Mwezi Oktoba Umetengwa Maalum Kwa Ajili ya Ibada Kwa Rozari Takatifu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu. Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima yaani Francis, Yacinta na Lucia aliwaagiza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani na amani duniani. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake, Jumatano tarehe 9 Oktoba 2024 amewakumbusha waamini kwamba, Mwezi Oktoba, umetengwa rasmi na Mama Kanisa kwa ajili ya Ibada ya Rozari Takatifu. Anawaalika waamini kuendelea kuwa waaminifu katika Mapokeo haya kwa kujitahidi kusali Rozari Takatifu, kama mtu binafsi, jumuiya, lakini inapendeza zaidi, ikiwa kama wanafamilia watasali na kutafakari kwa pamoja historia ya kazi ya ukombozi iliyotekelezwa kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Kwa njia ya Rozari Takatifu, waamini wanamshirikisha Bikira Maria furaha, machungu na matumaini yao. Baba Mtakatifu anawatakia waamini wote maadhimisho mema na baraka kwa mwezi Oktoba 2024, katika shida na mahangaiko yao wamkimbilie Bikira Maria wa Rozari Takatifu na hasa kwa ajili ya kuombea amani duniani na kwa namna ya pekee amani nchini Ukraine, Palestina, Israel, Myanmar na Sudan.
Itakumbukwa kwamba, Papa Leo XIII kunako mwaka 1884 alitangaza rasmi kuwa mwezi wote wa Oktoba utakuwa mwezi wa kutafakari na kusali Rozari Takatifu, kama kumbukumbu endelevu ya ushindi ambao Wakristo waliupata katika vita vya Lepanto tarehe 7 Oktoba 1571. Lengo ni kumheshimu na kumshukuru Bikira Maria, ambaye kwa ulinzi na tunza yake ya kimama aliwawezesha Wakristo tarehe 7 Oktoba 1571 kuibuka kidedea katika vita. Naye Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” anamwangalia Bikira Maria aliyyejitahidi kumwilisha “Heri za Mlimani” muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu, kuliko mtakatifu yoyote yule. Ni mwanamke aliyefurahia uwepo wa Mungu katika maisha yake na kuhifadhi yote katika sakafu ya moyo wake! Bikira Maria ni Mtakatifu kuliko watakatifu wote. Ni kimbilio la waamini katika ulinzi na tunza ya kimama. Anawafundisha na kuwasindikiza waamini katika utakatifu wa maisha; anawalinda bila kuwahukumu; anawafariji, kuwaombea na kuwatakatifuza kwa uwepo wake mwanana, changamoto na mwaliko kwa waamini kumkimbilia katika sala, lakini zaidi kwa njia ya tafakari ya Rozari Takatifu.
Baba Mtakatifu anasema, Rozari Takatifu ni muhtasari wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Sala ya Rozari ni njia muafaka kabisa ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya upendo kwa jirani wenye shida na mahangaiko mbalimbali wanaokumbukwa katika Sala ya Rozari Takatifu. Kwa njia ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kila mtu ajitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake katika mchakato wa kuponya ulimwengu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumtaza Kristo Yesu aliyeanzisha Ufalme wa Mungu kwa ujasiri, kwa tafakuri na kwa njia ya ushuhuda wa maisha, ili kwa pamoja waweze kuujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani ili kukuza na kudumisha haki, furaha, uponyaji na wokovu kwa wale wote wanaoteseka kwa magonjwa na kifo. Baba Mtakatifu anawatakia heri na faraja wazee, vijana, wagonjwa na wanandoa wapya. Kila mtu katika hali na nafasi yake, ajitahidi kuwa mkarimu, kwa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi. Wakubali kupokea kwa imani na matumaini majaribu, matatizo na changamoto za maisha, huku wakishirikishana upendo kama sehemu ya ujenzi wa familia ya kweli inayosimikwa katika msingi wa amani na utulivu.