Tafuta

Papa Francisko:Tuna imani ni Roho Mtakatifu atoaye uzima kwa Baba na Mwana!

Papa katika katekesi tarehe 16 Oktoba 2024 alielekeza njia ya Kanisa ya kulewa umungu kamili katika Nafsi ya tatu ya Utatu,akibainisha kwamba Roho Mtakatifu ndiye anayewapatia waamini maisha mapya.Tunaposema ninasadiki Roho Mtakatifu wakati wa misa tunathibitisha kuwa Roho ni Mungu na lazima iendelezwe hata kwa ambao,mara nyingi bila kosa lao,wananyimwa na hawawezi kutoa maana ya maisha.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican Jumatano tarehe 16 Oktoba 2024, amendeleza katekesi ya 9 ya Mada: “Naamini katika Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu katika imani ya Kanisa.” Akiwageukia waamini na mahujaji wengi katika uwanja huo alisema: “Kwa katekesi ya leo, tutaendelea kutoka kwa yale ambayo Roho Mtakatifu alitufunulia katika Maandiko Matakatifu hadi jinsi Yeye aliyepo na anafanya kazi katika maisha ya Kanisa, katika maisha yetu ya Kikristo.” Baba Mtakatifu aliendelea “Katika karne tatu za kwanza, Kanisa halikuhisi haja ya kutoa uundaji wa wazi wa imani yake katika Roho Mtakatifu. Kwa mfano, katika Imani ya kale zaidi ya Kanisa, ile inayoitwa Alama ya Mitume, baada ya kutangaza: “Nanasadiki Mungu Baba Mwenyezi, Muumba wa mbingu na nchi, na katika Yesu Kristo, Mwanawe pekee, Bwana wetu, aliyezaliwa, akafa, akashuka kuzimu, akafufuka kutoka kwa wafu na kupaa mbinguni”, aliongeza: “Ninasadiki katika Roho Mtakatifu” na hakuna zaidi, bila maelezo yoyote.

Papa akipiga picha na makundi ya wanahija
Papa akipiga picha na makundi ya wanahija

Papa ameongeza "Lakini ni uvumi uliolisukuma Kanisa kufafanua imani hii. Wakati mchakato huu ulipoanza na Mtakatifu Athanasius katika karne ya nne, ilikuwa uzoefu aliokuwa nao wa utakaso na uchaguzi wa Roho Mtakatifu ambao uliongoza Kanisa kwenye uhakika wa umungu kamili wa Roho Mtakatifu. Hii ilitokea wakati wa Mtaguso wa Kiekumene wa Konstantinopoli mnamo mwaka 381, ambao ulifafanua umungu wa Roho Mtakatifu kwa maneno yanayojulikana sana ambayo bado tunayarudia leo hii katika  kanuni ya Imani: “Ninasadiki Roho Mtakatifu, Bwana, mleta uzima, atokaye kwa Baba na Mwana, ambaye pamoja na Baba na Mwana anaabudiwa na kutukuzwa, ambaye amesema kupitia manabii.”

Papa wakati wa Katekesi 16 Oktoba 2024
Papa wakati wa Katekesi 16 Oktoba 2024

Kusema kwamba Roho Mtakatifu “ni Bwana” ilikuwa sawa na kusema kwamba  yeye "Anashiriki “Ubwana” wa Mungu, na kwamba Yeye ni wa ulimwengu wa Muumba, si wa viumbe! Uthibitisho wenye nguvu zaidi ni kwamba anastahili utukufu na kuabudiwa sawa na Baba na Mwana. Baba Mtakatifu amefafanua kuwa “Ni hoja ya usawa katika heshima, inayopendwa na Mtakatifu Basil Mkuu, ambaye alikuwa mbunifu mkuu wa kanuni hiyo: Roho Mtakatifu ni Bwana, Yeye ni Mungu. Ufafanuzi wa Mtaguso haukuwa mahali pa kuwasili, bali wa kuondoka. Na kwa hakika, mara tu sababu za kihistoria zilizokuwa zimezuia uthibitisho wa wazi zaidi wa umungu wa Roho Mtakatifu ziliposhindwa, hili lilitangazwa kwa ujasiri katika ibada ya Kanisa na katika talimungu yake.

