Mtakatifu Yohane Paulo II: Mtetezi wa Tunu Msingi za Maisha ya Ndoa na Familia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 23 Oktoba 2024 amewakumbusha waamini kwamba, Mama Kanisa tarehe 22 Oktoba, anamkumbuka Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili aliyezaliwa huko Wadowice nchini Poland tarehe 18 Mei 1920 na kupewa jina la Karol Josef Wojtyla. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kuwaweka chini ya ulinzi na maombezi ya Mtakatifu Yohane Paulo II watu wa Mungu nchini Poland. Katika maisha yao, daima waendelee kukumbuka huruma na upendo wa Kristo. Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro alikuwa ni mtetezi wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Ni vyema kukumbuka kwamba, nyumba ya Kikristo ni mahali ambapo watoto wanapokea tangazo la kwanza la imani. Kwa sababu hii, nyumba ya familia imeitwa kwa haki “Kanisa dogo la nyumbani,” Jumuiya ya neema na sala; shule ya fadhila za kibinadamu na mapendo ya Kikristo. Rej. KKK 1666. Nguvu ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia lazime ipate chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Waamini wasichoke kumwomba Roho Mtakatifu awakirimie nguvu ya kuweza kujisadaka kwa ajili ya maisha ya ndoa na familia na furaha ya kuishi kwa pamoja katika umoja! Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wawe na ujasiri na furaha ya kweli kama mashuhuda wa Kristo Yesu ndani ya familia, katika Parokia na katika mazingira mbalimbai ya maisha yao. Baba Mtakatifu amewataka watu wa Mungu kuwa makini na kuendelea kukesha, ili wasiwepo wajanja, siasa au kampeni zinazotaka kuwatenganisha na upendo wa Kristo Yesu. Na kamwe wasikubali kutumbukia katika kishawishi cha kupuuzia mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Watu wa Mungu nchini Poland wasimame kidete kupinga kile kinachobomoa na kudhohofisha ushirika wao na Kristo Yesu pamoja na Kanisa Kanisa lake.
Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 2 Juni 1997. Itakumbukwa kwamba, akiwa na umri wa miaka 20, alifiwa na wazazi wake pamoja na ndugu yake. Katika huzuni na upweke huu, Karol alivutwa sana na maisha na wito wa kipadre na hatimaye, akajiunga na seminari ya siri na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre, tarehe Mosi, Novemba 1946. Papa Pius XII kunako tarehe 4 Julai 1958 akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Kraków, nchini Poland. Akatekeleza dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu wa hali ya juu kabisa. Mtakatifu Paulo VI kunako tarehe 13 Januari 1964, akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kraków. Tarehe 26 Juni 1967 akateuliwa na Mtakatifu Paulo VI kuwa Kardinali. Akachaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki tarehe 16 Oktoba 1978, akiwa ni Papa wa 264 kuliongoza Kanisa Katoliki. Tarehe 22 Oktoba 1978 Mtakatifu Yohane Paulo II akasimikwa na kuanza kutekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ndiyo maana Kanisa linamkumbuka na kumwadhimisha kila mwaka ifikapo tarehe 22 Oktoba. Alifariki dunia tarehe 2 Aprili, 2005 na kuzikwa tarehe 8 Aprili 2005. Ilikuwa ni Mei Mosi, 2011, Baba Mtakatifu Benedikto XVI alipomtangaza kuwa Mwenyeheri mbele ya bahari ya watu waliofurika kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 27 Aprili 2014 sanjari na Papa Yohane XXIII, Muasisi wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, tarehe 22 Oktoba, 2019 Kanisa linapomkumbuka Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, anapenda kuchukua fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II sehemu mbali mbali za dunia. Mwaliko wa kudumu ni kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha. Mtakatifu Yohane Paulo II ameacha kumbukumbu ya kudumu katika akili na nyoyo za watu na kwamba, haitakuwa rahisi sana kuweza kufutika. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuiga karama na maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, sanjari na kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kukuza ari na mwamko na huduma za kimisionari. Itakumbukwa kwamba, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ulikuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, daima binadamu na mahitaji yake msingi, ndicho alichopenda kuona kwamba, kinavaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo!
Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni neema kubwa sana ambayo Mwenyezi Mungu amelijalia Kanisa lake. Neema hii ikamwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Mtakatifu Yohane Paulo II aliyetangaza na kushuhudia amana na utajiri wa Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Binadamu na mahitaji yake msingi, alipewa kipaumbele cha pekee kabisa katika maisha na utume wa Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II aliweza kufanya hija za kitume 104 nje ya Italia. Akabarikiwa kufanya hija za kichungaji 142 nchini Italia, daima maneno yake yaliambatana na vitendo; akagusa na kufariji mamilioni ya watu duniani, huku akitangaza na kushuhudia uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu kama kiini cha haki msingi za binadamu! Matokeo yake ni kuanguka kwa Ukuta wa Berlin kunako mwaka 1989. Kanisa likatoka kidedea na kusimama kifua mbele ili kupinga sera za kibaguzi zilizoigawa dunia, kati ya Kaskazini na Kusini: likaimarisha tunu msingi za maisha ya Kikristo, kwa kujikita katika haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi kama kanuni msingi za Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kufuata dira na mwongozo wa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, akaimarisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; kiasi hata cha kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Ni kiongozi aliyetambua na kuthamini sana mchango wa wanawake katika ustawi na maendeleo ya jamii na Kanisa katika ujumla wake, mambo yanayojionesha hata katika Nyaraka zake za kichungaji “MULIERIS DIGNITATEM dignitatem” yaani “Utu na wito wa mwanamke”. Alikazia sana umuhimu wa utakatifu wa maisha ya Kikristo kama kielelezo cha uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi cha kuthubutu kuwatangaza watakatifu wapya 482 na wenyeheri 1319, mwaliko na changamoto ya kumfuasa Kristo Yesu kama chemchemi ya utakatifu na utimilifu wa maisha ya Kikristo. Mtakatifu Yohane Paulo II, alikuwa na karama ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa kwa vijana, kwani hawa kwake walikuwa ni jeuri na matumaini ya Kanisa na jamii katika ujumla wake, utume ambao unaendelea kutekelezwa na Mama Kanisa hata nyakati hizi. Katika maisha na utume wake, aligusa medani mbali mbali za maisha ya binadamu; akaimarisha mafundisho msingi ya Kanisa yanayofumbatwa katika huruma ya Mungu, Roho Mtakatifu, Uhusiano kati ya imani na akili; Ari na mwamko wa kimisionari ndani ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II, hata dakika zake za mwisho wa maisha yake hapa duniani, katika udhaifu wa mwili na magonjwa, aliendelea kuwa ni: Shuhuda, Nabii na Chombo cha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Akafanikiwa kuonesha ukuu, utakatifu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.