Papa,Misa ya ufunguzi wa Sinodi ya Maaskofu:Tusikilize sauti ya Mungu na Malaika wetu!

Papa katika Misa ya ufunguzi wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu mjini Vatican,Oktoba 2,amesisitizia ushirikiano wazi ili kuwezesha mafanikio ya Sinodi na na kwamba tarehe 6 Oktoba atakwenda Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu kusali Rozari kwa Mama Maria na kuomba ushiriki wa washiriki wa Sinodi na wakati huo Oktoba 7,ameomba Sala na kufunga kwa ajili ya Amani duniani.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican uliosheheni waamini, mahujaji kutoka Pande za Dunia, na hasa washiriki wote wa Sinodi hiyo,  Baba Mtakatifu Francisko aliongoza Ibada ya Misa Takatifu ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa XVI wa kawaida wa Sinodi ya Maaskofu ambayo imezinduliwa tarehe 2 Oktoba na itaendelea hadi tarehe 27 Oktoba 2024. Baba Mtakatifu Francisko akianza  mahubiri alisema "Leo tunaadhimisha kumbukumbu ya liturujia ya Malaika Walinzi na tunafungua kipindi cha Mkutano wa Sinodi ya Maaskofu. Kwa kusikiliza kile ambacho Neno la Mungu linatushauri, tunaweza kwa hiyo kuleleza picha tatu kwa ajili ya tafakari yetu: sauti, kimbilio na mtoto.” Papa amefafanua kwanza sauti kwamba: "Katika safari kulekea Nchi ya ahadi, Mungu aliwahimiza watu wasikiliza “sauti ya Malaika” ambaye Yeye alimtuma (Kut 23,20-22). Ni picha ambayo inatugusa kwa karibu, kwa sababu hatua ya Sinodi ni safari, ambamo Bwana anaweka historia yake katika mikono yetu, ishara na matumaini makubwa ya watu kama vile kaka na dada waliotawanyika katika sehemu mbali mbali za Ulimwengu kwa kuhuishwa na imani sawa, kwa kusukumwa na shauku sawa ya utakatifu, ili pamoja nao na kwa ajili yao tutafute kuelekea njia za kupitia na kufikia mahali ambapo Yeye anataka kutupeleka.

Misa ya uzinduzi wa Sinodi tarehe 2 Oktoba 2024
Misa ya uzinduzi wa Sinodi tarehe 2 Oktoba 2024

Baba Mtatifu ameongeza kusema "Lakini kwa jinsi gani sisi tunaweza kujiweka kwenye usikivu wa “sauti ya Malaika.” Njia kwa hakika ni ili ya kuwa karibu na heshima na umakini katika sala na katika nuru ya Neno la Mungu, kwa mchango uliokusanywa kwa wote katika miaka hii mitatu ya kazi ya kina, ya kushirikishana, ya kukabiliana na ya uvumilivu wa nguvu ya kujitakasa kiakili na moyo. Hii ni kwa msaada wa Roho Mtakatifu, wa kusikiliza na kueleza sauti yaani, mawazo, matarajio, mapendekezo, kwa ajili ya kufanya mang’amuzi pamoja ya sauti ya Mungu ambaye anazungumza kwa Kanisa. Kama tulivyokumbusha mara nyingi, Papa ameongeza kusema, "mkutano wetu siyo bunge, lakini ni mahali pa kusikiliza katika umoja, ambao kama asemavyo Mtakatifu Gregori Mkuu, kile ambacho kila mmoja anacho kidogo, kipo kwa namna kamili kwa mwingine na kwa sababu baadhi wanaweza kuwa zawadi maalum na kila kitu kwa ndugu katika upendo wa Roho."

Misa ya Uzinduzi wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu
Misa ya Uzinduzi wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu

