Askofu Paskalis Bruno Syukur, O.F.M amemwomba Papa Francisko kutokumtangaza kuwa Kardinali tarehe 7 Desemba 2024 ili aendelee kukomaa katika maisha na utume wa Kipadre, Huduma kwa Kanisa na kwa watu wa Mungu. Askofu Paskalis Bruno Syukur, O.F.M amemwomba Papa Francisko kutokumtangaza kuwa Kardinali tarehe 7 Desemba 2024 ili aendelee kukomaa katika maisha na utume wa Kipadre, Huduma kwa Kanisa na kwa watu wa Mungu.  (https://ofm.org/en/pope-francis-has-named-new-cardinals.html)

Papa Francisko Aridhia Ombi la Askofu Sykur Kutosimikwa Kuwa Kardinali!

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Paskalis Bruno Syukur, O.F.M., wa Jimbo la Bogor, Indonesia la kutosimikwa kuwa Kardinali hapo tarehe 7 Desemba 2024. Sababu kuu ni kutaka kuendelea kukua na hatimaye, kukomaa katika maisha na utume wa Kipadre, Huduma kwa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wake. Askofu Syukur alizaliwa mwaka 1962, Kaweka nadhiri mwaka 1989, Daraja Takatifu ya Upadre 1989; Uaskofu mwaka 2013

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Makardinali kimsingi ndio washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kukoleza juhudi za toba, haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu; kwa kukuza na kudumisha: Haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu, ili watu waweze kuishi katika mazingira bora zaidi. Ukardinali umegawanyika katika ngazi kuu tatu: Kardinali Askofu, Kardinali Padre na Kardinali Shemasi. Uteuzi wa Makardinali wapya na hatimaye kusimikwa kwao ni changamoto kubwa inayowataka kujizatiti zaidi katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu, kwa kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika matendo; daima wakijielekeza zaidi katika huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Makardinali wanajitambulisha kwa mavazi mekundu, wanaitwa kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, tayari kuwashirikisha watu wa Mataifa, ile furaha ya Injili. Ni mwaliko wa huduma makini kwa watu wa Mungu.

Makardinali wapya 20 watasimikwa tarehe 7 Desemba 2024
Makardinali wapya 20 watasimikwa tarehe 7 Desemba 2024

Jicho la kibaba linalooneshwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa maskini na wale wote wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii, ni chachu ya matumaini na mapendo ambayo yanapaswa kutawala katika maisha ya watu! Urika wa Maaskofu hauwezi kuwa na mamlaka usipounganika na Baba Mtakatifu, aliye Mwandamizi wa Petro, Mtakatifu na Mtume; kwa nguvu ya wadhifa wake kama Wakili wa Kristo na Mchungaji wa Kanisa lote, ana mamlaka katika Kanisa, iliyo kamili, ya juu kabisa na iwahusuyo wote (plenam, supremama et universalem potestatem) ambayo anaweza kuyatimiza kwa uhuru. Urika wa Maaskofu ni urithi wa urika wa Mitume katika kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Rej. Lumen gentium, 22-27.

Makardinali ni washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro
Makardinali ni washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro

Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 6 Oktoba 2024 ametangaza majina ya Makardinali wapya ishirini na moja, watakaosimikwa rasmi tarehe 7 Desemba 2024 katika mkesha wa maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kukingiwa Dhambi ya Asili. Kati ya Makardinali wapya yumo Kardinali Angelo Acerbi, mwenye umri wa miaka 99. Mama Kanisa anatambua na kuthamini mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa. Yumo pia Askofu Mykola Bychok, C.Ss.R., wa Jimbo la “Saints Peter na Paul, huko Melbourne nchini Ukraine, Yeye ana umri wa miaka 44. Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Paskalis Bruno Syukur, O.F.M., wa Jimbo Katoliki la Bogor, Indonesia la kutosimikwa kuwa Kardinali hapo tarehe 7 Desemba 2024. Sababu kuu ni kutaka kuendelea kukua na hatimaye, kukomaa katika maisha na utume wa Kipadre, Huduma kwa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wake. Itakumbukwa kwamba, Askofu Paskalis Bruno Syukur, O.F.M., alizaliwa tarehe 17 Mei 1962. Mara baada ya masomo yake ya kitawa na kipadre tarehe 22 Januari 1989 akaweka nadhiri zake za kitawa kwenye Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko Wakapuchini “OFM.Cap. Tarehe 2 Februari 1989 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 21 Novemba 2013 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Borgor, nchini Indonesia.

Kardinali
23 October 2024, 14:30