Papa akisalimiana na wanandoa wapya
Papa akisalimiana na wanandoa wapya

Mtakatifu Gregory wa Nazianzus, baada ya Mtaguso, aliendelea kusema hivi bila kusita: “Je, Roho Mtakatifu basi ni Mungu? Hakika! Je, Yeye ni thabiti? Ndiyo, ikiwa Yeye ni Mungu wa kweli” (Oratio 31, 5.10). Je, Kanuni ya  imani tunasali kila Dominika kwenye Misa inatuambia nini, sisi waamini wa leo: “Nasadiki katika Roho Mtakatifu?” Hapo awali, ilihusika zaidi na taarifa kwamba Roho Mtakatifu “hutoka kwa Baba.” Upesi Kanisa la Kilatini liliongezea kauli hii kwa kuongeza, katika kanuni ya  Imani ya Misa, kwamba “Roho Mtakatifu hutoka pia kwa Mwana," Papa Francisko alifafanua. Kwa kuendelea Baba Mtakatifu Francisko alibainisha kwamba: “Kwa kuwa katika Kilatini usemi “na kutoka kwa Mwana” unaitwa ‘Filioque’, hilo lilizua mzozo unaojulikana kwa jina hili, ambao umekuwa sababu (au kisingizio) cha mabishano na migawanyiko mingi kati ya Kanisa la Mashariki na Kanisa la Magharibi. Kwa hakika sivyo ilivyo kuzungumzia suala hili hapa, ambalo, zaidi ya hayo, katika mazingira ya mazungumzo yaliyoanzishwa kati ya Makanisa haya mawili, yamepoteza uhasama wa siku za nyuma na leo hii inatuwezesha kutumainia kukubalika kamili kwa pande zote mbili, kama moja ya mambo makuu ya tofauti zilizopatanishwa.”

Papa akimpungia mkono Mtoto
Papa akimpungia mkono Mtoto

Papa Francisko kwa njia hiyo amesisitiza kwamba “ Ninapenda kusema hivi: “tofauti zilizopatanishwa.” Miongoni mwa Wakristo kuna tofauti nyingi: huyo ni wa shule hii, na mwingine ile; mtu huyu ni Mprotestanti, mtu huyo… Jambo muhimu ni kwamba tofauti hizi zipatanishwe, katika upendo wa kutembea pamoja. Baada ya kushinda kikwazo hiki, leo hii tunaweza kuthamini haki muhimu zaidi kwetu ambayo imetangazwa katika kifungu cha Imani, ambayo ni kwamba Roho Mtakatifu ndiye “anatoa uzima, yaani mtoaji wa uzima.” Hebu tujiulize: Roho Mtakatifu hutoa maisha gani? Hapo mwanzo, katika uumbaji, pumzi ya Mungu inampatia Adamu uhai wa asili; sanamu ya matope inafanywa kuwa “kiumbe hai” (rej. Mwa 2:7). Sasa, katika uumbaji mpya, Roho Mtakatifu ndiye anayewapatia waamini uzima mpya, uzima wa Kristo, uzima usio wa kawaida, kama watoto wa Mungu.

Ngoma ya kiutamaduni waliomchezea Papa
Ngoma ya kiutamaduni waliomchezea Papa

Paulo aliweza kusema: “Sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniweka huru mbali na sheria ya dhambi na mauti” (Rm 8:2). Katika haya yote, ziko wapi habari kuu na za kufariji kwetu? Ni kwamba uzima tuliopewa na Roho Mtakatifu ni uzima wa milele! Imani hutuweka huru kutokana na hofu ya kukiri kwamba kila kitu kinaishia hapa, kwamba hakuna ukombozi kwa ajili ya mateso na ukosefu wa haki unaotawala enzi kuu duniani. Neno lingine la Mtume linatuhakikishia hili: “Ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.” (Rm 8:11). Roho anakaa ndani yetu, Yeye yu ndani yetu. Tuimarishe imani hii pia kwa wale ambao, mara nyingi bila kosa lao wenyewe, wamenyimwa imani hiyo na hawawezi kuyapa maana maisha. Na tusisahau kumshukuru, ambaye kwa kifo chake, alipata zawadi hii isiyo na kifani kwa ajili yetu!

Katekesi ya Papa 16 Oktoba 2024
16 October 2024, 10:31