Katekesi Kuhusu Roho Mtakatifu na Bi Arusi: Roho Mtakatifu na Ndoa Takatifu

Papa katika Katekesi yake tarehe 23 Oktoba 2024 amejikita katika Kanuni ya Imani kama inavyofafanuliwa na Mababa wa Kanisa; Roho Mtakatifu anavyoangaza katika maisha na utume wa Kanisa na hasa katika Sakramenti ya Ndoa Takatifu. Maisha yote ya Kikristo yana alama ya mapendo ya uchumba wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Tayari Ubatizo, mlango wa kuingilia katika Taifa la Mungu, ni fumbo la ndoa; ni kama kusema mwosho wa arusi unaitangulia karamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuhitimisha Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo, Jumatano tarehe 29 Mei 2024 alianza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu.” Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 25 Septemba 2024 ilijikita kwa Roho Mtakatifu aliyemwongoza Kristo Yesu jangwani na kwamba, Roho Mtakatifu ni mwenza wa waamini katika mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi. Mwenyezi Mungu ndiye aliyemtuma Kristo Yesu kwenda Jangwani na baada ya kushinda majaribu yote ya Shetani, Ibilisi “Yesu akarudi kwa nguvu za Roho Mtakatifu.” Lk 4:14. Kristo Yesu akarudi akiwa ni mshindi, tayari kuwakomboa wale wote wanaoteswa kwa nguvu za Shetani, Ibilisi, kielelezo cha uwepo wa Ufalme wa Mungu kati ya waja wake. Shetani, Ibilisi yupo na anaishi na kwamba, dunia imesheheni matendo ya Shetani, Ibilisi, licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.

Katekesi Kuhusu Roho Mtakatifu, Kanisa: Na Ndoa Takatifu
Katekesi Kuhusu Roho Mtakatifu, Kanisa: Na Ndoa Takatifu

Baba Mtakatifu anasema, ukimshinda Shetani, Ibilisi kwa imani, anaingia kwa mkwara wa uchawi. Ikumbukwe kwamba, Shetani, Ibilisi anaishi si tu na wadhambi, bali hata na watakatifu wateule wa Mungu; anaishi katika matendo maovu ambayo mwanadamu anakutana nayo kila siku ya maisha yake! Mababa wa Kanisa wanasema, Kanisa, ushirika hai katika imani ya Mitume ambayo linaiendeleza, ni mahali muafaka pa kuweza kumfahamu Roho Mtakatifu: Katika Maandiko Matakatifu ambayo ameyavuvia; katika Mapokeo ya Kanisa yanayoshuhudiwa na Mababa wa Kanisa; Katika Mamlaka ya ufundishaji katika Kanisa “Magisterium” ambayo anayauauni, Katika Liturujia ya Sakramenti kwa njia ya maneno na alama zake, ambazo Roho Mtakatifu huwaingiza waamini katika ushirika na Kristo Yesu; Katika Sala ambamo anawaombea waamini; Katika karama na huduma zinazolijenga Kanisa; Katika ishara za maisha ya kitume na kimisionari; Katika ushuhuda wa watakatifu, ambamo anadhihirisha utakatifu wake na anaendeleza kazi ya wokovu.

Ndoa inapovunjika waathirika wakuu ni watoto
Ndoa inapovunjika waathirika wakuu ni watoto

Roho Mtakatifu na Kanisa: Utume wa Kristo Yesu na wa Roho Mtakatifu unakamilika katika Kanisa, mwili wa Kristo na Hekalu la Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu hutayarisha watu, akiwaendea kwa neema yake ili kuwapeleka kwa Kristo Yesu. Anamdhihirisha kwao, analifanya Fumbo la Kristo liwepo kwao na mwisho huwapatanisha na kuwaweka katika umoja na Mwenyezi Mungu, ili wazae matunda mengi. Kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, Kristo Yesu anavishirikisha viungo vya mwili wake Roho wake Mtakatifu na Mtakasaji. Kumbe, Kanisa ni Sakramenti ya umoja wa Fumbo la Utatu na wa watu. Rej. KKK 683-747. Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake, Jumatano tarehe 9 Oktoba 2024 ameendeleza Katekesi kuhusu Roho Mtakatifu na Kanisa mintarafu Matendo ya Mitume, Siku ile ya Pentekoste ya kwanza, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kwa kasi; kukatokea ndimi zilizogawanyika, kama ndimi za moto na wakaanza kuzungumza kwa lugha nyingine.

