Hotuba ya Papa Francisko Kwa Mkutano Mkuu wa Jimbo Kuu la Roma
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni tarehe 25 Oktoba 2024 ameshiriki katika hitimisho la Mkutano Mkuu wa Jimbo Kuu la Roma, uliozinduliwa mwezi Februari 2024 kama sehemu ya tafakari ya kina ya Kumbukizi ya Miaka 50 tangu kulipofanyika Kongamano kuhusu “Dhamana na Wajibu wa Wakristo Mintarafu Matarajio ya Upendo na Haki kutoka Jiji la Roma.” Kongamano hili lilifanyika kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 15 Februari mwaka 1974 na likapachikwa jina kuwa ni “Kongamano Juu ya Dhambi za Roma.” Huu umekuwa ni muda wa tafakari ya kina iliyotolewa na Kardinali Mteule Baldassare Reina, anayejulikana kwa kifupi kama Baldo, Makamu wa Askofu Jimbo kuu la Roma ambaye amegusia umaskini wa watu wa Mungu Jijini Roma, uliopelekea mageuzi makubwa ya maisha na utume wa Kanisa Jimbo kuu la Roma, mara baada ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Kanisa likajikita katika majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi, ili kuamsha dhamiri nyofu miongoni mwa raia, wanasiasa na Wakristo katika ujumla wao. Leo hii, Mama Kanisa anaendelea kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari; na Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Matukio yote haya ni fursa kwa watu wa Mungu kuweza kukutana na hatimaye, kuambata huruma na upendo wa Mungu, tayari kupambana na changamoto za umaskini wa: elimu, ajira, makazi na mmong’onyoko wa tunu msingi za kimaadili na utu wema. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kujielekeza zaidi katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: haki na amani; Ukweli na uzima; Utakatifu na neema tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo. Bwana Marco Damilano amefafanua kwa muhtasari yale yaliyotendeka katika kipindi cha miaka 50 tangu kuliponyanyika Kongamano lile pamoja na kusikiliza shuhuda za watu waliokuwepo nyakati zile. Baada ya utangulizi huu, ilifika zamu ya Baba Mtakatifu Francisko kuwahutubia wajumbe wa Baraza kuu la Jimbo kuu la Roma.
Baba Mtakatifu katika hotuba yake amejikita zaidi katika ukosefu wa usawa na mifumo mipya ya umaskini unaoendelea kujitokeza; wito kwa watu wa Mungu ni kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu, kwa sababu maskini ni sehemu ya vinasaba na Sakramenti ya Kanisa; wanapaswa kupewa kipaumbele katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na kujenga mshikamano wa upendo unaojikita katika majadiliano, tayari kupandikiza mbegu ya matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, takwimu na shuhuda zinaonesha kwamba bado kunakosekana usawa na kwamba, mifumo mipya ya umaskini inaendelea kuwapekenya watu wa Mungu Jijini Roma. Kuna watu wanaoishi katika hali na mazingira magumu, kiasi hata cha kukosa makazi maalum na matokeo yake wanaishi barabarani. Kuna vijana ambao wanashindwa kupata ajira na makazi; kuna wazee na wagonjwa wanaoelemewa na upweke hasi. Kuna kundi kubwa la vijana walioathirika kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia, kiasi kwamba, idadi ya waathirika wa magonjwa ya afya ya akili inaendelea kuongezeka maradufu. Kuna wagonjwa ambao hawana bima ya afya na hivyo hawawezi kupata tiba mahali popote pale. Kumbe, hawa si idadi bali ni ndugu na jamaa wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na mifumo mbalimbali ya umaskini mamboleo. Hawa ni sehemu ya Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu, mwaliko kwa waamini kuyaangalia na kuyatafakari.
Kumbe, huu ni wito na mwaliko kwa waamini kujizatiti katika kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu, kwa sababu hawa ni sehemu muhimu sana ya Mwili wa Kristo na ni kama Sakramenti inayoonekana kwa macho matupu! Hawa wanapaswa kuhudumiwa kwa moyo wa ukarimu na upendo; watambue kwamba, Kristo Yesu anawapenda upeo! Utu, heshima na haki zao msingi ni mambo yanayopaswa kulindwa na kuendelezwa. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza watu mbalimbali wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa hali na mali. Huduma hii inapaswa kuwa ni wajibu shirikishi kwa watu wote. Kwa upande wa Mama Kanisa, anaitwa na kutumwa, ili kuhakikisha kwamba, maskini wanapewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Kanisa linapenda kuwahakikishia maskini ukarimu, huruma na upendo wa Mungu kwao. Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma kuangalia tena mtindo wao wa maisha; kwa kujenga mtandao wa mshikamano ili utu, heshima na haki msingi za binadamu zipewe kipaumbele cha kwanza na hivyo kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangiko ya jirani. Huu ni mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi na taasisi mbalimbali, tayari kupyaisha mafungamano ya kijamii yanayowahusisha na kuwashirikisha watu wote wa Mungu. Huu ni wakati wa kufikiri na kutenda, kwani maneno matupu hayavunji mfupa! Kuna haja ya kukazia tena na tena malezi na majiundo juu ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili Injili iweze kumwilishwa katika medani mbalimbali za maisha, ili hatimaye, waamini waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na udugu wa kibinadamu. Huu ni ujenzi wa mtandao wa mshikamano wa kijamii, ili kujenga na kudumisha umoja.
Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; Rerum Novarum.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, waamini wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini, huruma na mapendo kama walivyokuwa akina Don Di Liegro, Mkurugenzi wa Caritas Roma. Lakini pia kuna umati mkubwa wa watu wa Mungu wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini, dhamana na wajibu wa mshikamano wa kijamii. Watu wa Mungu wathubutu kuwa ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu, ili kuendelea kuwa waaminifu katika imani na watendaji katika upendo. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza waamini wa Jimbo kuu la Roma kwa yale yote wanayotenda kama mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Wawe tayari kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu na hatimaye, kupandikiza mbegu ya matumaini.