa Mungu. Anamwomba Kristo Yesu aweze kuwabariki na Bikira Maria aweze kuwasindikiza katika safari yao ya huduma.

Makardinali waketi kwenye Shule ya Yohane wa Msalaba
Makardinali waketi kwenye Shule ya Yohane wa Msalaba

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko anasema lengo la kuwa na wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwenye Baraza la Makardinali ni kuweza kushuhudia Kanisa moja, takatifu, katoliki na la Mitume; kuendeleza umoja wa Kanisa huku wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Makanisa mahalia. Makardinali wapya kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha kwamba, kusudi uaskofu uwe na umoja usiogawanyika, Kristo Yesu alimweka Mtakatifu Petro, juu ya Mitume wengine, na katika yeye akatia chanzo na msingi unaodumu na unaoonekana wa umoja wa imani na ushirika wa Kanisa. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, kwa nguvu ya Ukatoliki (Catholicitatis) huu kila sehemu huvipeleka vipaji vyake yenyewe kwa sehemu nyingine na kwa Kanisa lote, hivi kwamba sehemu zote pamoja, na kila moja pia, hukithiri kwa kushirikiana zenyewe kwa zenyewe na kufanya juhudi ili kupata ukamilifu katika umoja. Mamlaka kuu ya Kiti cha Mtakatifu Petro imepewa dhamana ya kusimamia ushirika wote wa mapendo, hulinda tofauti za haki zilizopo kwa kukazia ushirika katika mema na huduma makini kwa watu wa Mungu. Rej. Lumen gentium, 13.

Papa Francisko amewaandikia Makardinali Barua ya kuwashukuru
Papa Francisko amewaandikia Makardinali Barua ya kuwashukuru

Urika wa Maaskofu hauwezi kuwa na mamlaka usipounganika na Baba Mtakatifu, aliye Mwandamizi wa Petro, Mtakatifu na Mtume; kwa nguvu ya wadhifa wake kama Wakili wa Kristo na Mchungaji wa Kanisa lote, ana mamlaka katika Kanisa, iliyo kamili, ya juu kabisa na iwahusuyo wote (plenam, supremama et universalem potestatem) ambayo anaweza kuyatimiza kwa uhuru. Urika wa Maaskofu ni urithi wa urika wa Mitume katika kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Rej. Lumen gentium, 22-27. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 6 Oktoba 2024 ametangaza majina ya Makardinali wapya ishirini na moja, watakaosimikwa rasmi tarehe 7 Desemba 2024 na kuadhimisha Ibada ya Misa na Baraza la Makardinali katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kukingiwa Dhambi ya Asili, tarehe 8 Desemba 2024. Kati ya Makardinali wapya yumo Kardinali Angelo Acerbi, mwenye umri wa miaka 99. Mama Kanisa anatambua na kuthamini mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa. Yumo pia Askofu Mykola Bychok, C.Ss.R., wa Jimbo la “Saints Peter na Paul, huko Melbourne nchini Ukraine, Yeye ana umri wa miaka 44. Kutoka Barani Afrika tunaye Askofu mkuu Ignace Bessi Dogbo, wa Jimbo kuu la Abidjan, Pwani ya Pembe pamoja na Askofu mkuu Jean-Paul Vesco, O.P., Jimbo kuu la Alger, Algeria.

Makardinali wapya ni wajumbe wa Baraza la Makardinali
Makardinali wapya ni wajumbe wa Baraza la Makardinali

Na orodha rasmi ni kama ifuatayo!

1. Askofu mkuu Angelo Acerbi, Balozi Mstaafu wa Vatican.

2. Askofu mkuu Carlos Gustavo Castillo Mattasoglio, wa Jimbo kuu la Lima, Perù

3. Askofu mkuu Vicente Bokalic Kalic Iglic C.M., wa Jimbo kuu la Santiago Argentina

4. Askofu mkuu Luis Gerardo Cabrera Herrera, O.F.M., wa Jimbo kuu la Guayaquil, Ecuador.

5. Askofu mkuu Fernando Natalio Chomalí Garib, wa Jimbo kuu la Santiago de Cile Chile.

6. Askofu mkuu Tarcisio Isao Kikuchi, S.V.D., wa Jimbo kuu la Tokyo, Japan

7. Askofu mkuu Pablo Virgilio Siongco David, wa Jimbo kuu la Kalookan, Ufilippin

8. Askofu mkuu Ladislav Niemet, S.V.D., wa Jimbo kuu la Beograd-Smederevo, Serbia

9. Askofu mkuu Jaime Spengler, O.F.M., wa Jimbo kuu la Porto Alegre, Brazil

Makardinali wapya na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kiekumene
Makardinali wapya na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kiekumene

10. Askofu mkuu Ignace Bessi Dogbo, wa Jimbo kuu la Abidjan, Pwani ya Pembe

11. Askofu mkuu Jean-Paul Vesco, O.P., Jimbo kuu la Alger, Algeria.

12. Askofu Paskalis Bruno Syukur, O.F.M., wa Jimbo la Bogor, Indonesia.

13. Askofu mkuu Dominique Joseph Mathieu, O.F.M. Conv., wa Jimbo kuu la Teheran Ispahan, Iran.

14. Askofu mkuu Roberto Repole, wa Jimbo kuu la Torino, Italia.

15. Askofu Msaidizi Baldassare Reina, Jimbo kuu la Roma, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma.

16. Askofu mkuu Francis Leo, wa Jimbo Katoliki la Toronto, Canada.

Makardinali ni washirika wa Jimbo kuu la Roma
Makardinali ni washirika wa Jimbo kuu la Roma

17. Askofu mkuu Mwandamizi Rolandas Makrickas, Kiongozi mkuu, Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma.

18. Askofu Mykola Bychok, C.Ss.R., wa Jimbo la “Saints Peter na Paul wa Melbourne nchini Ukraine

19. Padre Timothy Peter Joseph Radcliffe, OP, Mwanataalimungu.

20. Padre Fabio Baggio, C.S., Katibu mkuu msaidizi Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu ya Binadamu

21. Monsinyo George Jacob Koovakad, Afisa Mwandamizi Sekretarieti kuu ya Vatican na Mratibu wa Hija za Kitume za Baba Mtakatifu.

Barua Kwa Makardinali Wapya
12 October 2024, 14:59