Tafuta

Hayati Kardinali Eugenio Dal Corso, P.S.D.P.. 1939 hadi 2024 Hayati Kardinali Eugenio Dal Corso, P.S.D.P.. 1939 hadi 2024  (Vatican Media)

Hayati Kardinali Eugenio Dal Corso 1939 -2024: Mmisionari: Argentina na Angola

Kardinali Eugenio Dal Corso alisadaka maisha yake katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu nchini Argentina na Angola. Alizaliwa tarehe 16 Mei 1939 huko Calabria. Baada ya malezi na majiundo yake ya kitawa, tarehe 8 Septemba 1959 akaweka nadhi na hatimaye, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 17 Julai 1963. Mwaka 1975 alianza utume wake wa kimisionari nchini Argentina na mwaka 1986 akahamishiwa nchini Angola; akawekwa wakfu na kuwa Askofu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 98 ya Kimisionari Ulimwenguni Dominika tarehe 20 Oktoba 2024 umenogeshwa na kauli mbiu “Enendeni na alikeni kila mtu kwenye Karamu” (Rej. Mt. 22:9) Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anakazia: Umuhimu wa kutoka na kualika na kwamba, kila Mkristo anawajibika. Kwenda arusini ni mwelekeo wa kieskatolijia na kiekaristi wa utume wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kila mtu anaitwa kushiriki katika utume wa Kiulimwengu wa wafuasi wa Kristo Yesu katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari katika utimilifu wake na uwajibikaji wake wote katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kama wafuasi wamisionari wa Kristo Yesu wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi kama inavyobainishwa kwenye kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.”

Kardinali Eugenio Dal Corso
Kardinali Eugenio Dal Corso

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Siku ya 98 ya Kimisionari Ulimwenguni, Kardinali Eugenio Dal Corso alipofariki dunia, huko Jimbo Katoliki la Verona, Italia, akiwa na umri wa miaka 85 na Ibada ya mazishi kuadhimishwa Alhamisi tarehe 24 Oktoba 2024, kwenye Kanisa kuu la Jimbo la Verona. Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa na Askofu Domenico Pompili wa Jimbo la Verona. Kardinali Eugenio Dal Corso alisadaka maisha yake katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu nchini Argentina na Angola. Alizaliwa tarehe 16 Mei 1939 huko Calabria. Baada ya malezi na majiundo yake ya kitawa, tarehe 8 Septemba 1959 na hatimaye, kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 17 Julai 1963. Mwaka 1975 alianza maisha na utume wake wa kimisionari nchini Argentina na mwaka 1986 akahamishiwa nchini Angola. Tarehe 15 Desemba 1995 aliteuliwa kuwa Askofu mwandamizi mwenye dhamana ya kurithi Jimbo Saurino na hatimaye, kuwekwa wakfu kama Askofu tarehe 15 Januari 1997. Tarehe 18 Februari alihamishiwa kwenye Jimbo la Benguela nchini Angola. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Oktoba 2019 akamtangaza kuwa ni Kardinali. 

Kardinali Eugenio Dal Corso
Kardinali Eugenio Dal Corso

Baba Mtakatifu Francisko kwa masikitiko makubwa amepokea taarifa za kifo cha Kardinali Eugenio Dal Corso, Mtoto wa kiroho wa Mtakatifu Yohane Calabria, Mtawa mwaminifu na mmisionari mahiri aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu nchini Argentina na Angola ambako aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Saurimo na baadaye Benguela. Kardinali Eugenio Dal Corso, alisadaka maisha yake kwa ajili ya huduma kwa maskini na wanyonge na hawa akawashirikisha ushuhuda wa upendo wa Kristo usiokuwa na mipaka. Baba Mtakatifu anamwombea Marehemu Kardinali Eugenio Dal Corso, Mtumishi mwema wa Mungu, ili kwa msaada wa sala na maombezi ya Bikira Maria, aweze kupokelewa mbinguni kwenye maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu ametoa baraka zake za kitume kwa Wanashirika wa “Poveri Servi della Divina Provvidenza; na kwa watu wote wa Mungu walioshiriki katika Ibada ya maziko ya Kardinali Eugenio Dal Corso.

Hayati Kardinali Eugenio

 

25 October 2024, 14:33