Tafuta

"Dilexit nos” yaani “Alitupenda” Waraka wa Kitume juu ya upendo wa kibinadamu na wa Kimungu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Kristo.” "Dilexit nos” yaani “Alitupenda” Waraka wa Kitume juu ya upendo wa kibinadamu na wa Kimungu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Kristo.”  

Dilexit nos: Yaani Alitupenda: Upendo wa Kibinadamu na Kimungu wa Moyo Mt. wa Yesu

Papa Francisko, Alhamisi tarehe 24 Oktoba 2024 amechapisha Waraka wa Kitume: "Dilexit nos” yaani “Alitupenda” Waraka wa Kitume juu ya upendo wa kibinadamu na wa Kimungu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Kristo." Yesu aliwapenda waja wake upeo na kuwataka kutambua kuwa, hakuna jambo lolote linaloweza kuwatenga na upendo wake, kiasi kwamba aliwaita rafiki zake. Yesu anapenda kuwapatia waja wake upendo na urafiki na kwamba, “alitupenda sisi kwanza!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 24 Oktoba 2024 amechapisha Waraka wa Kitume unaojulikana kama "Dilexit nos” yaani “Alitupenda” Waraka wa Kitume juu ya upendo wa kibinadamu na wa Kimungu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Kristo.” Kristo Yesu aliwapenda waja wake upeo na kuwataka kutambua kuwa, hakuna jambo lolote linaloweza kuwatenga na upendo wake, kiasi kwamba aliwaita rafiki zake. Kristo Yesu anapenda kuwapatia waja wake upendo na urafiki na kwamba, “alitupenda sisi kwanza. Rej. 1Yn 4:10. Na kwa sababu ya Kristo Yesu “Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi.” 1Yn 4:16. Waraka huu umegawanyika katika Sura tano: Umuhimu wa Moyo; Matendo na Maneno ya Moyo. Huu ni moyo uliopenda upeo. Moyo unaojitoa kama kinywaji; Upendo kwa upendo na hatimaye ni hitimisho! Baba Mtakatifu Francisko katika Sura ya Kwanza anasema, Moyo ni kielelezo ambacho kimetumika kuonesha upendo wa Kristo Yesu. Moyo kwa lugha ya Kigiriki unajulikana kama “Kardia” kiungo muhimu sana kwa maisha ya binadamu na mahali ambapo maamuzi muhimu yanafanyika. Moyo katika Maandiko Matakatifu ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake kama ilivyokuwa kwa wale wanafunzi wa Emau; ni mahali panapotunza ukweli, nia na siri za ndani kabisa za maisha ya mwanadamu. Huu ni mwaliko kwa waamini kurejea katika undani wa mioyo yao ili kuzungumza kutoka katika undani wa maisha yao, ili kujenga na kurutubisha mahusiano na mafungamano ya dhati. Moyo unaweza kuelezwa kwa kutumia sayansi za dunia hii, lakini kimsingi moyo ni bandari ya upendo, yenye uwezo wa kusikiliza katika ukimya. Moyo unaunganisha yale yaliyotawanyika na kusambaratika; ni kiungo kinachounganisha nafsi ya mtu na jirani zake. Ni mahali pa kuhifadhi sanjari na kuendeleza majadiliano na tafakari ya kina katika nafsi kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Rej. Lk 2:19. Vita na majanga yanayoendelea kumwandama mwanadamu ni kielelezo kwamba, ulimwengu unakosa moyo!

Vita na majanga asilia ni kielelezo cha walimwengu kukosa moyo!
Vita na majanga asilia ni kielelezo cha walimwengu kukosa moyo!