Kanisa ni Sakramenti ya Huruma ya Mungu
Kanisa ni Sakramenti ya Huruma ya Mungu

Roho Mtakatifu ndiye anayelihakikishia Kanisa umoja, baada ya kumpokea Roho Mtakatifu, Mitume walianza kuzungumza kwa lugha na kutoka nje kwenda kumtangaza na kumshuhudia, kielelezo cha utume wa Mama Kanisa katika kutangaza na kushuhudia hadi miisho ya dunia; katika toba na wongofu wa ndani kama ilivyotokea kwa Akida Kornelio kule Kaisaria, na hiyo ikawa ni Pentekoste mpya, iliyobomoa ukuta wa utengano kati ya Wayahudi na Wapagani, waliomwongokea Kristo Yesu katika maisha yao na Kanisa likakua na kupanuka kijiografia, utume uliofanywa na Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa kwa maongozi ya Roho Mtakatifu. Rej. Mdo 16:6-10. Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu kama ilivyokuwa pia Bithinia hadi wakafika Makedonia na huko wakahubiri Habari Njema ya Wokovu.

Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo
Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo

Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: Aliyenena kwa vinywa vya Manabii. Hii ni sehemu ya Kanuni ya Imani. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima ni kipengele kinachofafanua asili ya Nafsi ya Tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu anayetenda kazi zake kwa njia ya: Imani, Neno, Sakramenti na Sala za Kanisa. Roho Mtakatifu anawakirimia waamini uzima unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Anawapatia waamini maisha mapya kwa kufisha matendo ya mwili yanayoleta kifo! Atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa na Baba na Mwana ni imani inayoonesha Nafsi ya tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Wanandoa waheshimiane, wapendane na kuthaminiana
Wanandoa waheshimiane, wapendane na kuthaminiana

Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake Jumatano tarehe 23 Oktoba 2024 amejikita katika Kanuni ya Imani kama inavyofafanuliwa na Mababa wa Kanisa; Roho Mtakatifu anavyoangaza katika maisha na utume wa Kanisa na hasa katika Sakramenti ya Ndoa Takatifu. Maisha yote ya Kikristo yana alama ya mapendo ya uchumba wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Tayari Ubatizo, mlango wa kuingilia katika Taifa la Mungu, ni fumbo la ndoa; ni kama kusema mwosho wa arusi unaitangulia karamu ya arusi, Ekaristi. Ndoa ya Kikristo inakuwa kwa zamu yake ishara halisi, Sakramenti ya Agano la Kristo Yesu na Kanisa. Kwa kuwa inaashiria na kushirikisha neema, ndoa kati ya Wabatizwa ni Sakramenti ya kweli ya Agano Jipya. Rej. KKK 1601-1617. Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa anakazia fadhila ya upendo akisema, Mungu ni upendo. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Rej. 1 Yn 4:8. Fumbo la Utatu Mtakatifu ni chimbuko la upendo, kielelezo cha umoja na ushirika katika upendo; hiki ndicho kiini cha umoja wa Kanisa unaolifanya kuwa ni “Mwili mmoja.” Baba Mtakatifu Francisko anasema, Roho Mtakatifu ndiye kiungo cha familia katika Sakramenti ya Ndoa Takatifu, mwaliko kwa wanandoa kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kuweza kuwa ni zawadi kwa mwenzi wake wa ndoa, kadiri ya mpango wa Mungu, aliyemwumba mwanaume na mwanamke kwa sura na mfano wake. Rej. Mwa 1:27.

Roho Mtakatifu ni chemchemi ya furaha ya familia
Roho Mtakatifu ni chemchemi ya furaha ya familia

Familia ya binadamu ni kielelezo cha umoja, ushirika na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Wanandoa pamoja na watoto wao wanapaswa kuunda umoja na ushirika kiasi cha kudiriki kusema kama alivyosema Bikira Maria “Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni.” Lk 2:48. Wazazi wanapaswa kujisikia kuwa ni wamoja, katika mateso na mahangaiko ya familia. Ili kujenga na kudumisha Ndoa Takatifu, kuna haja kwa wanandoa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa kutoa nafasi kwa Fumbo la Utakatifu Mtakatifu. Na ikumbukwe kwamba, Roho Mtakatifu ni chemchemi ya furaha katika maisha ya ndoa na familia. Umoja huu katika maisha ya ndoa na familia si lelemama hata kidogo, kwani hii ni changamoto kwa wanandoa kujenga familia katika mwamba thabiti. Rej. Mt 7:24-27. Kuteleza na hatimaye kuvunjika kwa maisha ya ndoa na familia, waathirika wakubwa ni watoto. Wanandoa wengi wanapaswa kurudia tena na tena ombi la Bikira Maria kwa Kristo Yesu: “Hawana divai.” Yn 2:3. Baba Mtakatifu anawakumbusha wanandoa kwamba, ni Roho Mtakatifu anayeendelea kutenda miujiza katika maisha na utume wao, pale wanandoa wanapothubutu kumkaribisha katika safari ya maisha yao. Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu kufanya maandalizi ya kina, kuhusu maisha ya kiroho kabla ya kufunga Ndoa Takatifu kwa kutambua nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha ya ndoa na familia. Wanandoa wawe tayari kumkaribisha Roho Mtakatifu katika maisha na utume wao!

Roho Mtakatifu na Ndoa
23 October 2024, 15:58

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >