Wajumbe wa mkutano mkuu wa 48 wa Shirika na Wamisionari wa Mateso ya Yesu, Ijumaa tarehe 25 Oktoba 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Wajumbe wa mkutano mkuu wa 48 wa Shirika na Wamisionari wa Mateso ya Yesu, Ijumaa tarehe 25 Oktoba 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.  (Vatican Media)

Mkutano Mkuu wa 48 wa Shirika la Mapadre wa Mateso: Mateso ya Kristo Kiini Cha Utume Wao

Papa Francisko katika hotuba yake amekazia kuhusu: Umuhimu wa kupyaisha ari na mwamko wa utume wao wa kimisionari mintarafu maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Maisha ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu na kwamba, Uinjilishaji wa kina unafumbatwa kwenye ushuhuda wa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu na kwamba, Wamisionari wa Mateso wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini. Mateso ya Kristo Kiini cha Utume Wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mikutano mikuu ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume inayoadhimishwa wakati huu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la kimisionari na Kisinodi ni muhimu sana katika maisha na utume wa kila Shirika la Kitawa na Kazi za Kitume, ili kulinda, kutunza na kuendeleza karama za waanzilishi wa Mashirika haya. Huu ni muda muafaka wa kujenga utamaduni wa kusikilizana; kuchunguza na kusoma alama za nyakati na kuzifafanua katika mwanga wa tunu msingi za Injili, ili kubaini masuala yenye uzito zaidi katika ulimwengu mamboleo. Rej, Gaudium et spes, 4. Ni wakati wa kufanya tafakari ya kina kuhusu: mang’amuzi, majiundo na Injili ya upendo. Huu ni muda muafaka kwa kila mwanashirika kujikita katika mchakato wa upyaisho wa maisha yake binafsi na ule wa kijumuiya, tayari kuzama katika maendeleo ya Shirika kwa sasa na kwa siku usoni. Tangu mwanzo wa Kanisa wamekuwepo watu kwa kutekeleza mashauri ya Injili walinuia kumfuasa Kristo Yesu kwa hiari zaidi na kumwiga kwa karibu, walienenda, kila mmoja kwa jinsi yake, katika maisha ya wakfu kwa Mungu ambao unapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo, na unaojitoa kabisa kwa Mungu na kwa msukumo wa Roho Mtakatifu, wanaamua kumfuata Kristo Yesu kwa karibu zaidi kwa kujisadaka na kuonesha upendo kwa Mungu, anayepaswa kupendwa kuliko vitu vyote. Rej. Perfectae caritatis, 1 na KKK, 916.

Umuhimu wa Kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari
Umuhimu wa Kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari

Ni katika muktadha huu, Mapadre wa Shirika la Mateso ya Yesu (Passionist Fathers) wanaadhimisha Mkutano mkuu wa 48 wa Shirika unaonogeshwa na kauli mbiu “Mimi hapa, nitume mimi.” Isa 6:8. Mateso ya Kristo Yesu ni chemchemi ya maisha na utume.” Mkutano mkuu umemchagua Mheshimiwa Giuseppe Adobati Carrara kuwa mkuu mpya wa Shirika. Wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika, Ijumaa tarehe 25 Oktoba 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia kuhusu: Umuhimu wa kupyaisha ari na mwamko wa utume wao wa kimisionari mintarafu maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Maisha ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu na kwamba, Uinjilishaji wa kina unafumbatwa kwenye ushuhuda wa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu na kwamba, Wamisionari wa Mateso wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini. Shirika hili kwa sasa lina wanovisi 150 kutoka sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, wanapaswa kuendelea kusali ili Bwana wa mavuno aweze kupeleka watenda kazi katika shamba lake. Huu ni wakati muafaka wa kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari, mintarafu maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa kuzingatia vipaumbele, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, waangalie uwezekano wa kutafuta njia mpya zitakazowawezesha watu wa Mungu kukutana na Kristo Yesu anayetaka watu wote waokoke na waweze kuufikia ukweli 1 Tim 2:4.

Mateso ya Kristo Yesu ni kiini cha maisha na utume wa Pasionisti!
Mateso ya Kristo Yesu ni kiini cha maisha na utume wa Pasionisti!

Huu ni mwaliko kwa wanashirika kuzama katika maisha ya taamuli, kwa kutembea pamoja katika umoja ili kutangaza na kushuhudia uwepo wa Mwenyezi Mungu kati yao, na ufunuo wa uzuri wa Kristo na Kanisa lake kwa kujikita katika sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu. Mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili utekelezwe kwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma.” Katika mahubiri na ushuhuda wao, watangaze huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu na kwamba, kifo cha Kristo Yesu Msalabani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma na upendo wa Mungu, shule ya kujifunza fadhila mbalimbali za Kikristo na nguvu inayowasaidia waamini kubeba mateso na magumu ya maisha.

Mimi hapa, nitume Isa 6:8
Mimi hapa, nitume Isa 6:8

Ni wajibu wao kuhakikisha kwamba, upendo wa Mungu unafahamika na kuthaminiwa na wengi, hali inayodai tafakari ya kina na maisha ya taamuli, ili kuwa tayari kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Karama ya Shirika lao, iwasaidie kuambata nadhiri ya ufukara, utii na usafi kamili; huku wakiwa tayari kujenga na kudumisha umoja na ushirika. Huu ni mwaliko kwa wanashirika kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi, tayari kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Kumbe, huu ni wito wa kumwilisha imani katika matumaini na hivyo kutenda kama Bikira Maria, Mtumishi mwaminifu wa Bwana, aliyeondoka kwa haraka kwenda kumhudumia binamu yake Elizabeti, changamoto na mwaliko wa kumwilisha imani katika matendo. Wamisionari wa Shirika la Mateso ya Yesu wanao wajibu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kwa kutembea pamoja, huku wakiambata na kushikamana kwa pamoja katika upendo, tafakari ya kina ya Neno la Mungu sanjari na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Mapadre wa Mateso
25 October 2024, 15:38