Sinodi ya XVI ya Maaskofu: Hotuba ya Papa Francisko Kufunga Sinodi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko mwanzoni kabisa mwa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu 2021-2024, Jumamosi tarehe 9 Oktoba 2021, alitoa hotuba elekezi, ambayo ni msingi wa maadhimisho ya Sinodi katika hatua mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Watu wa Mungu wakajitambua kuwa wao ni sehemu ya Kanisa la Kisinodi, tayari kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu, kwa kushirikiana na binadamu wote, kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini kile ambacho Roho Mtakatifu anataka kuyaambia Makanisa. Huu ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyozinduliwa kunako mwaka 2021 na kufikia kilele chake Dominika tarehe 27 Oktoba 2024 kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mababa wa Sinodi Jumamosi tarehe 26 Oktoba 2024 walihitimisha Mapendekezo ya Hati ya Mwisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, ushuhuda wa hija ya pamoja ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, changamoto na mwaliko wa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza, ili hatimaye kuweza kuwachunga na hatimaye kuwaimarisha waamini katika imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Dhamana na wajibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kutunza na kuendeleza, amani, utulivu na mshikamano wa Kikanisa, licha ya matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazoendelea kujitokeza kwenye Makanisa mahalia, ili hatimaye, watu wote wa Mungu waweze kushiriki katika karamu kielelezo cha umoja na ushirika wa watu wa Mungu kama ilivyokuwa kwenye Sherehe ya Pentekoste ya mwanzo, watu walipoanza kuzungumza kwa lugha nyingine kama Roho Mtakatifu alivyowajalia kutamka.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa linalosafiri duniani, kwa tabia yake ni la kimisionari, limetumwa na Mwenyezi Mungu kwa Mataifa yote “Ad gentes” ili liwe “Sakramenti ya Wokovu kwa wote” sanjari na kutangaza pamoja na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kumbe, ni wajibu wa waamini kuendeleza kazi hii ili Neno la Mungu liendelee kutukuzwa na Ufalme wa Mungu utangazwe na kusimikwa duniani kote. Rej. Ad gentes, 1. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni wito wa kulitangaza Neno la Mungu bila kuliwekea vizingiti; kulifungulia malango ya maisha, bila kuliwekea kuta, ili huruma, upendo na neema ya Mungu iweze kuwafikia watu wote. Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yalianza kwa kuomba toba na wongofu wa ndani; kwa kuona aibu na kwamba, waamini wote wanafaidika na huruma ya Mungu.
Hati ya Mababa wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kuijifunza, kuimwilisha, kuipenda, kuiadhimisha na kuikumbatia, ili ulimwengu wote uweze kujazwa na fadhila ya upendo kwa Mungu na jirani. Katika Hati hii, kuna maamuzi yanayopaswa kufanyiwa kazi, ili Kanisa liendelee kuwa ni shuhuda wa amani, kwa kujifunza kuishi katika hali ya utulivu kwa kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza miongoni mwa watu wa Mungu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, hana mpango wa kuchapisha Wosia wa Kitume mara baada ya maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kwa sababu Hati ya Mababa wa Sinodi inasheheni dira, mwongozo na mwelekeo wa maisha na utume wa Kanisa, katika sehemu mbalimbali za dunia, katika hali na mazingira mbalimbali. Baba Mtakatifu Francisko amewakabidhi watu wa Mungu Hati ya Mababa wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu, ili ichapwe na kusambazwa. Baba Mtakatifu anasema, hii inaonesha dhamiri yake ya kuthamini mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ulioanza tangu mwaka 2021.
Tume mbalimbali zitaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa uhuru kamili, ili hatimaye, kutoa ushauri kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, lakini huu pia ni mchakato unaopaswa kuwahusisha watu wote wa Mungu na kwamba, kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ataendelea kuwasikiliza Maaskofu pamoja na Makanisa mahalia wanayoyaongoza. Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, huu ndio mwelekeo sahihi wa kufikia maamuzi Kisinodi kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza, kufanya mang’amuzi, kuamua na hatimaye kufanya upembuzi yakinifu. Ili kuweza kufikia hatua hii, kuna haja kwa watu wa Mungu kujikita katika ukimya, kusimama: kusali na kutafakari kwa kumsikiliza Roho Mtakatifu kwa kutambua kwamba, kuna umuhimu wa kufanya toba na wongofu wa ndani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican watamsaidia ili aweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake.
Hati ya Mababa wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu ni zawadi kwa watu wote wa Mungu katika utofauti wao. Huu ni mwaliko kwa Mababa wa Sinodi kuhakikisha kwamba, Hati hii inasomwa kwa watu wote wa Mungu katika majimbo yao; na wao wawe ni vyombo na mashuhuda wa uzoefu na mang’amuzi ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, ili watu wa Mungu waweze kutambua thamani ya Hati hii katika maisha na utume wa Kanisa. Hati hii inaakisi uzoefu na mang’amuzi ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu na ni ushuhuda wa ujasiri kwamba, inawezekana kutembea kwa pamoja katika tofauti msingi, bila kutoa laana. Wajumbe wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu wanatoka sehemu mbalimbali za dunia ambazo zimeguswa na kutikiswa na vita, umaskini na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko yaw engine. Wajumbe wakiwa wameungana kwa pamoja katika tumaini lisilodanganya, wanaendelea kuwa na ndoto pamoja na kujikita katika mchakato wa kutafuta amani, kwani amani kimsingi ni chimbuko la utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kujadiliana katika ukweli na uwazi na hatimaye, ni upatanisho.
Kanisa lenye hulka ya Kisinodi kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa linahitaji mshikamano unaomwilishwa katika matendo na kwamba, hii ndiyo hija ya Kisinodi. Hati hii ni zawadi ya Roho Mtakatifu anayelijalia Kanisa kuwa na amani na utulivu, changamoto na mwaliko wa kuendeleza umoja na ushirika hata baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, tayari kuwashirikisha wengine uzoefu na mang’amuzi ya Maadhimisho haya, kwani Roho Mtakatifu anaendelea kutenda kazi sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu mwishoni mwa hotuba yake, amewashukuru viongozi wakuu wa Sekretarieti kuu ya Sinodi, bila kuwasahau wale wote ambao hawakuonekana hadharani lakini wamefanya kazi kubwa ili kuwezesha kufanikisha Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.”