Akiwa nchini Ubelgiji, Baba Mtakatifu tarehe 28 Septemba 2024 alikutana na kuzungumza na Wajesuit 150 wanaotekeleza dhamana na utume wao nchini Ubelgiji. Akiwa nchini Ubelgiji, Baba Mtakatifu tarehe 28 Septemba 2024 alikutana na kuzungumza na Wajesuit 150 wanaotekeleza dhamana na utume wao nchini Ubelgiji.   (Vatican Media)

Mahojiano Kati ya Papa Francisko na Wayesuit Nchini Ubelgiji: Msiogope!

Mahojiano kati ya Papa na Wayesuit Ubelgiji: Kati ya tema alizogusia ni: Utamadunisho, dhamana na nafasi ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa; Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; Mang’amuzi; Wimbi la wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu anawataka Wajesuiti kuwa na ari na moyo mkuu katika kutekeleza dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa. Wajitahidi kumtafuta Mungu katika: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na huduma makini kwa watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya 46 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Ubelgiji kuanzia tarehe 26 hadi 29 Septemba 2024 ilinogeshwa na kauli mbiu “En route, avec Espérance”, yaani “Safari na Matumaini.” Akiwa nchini Ubelgiji, Baba Mtakatifu tarehe 28 Septemba 2024 alikutana na kuzungumza na Wajesuit 150 wanaotekeleza dhamana na utume wao nchini Ubelgiji. Padre Antonio Spadaro, SJ, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu, amehariri mahajiano maalum kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Wajesuit hao. Kati ya tema alizogusia ni: Utamadunisho, dhamana na nafasi ya wanawake katika maisha na utume wa Kanisa; Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; Mang’amuzi; Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu anawataka Wajesuiti kuwa na ari na moyo mkuu katika kutekeleza dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa. Wajitahidi kumtafuta Mungu katika: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na huduma makini kwa watu wa Mungu.

Papa Francisko anakazia ushuhuda wa imani katika matendo
Papa Francisko anakazia ushuhuda wa imani katika matendo

Baba Mtakatifu anasema Kanisa Katoliki halina utamaduni unaoweza kujitambulisha nao. Waamini watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, watu ambao wanapaswa kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili na kwamba, Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa mchakato wa Uinjilishaji. Kumbe, utamadunisho na uinjilishaji ni sawa na chanda na pete; ni mambo yanayokwenda sanjari, lakini hapa kuna haja ya kuwa na mang’amuzi, tayari kuthubutu kutenda na kwamba, huu ni utajiri na urithi wao kama Wayesuit. Tabia ya ukanimungu inaenea kwa haraka sana sehemu mbalimbali za dunia, lakini zaidi Barani Ulaya na madhara yake ni makubwa kwa maisha na utume wa Kanisa, kwa sababu mtu anayemkana Mwenyezi Mungu, hujitukuza mwenyewe, kinyume kabisa cha watakatifu wa Mungu ambao hutenda mengi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na Kanisa katika ujumla wake. Kumbe, watakatifu ni mwanga wa maisha adilifu na matakatifu

Huduma makini kwa watu wa Mungu
Huduma makini kwa watu wa Mungu

Ushindi dhidi ya ukanimungu unafumbatwa katika maisha adili na matakatifu; Injili ya upendo kwa watu wa Mungu na hasa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mama Kanisa haitaji wongofu wa shuruti, bali ushuhuda unaomwilishwa katika Injili ya upendo, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wanawake wanao mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Hivi karibuni, wanawake wamepewa dhamana na wajibu mkubwa kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican na mabadiliko yanaonekana; ni watu wanaotekeleza dhamana na majukumu yao kama wanawake wenye moyo wa kimama! Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya waamini ni muhimu sana kuliko hata uwepo wa Padre, kwa sababu mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Kuna Jumuiya za waamini zinazoongozwa na kuendeshwa na watawa pamoja na Makatekista. Hapa wanaadhimisha Ibada bila Padre, wanaadhimisha Sakramenti za Kanisa kadiri ya Sheria na taratibu za Kanisa wanahubiri na kutoa huduma kwa wagonjwa.