Kwakufafanua zaidi, Papa alisema "na ili litokee kuna sharti moja: kwamba tujikomboe wenyewe kutokana na kile, ambacho ndani yetu na kati yetu, kinaweza kuzuia “upendo wa Roho” wa kuunda maelewano katika utofauti. Wale wanaojidai kwa kiburi na kudai kuwa na haki za kipekee, hawawezi kusikia sauti ya Bwana(rej Mk 9:38-39). Kila neno lazima likaribishwe kwa shukrani na usahihi, ili kurudia kile ambacho Mungu ametoa kwa faida ya ndugu zetu (rej. Mt 10:7-8). Kwa maneno madhubuti, tujihadhari tusije tukabadilisha michango yetu kuwa hoja za kutetea au ajenda za kulazimisha, bali tuzitoe kama zawadi za kushiriki, hata kuwa tayari kutoa sadaka kwa kile ambacho ni maalum, ikiwa hii inaweza kutumika kuunda kitu kipya pamoja kulingana na mpango wa Mungu. Vinginevyo tutaishia kujifunga wenyewe katika mazungumzo kati ya viziwi, ambapo kila mtu anajaribu “kuvuta maji kwenye kinu chake,” bila kuwasikiliza wengine, na zaidi ya yote bila kusikiliza sauti ya Bwana. Hatuna masuluhisho ya matatizo tunayokabiliana nayo, lakini ni Yeye (rej. Yh 14:6), na tukumbuke kwamba jangwani hakuna mzaha: usipozingatia mwongozo, ukidhani kwamba wewe ni mtu binafsi wa kutosha, unaweza kufa kwa njaa na kiu, huku ukivuta wengine." Baba Mtakatifu Francisko ametoa onyo kwa washiriki hao kwamba "Kwa hiyo na tusikilize sauti ya Mungu na Malaika wake, ikiwa kweli tunataka kuendelea salama katika safari yetu kupitia mipaka na matatizo(rej. Zab 23:4).

Misa ya Ufunguzi wa Sinodi
Misa ya Ufunguzi wa Sinodi

Papa Francisko kuhusiana na hili aidha amesema: "Na hii inatuleta kwenye picha ya pili: kimbilio. Ishara ni ile ya mbawa zinazolinda: "chini ya mbawa zake utapata kimbilio" (Zab 91:4). Mabawa ni vyombo vyenye nguvu, vinavyoweza kuinua mwili kutoka chini na harakati zao kali, hata hivyo, licha ya kuwa na nguvu, zinaweza pia kupunguza na kukusanya, kuwa ngao na kiota cha kukaribisha watoto wadogo, wanaohitaji joto na ulinzi. Hii ni ishara ya kile ambacho Mungu anatufanyia, lakini pia ni kielelezo cha kufuata, hasa katika wakati huu wa Mkutano. Kati yetu, kaka na dada wapendwa, kuna watu wengi wenye nguvu, walioandaliwa, wenye uwezo wa kupanda juu na harakati kali za tafakari na maono ya kipaji. Yote haya ni utajiri, unaotuchangamsha, unatusukuma, unatulazimisha wakati fulani kufikiri kwa uwazi zaidi na kusonga mbele kimaamuzi, vilevile kutusaidia kubaki imara katika imani hata katika changamoto na magumu."

Wakati wa mahubiri ya Papa
Wakati wa mahubiri ya Papa

“Moyo ulio wazi, moyo katika mazungumzo. Lakini moyo uliofungwa katika nia ya mtu mwenyewe hautokani na Roho ya Bwana, huo  hautokani na Bwana. Kuufungua ni zawadi, "zawadi ambayo lazima iwe pamoja, kwa wakati unaofaa, na uwezo wa kupumzisha misuli na kuinama, kujitolea kwa kila mmoja kama kukumbatia kukaribisha na mahali pa makazi: kuwa, kama Mtakatifu Paulo wa VI alivyosema,: “nyumba ya ndugu […]. Hapa, kila mtu atajisikia huru kujieleza kwa hiari na kwa huru zaidi, ndivyo anavyoona zaidi uwepo wa marafiki karibu naye wanaowapenda na wanaoheshimu, kuthamini na kutaka kusikiliza wanachosema. Na kwetu sisi hii si mbinu ya “kuwezesha” tu, ni ukweli kwamba katika Sinodi kuna wawezeshaji, bali hii ni kutusaidia kusonga mbele; nilichosema si mbinu ya wawezeshaji” wa mazungumzo au wa  mawasiliano ya kikundi yenye nguvu kwa sababu: kukumbatia, kulinda na kujali kiukweli ni sehemu ya asili ya Kanisa.!

