Sala Maalum Kwa Ajili ya Kuombea Amani Ulimwenguni 2024
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 6 Oktoba 2024 baada ya kuwaongoza watu wa Mungu kusali Rozari Takatifu kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma, kwa ajili ya kuombea amani duniani, aliwaalika waamini kuunganika pamoja naye kusali sala ifuatayo: Ee Bikira Maria, Mama yetu, tuko hapa tena mbele yako. Unajua uchungu na dhiki zinazoelemea mioyo yetu wakati huu. Tunakutazama, tunajizamisha machoni pako na tunajikabidhi kwa Moyo wako Mtakatifu. Kwako wewe pia, Ee Mama Bikira Maria, maisha yamekuwekea majaribu magumu na hofu za kibinadamu, lakini umekuwa jasiri kiasi cha kumkabidhi Mwenyezi Mungu kila kitu, umemjibu kwa upendo, umejitoa sadaka bila kujibakiza.
Kama Mwanamke wenye upendo shupavu, ulikwenda haraka kumsaidia Elizabeti, ulifahamu mara moja hitaji la wanandoa wakati wa harusi huko Kana ya Galilaya; kwa ujasiri, pale Mlimani Kalvari ukaangaza usiku wa maumivu kwa tumaini la Pasaka. Hatimaye, kwa huruma ya Mama, uliwapa ujasiri wanafunzi walioogopa katika Chumba cha juu na, pamoja nao, ukakaribisha zawadi ya Roho Mtakatifu. Na sasa tunakuomba: karibu usikilize kilio chetu! Tunahitaji macho yako ya upendo ambayo yanatualika tumtumaini Mwanao Kristo Yesu, Wewe uliye tayari kukaribisha maumivu yetu uje kutusaidia katika nyakati hizi zinazokandamizwa na dhuluma, ukiwa na vita, futa machozi katika nyuso za mateso za wale wanao omboleza kutokana na kifo cha wa wapendwa wetu, utuamshe kutoka katika dhoruba kali ambayo imetia giza njia yetu na uondoe mioyo yetu kutoka kwenye silaha za jeuri, ili unabii wa Isaya utimie mara moja: “Nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe. (Isa 2:4).
Geuza macho yako ya kimama kwa familia ya kibinadamu, ambayo imepoteza shangwe ya amani na imepoteza hisia ya udugu wa kibinadamu. Uombee ulimwengu wetu ulio hatarini, ili uthamini uhai na kukataa vita, uwatunze wanaoteseka, maskini, wasio na ulinzi, wagonjwa na wanaoteseka, na kulinda Mazingira nyumba ya wote. Tunaomba rehema za Mwenyezi Mungu kupitia kwako, Ewe Bikira Maria Malkia wa Amani! Geuza mawazo ya wale wanaochochea chuki, nyamazisha kelele za silaha zinazozalisha kifo, zima jeuri inayofukuta moyoni mwa mwanadamu na kuhamasisha miradi ya amani katika matendo ya wale wanaotawala Mataifa.
Ee Malkia wa Rozari Takatifu, fungua mafundo ya ubinafsi na uondoe mawingu meusi ya uovu. Tujaze huruma yako, utuinue kwa mkono wako unaotujali na utupe sisi watoto wako mabembelezo yako ya kimama, ambayo yanatufanya tuwe na matumaini ya ujio wa ubinadamu mpya ambapo "... jangwa litakuwa bustani na bustani itachukuliwa kuwa msitu. Sheria itakaa jangwani na haki itatawala katika bustani. Kutenda haki kutazalisha amani…” (Isa 32:15-17). Ee Bikira Maria na Mama, Afya ya Warumi Utuombee! “Salus Populi Romani, Prega Per Noi!