Jubilei ya Miaka 600 ya Chuo Kikuu cha Leuven
Jubilei ya Miaka 600 ya Chuo Kikuu cha Leuven

Chuo Kikuu cha Louvain “Katholieke Universiteit Leuven” kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 600 tangu kuanzishwa kwake kwa utashi wa Papa Martin V, katika Waraka wake wa Kitume wa “Sapientie immarcessibilis” uliochapishwa tarehe 9 Desemba 1425. Na hiki kikawa ni Chuo Kikuu cha kwanza cha Kikatoliki duniani. Kumbe, Mwaka wa Masomo 2024-2025 Chuo Kikuu cha Louvain “Katholieke Universiteit Leuven” kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 600 tangu kuanzishwa kwake. Chuo kina jumla ya wanafunzi 60, 000 na wafanyakazi ni 10, 000. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, aligusia kuhusu: dhamana na wajibu wa Chuo Kikuu kuwa ni mahali pa majiundo ya kiakili na kitamaduni, mahali pa kupanua ujuzi na maarifa; ukomo wa ujuzi unaosababiswa na mchoko wa kiakili, uwezo wa kufikiri na hatimaye, ni neno la shukrani kwa kupanua wigo wa ujuzi na maarifa unaojikita katika uwajibikaji na matumaini.

Dhamana na wajibu wa Chuo Kikuu katika maisha ya waamini
Dhamana na wajibu wa Chuo Kikuu katika maisha ya waamini

Baba Mtakatifu anasema, Chuo kikuu kina dhamana ya kuwajengea uwezo wanafunzi nyenzo za kufasiri mambo ya sasa na hivyo kupanga ya mbeleni. Vyuo vikuu ni chemchemi ya mwamko mpya wa maisha ya binadamu na kwamba, Chuo kikuu cha Kikatoliki kinapaswa kuwa ni chumvi na mwanga wa Injili kadiri ya Mapokeo ya Mama Kanisa. Huu ni mwaliko wa kupanua mipaka ya ujuzi na maarifa, ili vyuo hivi viweze kuwa ni chemchemi ya ujuzi na maarifa; mahali ambapo wanafunzi wanapata nyenzo za kufanya upembuzi yakinifu ili kufahamu na hatimaye, kuzungumzia kuhusu maisha, hii ni dhamana na wajibu mkubwa wa Chuo kikuu, tayari kuzama katika kutafuta ukweli, usiokuwa na mipaka. Baba Mtakatifu anawataka Wajesuit katika sekta ya elimu kujikita katika kanuni maadili na utu wema; tafiti na uchapishaji wa kazi zao, ili ziweze kusaidia maboresho ya maisha ya watu sehemu mbalimbali za dunia. Mababa wa Kanisa wanasema, utakatifu ni wito kwa watu wote wa Mungu. Ili kufikia azma hii, wanapaswa kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao Matunda ya Roho Mtakatifu. Huu ni mchakato wa utakatifu unaosimikwa katika maisha ya kila mmoja, kwa kutumia karama na mapaji yake. Mchakato wa kuwatangaza Padre Henri De Lubac na Padre Pedro Arupe Wajesuit unaendelea, lakini unahitaji muda mrefu zaidi kutokana na wingi wa maandiko yao.

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ni hitaji muhimu la nyakati hizi
Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ni hitaji muhimu la nyakati hizi

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Maadhimisho haya, yamezinduliwa kwa mkesha wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho mambo msingi katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika utamaduni wa kujadiliana, kusikilizana na kutenda kwa pamoja! Hakuna ujenzi wa Kanisa la Kisinodi pasi na toba, wongofu wa ndani na upatanisho. Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa maadhimisho ya Sinodi mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican anasema, Sinodi ni chombo cha kimisionari na uinjilishaji mpya unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari, mang’amuzi na hatimaye, utekelezaji wake unaofanywa na watu wote wa Mungu kadiri ya wito na nafasi zao katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Juhudi za kichungaji na kitaalimungu zisaidie kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kiekumene, kwa kumpokea Roho Mtakatifu ili kuweza kujifunza mengi kutoka kwa wengine na kuvuna kile ambacho Roho Mtakatifu amepanda ndani yao, ambacho kimekusudiwa kuwa ni zawadi kwa wengine.

Wakimbizi wana mchango katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Wakimbizi wana mchango katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha. Mambo haya yasipotekelezwa wakimbizi na wahamiaji wanaweza kugeuka na kuwa ni hatari sana kwa jamii inayowazunguka. Wakimbizi na wahamiaji wanao mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kama rasilimali watu kwa kazi na ongezeko la watu. Kanisa linakabiliwa na changamoto kubwa katika maisha na utume wake, lakini halina budi kuwekeza katika umisionari!

Papa Wayesuit Ubelgiji
10 October 2024, 15:13