Papa Francisko amefafanua maneno haya ya "kukumbatia, kulinda na kujali." Kanisa kwa wito wake ni mahali pa kukutania kwa ukarimu, ambapo "msaada wa pamoja unahitaji maelewano kamili, ambapo kuna nguvu zake za kimaadili, uzuri wake wa kiroho na asili yake ya kielelezo hutokea. Neno hilo ni muhimu sana, 'maelewano.' Hakuna  walio wengi, wala wachache. Hii inaweza kuwa hatua ya kwanza kwenda mbele zaidi: cha muhimu na cha msingi ni maelewano, maelewano ambayo Roho Mtakatifu ndiye pekee anayeweza kuunda,  yeye ndiye Bwana wa maelewano, ambaye kwa tofauti nyingi ana uwezo wa kuunda sauti moja, lakini kwa sauti nyingi tofauti. Hebu tufikirie juu ya asubuhi ya Pentekoste, jinsi ambavyo Roho alivyoumba maelewano hayo katika tofauti.” Kanisa linahitaji “mahali pa amani na uwazi” ili kuumbwa kwanza katika mioyo ya watu, ambapo kila mtu anahisi kukaribishwa kama mtoto mikononi mwa mama yake (rej. Is 49:15; 66:13) na kama mtoto aliyeinuliwa kwenye shavu(Hos 11:4; Zab 103:13).

Na hapa tuko kwenye picha ya tatu ya mtoto. Papa Francisko amefafanua kuwa "Ni Yesu mwenyewe, katika Injili, ambaye “anamweka katikati” ambaye anawaonesha wanafunzi wake, akiwaalika wageuke na kuwa wadogo kama yeye. Walikuwa wamemuuliza ni nani aliyekuwa mkuu katika ufalme wa mbinguni: Akajibu kwa kuwatia moyo wajifanye wadogo kama mtoto. Lakini si hivyo tu: pia aliongeza kwamba kwa kumkaribisha mtoto kwa jina lake, unamkaribisha Yeye (taz Mt 18:1-5). Na kwetu sisi kitendawili hiki ni cha msingi. Sinodi, kwa kuzingatia umuhimu wake, kwa namna fulani inatutaka tuwe "wakubwa" katika akili, moyoni na katika maoni kwa sababu masuala ya kushughulikiwa ni makubwa na nyeti na matukio ambayo ndani yake ni mapana; hivyo yanahitaji kuingia katikati. Lakini kwa sababu hii hatuwezi kumudu kuondoa mtazamo wetu juu ya mtoto, ambaye Yesu anaendelea kumweka katikati ya mikutano yetu na meza zetu za kazi, ili kutukumbusha kwamba njia pekee ya kuwa sawa na kazi iliyotangulia,  tuliokabidhiwa, ni kujishusha, kujifanya wadogo na kukaribishana sisi kwa sisi kwa unyenyekevu. Aliye juu zaidi Kanisani ndiye anayejinyenyekeza zaidi. Tukumbuke kwamba ni kwa kujifanya wadogo ndipo Mungu “anatuonesha jinsi ukuu wa kweli ulivyo, kwa hakika, maana ya kuwa Mungu” ( Benedikto XVI, Mahubiri juu ya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, 11 Januari 2009). Si kwa bahati  tu kwamba Yesu alisema kwamba malaika wa watoto "sikuzote huona uso wa Baba [...] aliye mbinguni" (Mt 18: 10): yaani, wao ni kama "darubini" ya upendo wa Baba," Papa alisisitiza.

Misa ya uzinduzi wa Sinodi ya Maaskofu 2 Oktoba 2024
Misa ya uzinduzi wa Sinodi ya Maaskofu 2 Oktoba 2024

Kwa kuhitimisha Papa alisema “Ndugu na dada, tuanze tena safari hii ya kikanisa kwa jicho kuu kuelekea ulimwengu, kwa sababu jumuiya ya Kikristo daima iko katika huduma ya wanadamu, kutangaza furaha ya Injili kwa kila mtu. Kuna hitaji, hasa katika saa hii ya kushangaza ya historia yetu, wakati pepo za vita na moto wa ghasia unaendelea kusumbua watu na mataifa yote. Ili kuomba zawadi ya amani kutokana na maombezi ya Maria Mtakatifu, Dominika ijayo nitakwenda kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Maria Mkuu ambako nitasali Rozari Takatifu na kumwelekeza sala ya dhati kwa Bikira; ikiwezekana,pia ninawaomba ninyi washiriki wa Sinodi kuungana nami katika hafla hiyo. Na, siku itakayofuata, tarehe 7 Oktoba  ninaomba kila mtu aishi siku ya sala na kufunga kwa ajili ya amani ya ulimwengu. Twende pamoja. Hebu tumsikilize Bwana. Na tuongozwe na upepo wa Roho.”

Mahubiri ya Papa Francisko katika Ufunguzi wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu 2-27 Oktoba

 

02 October 2024, 10:24