Papa Francisko atoa ombi la kuombea amani na tupambanie amani!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kuombea amani, na kupambania amani, ndiyo ulikuwa mrejesho wa wito wa Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena kwa ulimwengu ulioharibiwa na vurugu kwa waamini na wengine. Haya yalisikikia mwishoni mwa Katekesi yake akitoa salamu kwa waamini na mahujaji kutoka pande zote dunia katika Uwanja wa Mtakatifu Petro Jumatano tarehe 16 Oktoba 2024.
Akitoa salamu kwa lugha ya kitaaliano, Baba Mtakatifu Francisko amehimiza kukumbuka maeneo yaliyoathiriwa na migogoro. "Tusisahau nchi zilizo kwenye vita. Tusisahau Ukraine, Palestina, Israel, Myanmar inayoteswa
Vita ni kushindwa
Papa Francisko amebainisha kwamba “vita daima, ni kushindwa, ni kushindwa." Na tena "Tusisahau kuomba amani. Tupambanie amani.”
Kumbukumbu ya Mwenyeheri Popiełuszko
Katika salamu zake kwa lugha ya Kipoland, Papa Fransisko alikumbuka ushuhuda wa Padre Mwenyeheri Jerzy Popiełuszko wakati wa mkutano uliofanyika mjini Roma kwa ajili ya kuadhimisha miaka 40 ya kifo chake cha kishahidi, kilichotokea mnamo Oktoba 1984 wakati wa utawala wa kikomunisti nchini Poland. Mwenyeheri huyu aliyefundisha kuushinda ubaya kwa wema, awasaidie katika kujenga umoja katika roho ya ukweli na kuheshimu hadhi ya mwanadamu.
Salamu kwa washiriki wa Kongamano la Kimataifa la Radio Maria
Mwishoni pia Baba Mtakatifu Francisko aliwasalimia washiriki wa Kongamano la Kimataifa la Radio Maria, wanaotoka nchi mbalimbali duniani, ambapo "aliwasihi kueneza tunu za udugu na mshikamano, kwa kufanya kuwa mwangwi wa maisha ya Kanisa.”
Siku kuu ya Mtakatifu Ignatius wa Antiokia
Hatimaye Baba Mtakatifu Francisko aliwasalimia vijana, wagonjwa, wazee na wenye ndoa mpya na kuwakumbusha kwamba "tarehe 17 Oktoba, ni kumbukumbu ya kiliturujia ya Mtakatifu Ignatius wa Antiokia, “mchungaji mwenye bidii kwa upendo kwa Kristo. Kielelezo chake na kisaidie kila mtu kugundua tena furaha ya kuwa Wakristo.”