Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka kwa Wazee uliochapishwa kunako mwaka 1999, kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Wazee Ulimwenguni analialika Kanisa kutoa kipaumbele kwa wazee. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka kwa Wazee uliochapishwa kunako mwaka 1999, kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Wazee Ulimwenguni analialika Kanisa kutoa kipaumbele kwa wazee.  (Vatican Media)

Kumbukizi ya Miaka 25 ya Waraka wa Papa Yohane Paulo II Kwa Wazee

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka kwa Wazee kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Wazee Ulimwenguni anazungumzia kuhusuu: Wazee katika Maandiko Matakatifu; Wazee ni walinzi wa kumbukumbu. Waheshimu Baba na Mama yako; Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso wako kuna furaha tele; Na katika mkono wako wa kulia Mna mema ya milele. Mwishoni, Mtakatifu Yohane Paulo II anawatakia wazee wote heri na baraka katika safari ya maisha! WAZEE!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 31 Oktoba 1999 katika muktadha wa Maadhimisho ya Siku ya Wazee Ulimwenguni, aliwaandikia Waraka Wazee “Vijana wa zamani”, akiwakumbusha kwamba, hata yeye ni Mzee na anataka kuingia katika majadiliano na wazee wenzake; kwa kumshukuru Mungu kwa zawadi na fursa ambazo Mwenyezi Mungu amemkirimia katika maisha na utume wake; kwa kuweza kukutana na umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia; kwa kushuhudia matukio yaliyosheheni furaha, mateso na matumaini, lakini daima mkono wa Mungu umekuwa ukitenda katika maisha ya waja wake. Waraka huu unapata amana na utajiri wake kutoka katika Maadhimisho ya Mwaka wa Kimataifa wa Wazee, lakini zaidi ya yote kwa mahangaiko makubwa ya kichungaji kwa mwanadamu, mwanadamu mzima katika kila awamu ya maisha yake. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Uzee ni kipindi cha “vuli ya maisha” na ni wakati wa kukuza na kudumisha hekima ya moyo; mambo msingi yanayo thamanisha uzee. Ikumbukwe kwamba, wazee ni walinzi wa kumbukumbu ya pamoja, na wafasiri waliobahatika kusimika maisha yao katika kanuni maadili ambayo hutawala na kuongoza maisha ya kijamii. Mtakatifu Yohane Paulo II anawataka wazee, kujiamini, kuwa na matumaini na kuendelea kuishi katika amani kadiri ya mpango wa Mungu. Licha ya changamoto mbalimbali alizokumbana nazo katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, lakini bado aliendelea kutunza ladha ya maisha, kwa kuendelea kujituma kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hadi mwisho wa maisha yake.

Upweke hasi ni changamoto kwa maisha ya wazee wengi duniani.
Upweke hasi ni changamoto kwa maisha ya wazee wengi duniani.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka huu, anazungumzia kuhusu wazee katika Maandiko Matakatifu; Wazee ni walinzi wa kumbukumbu ya kijamii. Waheshimu Baba na Mama yako; Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso wako kuna furaha tele; Na katika mkono wako wa kulia Mna mema ya milele. Zab 16:11. Mwishoni, Mtakatifu Yohane Paulo II anawatakia wazee wote heri na baraka katika safari ya maisha! Ni katika muktadha wa kumbukizi ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipoandika Waraka kwa Wazee, Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, wakati huo, Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa na umri wa miaka 79, tayari alikuwa amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa Kanisa kuwa na sera na mikakati ya kichungaji kwa wazee, ili waendelee kushiriki kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa. Mama Kanisa anatambua umuhimu wa utume wa waamini walei pamoja na walei kuthaminisha maisha ya wazee katika ulimwengu mamboleo kwa kutambua kwamba, wazee wanaunda idadi kubwa sana ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Kumbe, sera na mwelekeo wa shughuli za kichungaji kwa wazee, katika masuala ya maisha ya kiroho, kijamii na kichungaji ndani ya Kanisa Katoliki ni muhimu sana. Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alikuwa anazungumza na wazee walioonja adha ya vita sanjari na kufanya hija ya matumaini kwa siku za usoni.

Sera, mipango na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa wazee ni muhimu
Sera, mipango na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa wazee ni muhimu

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Wazee wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya watu wao hususan katika mchakato wa uinjilishaji na majadiliano kati ya wainjilishaji na wazee. Wanao mchango mkubwa katika kutangaza na kushuhudia: Wema, upendo na huruma ya Mungu, kwa kuthamini na kujali utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kuwaheshimu na kuwaenzi wazee kuna maanisha: kuwapokea, kuwatunza na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi. Ikumbukwe kwamba, maisha ni safari kuelekea uzima wa milele, kumbe, kuna haja ya kuwaandaa wazee katika hatua ya mwisho wa maisha yao, huku wakimshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai. Jubilei ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipowaandikia Waraka Wazee, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika sera, vipaumbele na maisha kwa wazee. Kwa sasa wazee wengi wanakumbana na upweke hasi, changamoto na mwaliko wa kukuza na kudumisha tasaufi ya maisha ya kiroho itakayowahamasisha wazee kuishi kikamilifu tunu msingi za uzee wao. Maadhimisho haya, iwe ni fursa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kufanya rejea katika Waraka wa Papa Yohane Paulo II kwa Wazee; mamlaka fundishi ya Kanisa “Magisterium” kutoka kwa Baba Mtakatifu Benedikto XVI pamoja na Papa Francisko. Hapa wazo kuu linalojitokeza katika Mamlaka fundishi ya Kanisa ni kuwatambua na kuwathamini wazee kama waamini, wenye dhamana na wajibu katika maisha na utume wa Kanisa; Pili ni kutengeneza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, ili wazee waweze kushirikisha karama na uzoefu wao katika maisha na utume wa Kanisa. Lengo ni kujibu mahitaji msingi ya maisha ya kiroho kwa wazee, kwa kuwasindikiza katika kila hatua ya maisha yao, wanapojiandaa kuonana na Kristo Mchungaji mwema. Waraka wa Mtakatifu Yohane Paulo II unaweza kuwa ni msingi wa kuanzia katika kutengeneza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa wazee.

Waraka kwa wazee
21 October 2024, 14:49