Mtakatifu Inyasi wa Loyola na Mtakatifu Bonaventura wanauangalia moyo kama “moto” unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Moyo wa mwanadamu una uwezo wa kuratibu nguvu na hisia ya upendo wenye utii kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ulimwengu unaweza kufanya mabadiliko kwa kuanzia katika moyo na hivyo kumruhusu Roho Mtakatifu kuwa ni mhimili wa umoja, na upatanisho; mambo msingi yanayofumbatwa katika Ibada ya Ekaristi Takatifu, inayotakasa. Kwa hakika kuna haja kwa watu kugeuza mioyo yao. Maana binadamu katika undani wake huzidi viumbe vyote; naye anaingia tena katika undani huo anapourudia moyo wake. Ndimo ambamo Mwenyezi Mungu anamngojea, Yeye ambaye ndiye mwenye kuichunguza mioyo, tena ambamo binadamu mbele ya macho ya Mungu huamua bahati yake. Kwa hakika Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kiunganishi. Katika Sura ya Pili, Baba Mtakatifu Francisko anazungumzia matendo na maneno ya upendo yanayojidhihirisha katika Fumbo la Umwilisho; kiasi cha kuwaita wafuasi wake kuwa ni rafiki na kwamba, Kristo Yesu ni ufunuo wa ukaribu, huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka katika kuganga na kuwaponya wagonjwa na wale wote waliokuwa wametengwa na hivyo kuwahamasisha kuondokana na hali ya kujikatia tamaa kwani Kristo Yesu anataka rehema na wala si sadaka. Rej. Mt 9:13. Kristo Yesu alikuwa na jicho la huruma na upendo; alitambua mahitaji msingi ya waja wake, kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa! Watu wengi walikuwa wakitafuta wokovu, ustawi na usalama wa maisha yao; kwa wote hawa anasema Mtakatifu Paulo, Kristo Yesu aliwaonesha upendo wake wa dhati!

Moyo Mtakatifu wa Yesu ni Muhtasari wa Injili
Moyo Mtakatifu wa Yesu ni Muhtasari wa Injili

Baba Mtakatifu katika Sura ya Tatu anauangalia Moyo Mtakatifu wa Yesu uliopenda upeo. Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kielelezo cha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani; kiini cha Ibada ya Kumwabudu na mwaliko wa kujikita katika majadiliano, upendo, uaminifu na Ibada kwa Kristo Yesu aliyewaganga na kuwaponya wagonjwa; aliyewasamehe na kuwaonesha huruma wadhambi. Huyu ndiye Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kristo ambaye amenyoosha mikono yake kuwaambata wote wanaokimbilia huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Huu ni mwaliko wa kuabudu Picha ya Moyo wake Mtakatifu; unaosheheni ubinadamu na umungu wake. Upendo wa Kristo Yesu unagusa na uko karibu na kila mtu! Waamini wanamwaubudu na kumtukuza Kristo Yesu katika: Njia ya Msalaba, Damu yake Azizi inayobubujika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu pamoja na Ibada ya Ekaristi Takatifu. Zote hizi ni juhudi za kumwilisha upendo kwa Kristo Yesu, matumaini na kumbukumbu. Huu ni mwaliko wa kutafakari upendo wa Kimungu, Kibinadamu pamoja na kuguswa na upendo wake usiokuwa na kifani. Upendo wa Kristo Yesu unabubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kama linavyofafanuliwa katika Liturujia ya Kanisa. Mamlaka fundishi ya Kanisa katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, imekuza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kama kielelezo cha imani na Ibada ya Kikristo. Hii ni njia muafaka ya kumfahamu Mungu na mwanadamu kujifahamu yeye peke yake, tayari kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo, kielelezo cha uwepo angavu wa Kristo Yesu ulimwenguni. Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu ni muhimu sana kwa sababu Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu ni muhtasari wa Injili. Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake na mahali muafaka pa kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano na Yesu wa Ekaristi, mwaliko kwa waamini kupyaisha tena na tena Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, na hivyo kuendelea kujiaminisha kwa Moyo wake Mtakatifu.

Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya huruma na faraja
Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya huruma na faraja

Baba Mtakatifu Francisko katika Sura ya Nne anazungumzia kuhusu Upendo unaojitoa kama kinywaji, ili kuendelea kuboresha mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu sanjari na Injili yake; kwa kukua na kukuza mahusiano ya kiroho, tayari kujifunga katika maisha na utume wa Kimisionari. Huu ni mwaliko wa kuzama katika Maandiko Matakatifu, Mapokeo Hai ya Kanisa na Shuhuda mbalimbali ambazo zimejitokeza katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki ni kielelezo cha Mungu wenye kiu ya upendo. Waamini wanahimizwa kunywa maji yanayobubujika kutoka katika ubavu wa Kristo Yesu, Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukuza, kudumisha na kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kama ilivyokuwa kwa watakatifu waliokuwa na Ibada ya pekee kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya imani, faraja, matumaini na mapendo. Kristo Yesu ni kiini cha upendo “Iesus Caritas.” Baba Mtakatifu anasema, Wayesuit wametoa mchango mkubwa katika kueneza Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu sanjari na Tasaufi ya Mtakatifu Inyasi, chemchemi ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu na Mchakato wa uinjilishaji. Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya faraja kwa Kanisa linalosafiri katika historia, ili waamini wenyewe waweze kuwa ni faraja kwa jirani zao.

Upendo unaomwilishwa katika huduma makini!
Upendo unaomwilishwa katika huduma makini!

Baba Mtakatifu Francisko katika Sura ya Tano anazungumzia kuhusu upendo kwa upendo, kwani Kristo Yesu anawataka waja wake wamwoneshe upendo, ili aweze kuwapenda zaidi na zaidi, ili hata wao wenyewe waweze kuwaonjesha jirani zao upendo. Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu ni muhtasari wa Injili ya upendo kwa Mungu na jirani. Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu ni utajiri unaoweza kuchotwa na wengine, na hivyo kumwezesha Bikira Maria na waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kupyaisha tena Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa kujikita katika upendo na kuepuka nafasi za dhambi, kwani kila dhambi inayotendwa na mwamini inaacha madhara katika Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Huu ni mwaliko kwa waamini kujikita katika kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Walimwengu wanahitaji maisha na nuru inayobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, tayari kuganga na kuponya mioyo iliyovunjika na kupondeka kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini. Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa mchakato wa upatanisho, ili hatimaye, kuweza kupata amani na utulivu wa ndani. Kuna umuhimu kwa waamini kufanya toba na kuomba msamaha wa dhambi. Waamini wanapaswa kurekebisha maisha yao mintarafu Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili kuonja upendo wake usikokuwa na mipaka; waendelee kujikita katika haki ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza waamini kuwa waadilifu na watu wenye amani na utulivu wa ndani. Kwa njia ya sadaka na mateso yake, Kristo Yesu katika unyenyekevu amewapatanisha wanadamu na Mungu pamoja na kuwaletea wokovu, mwaliko kwa waamini kuwa ni wanyenyekevu kwa kujenga mahusiano na maridhiano na watu; kwa kuendelea kuwa ni wamisionari, tayari kujikita katika ujenzi wa haki jamii inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu, amani na haki tayari kutangaza, kujenga na kushuhudia ufalme na ukuu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia.

Moyo Mtakatifu wa Yesu: Upendo wa kibinadamu na kimungu
Moyo Mtakatifu wa Yesu: Upendo wa kibinadamu na kimungu

Hii ni dhamana na jukumu la watu wote wa Mungu kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu tayari kujikita katika mchakato wa huduma ya upendo. Upendo uwe ni utambulisho wa maisha na utume wa Kanisa; mahali muafaka pa kukutana na Kristo Yesu ambaye daima anaambatana na waja wake, kama chemchemi ya huruma na upendo. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kuwa ni wamisionari tayari kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu; waamini wawe tayari kuwashirikisha jirani zao furaha na upendo unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Baba Mtakatifu anahitimisha Waraka huu wa Kitume: "Dilexit nos” yaani “Alitupenda” Waraka wa Kitume juu ya upendo wa kibinadamu na wa Kimungu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Kristo” kwa kusema kwamba, Waraka huu utawasaidia waamini kuona kwamba, Mamlaka fundishi ya Kanisa “Magisterium” yanayofumbatwa katika: Waraka wa Kitume, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” pamoja na Waraka wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” kuwa ni nyenzo muhimu zinazowasaidia waamini kukutana na huruma na upendo wa Kristo Yesu, tayari kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu; kwa kutambua na kuheshimu utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kuendelea kupyaisha upendo kwa watu wa Mungu. Moyo Mtakatifu wa Yesu usaidie kuganga na kutibu majeraha ya mwanadamu; isaidie kuimarisha uwezo wa waamini kupenda na kuhudumia, ili kufanya hija ya pamoja inayopania kujenga jamii inayosimikwa katika haki, mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Dilexit nos
24 October 2024, 14:37