Papa na wajumbe wa G7:ishara ya matumaini katika dunia inayopuuza watu wenye ulemavu
Na Angella Rwezaula – vatican.
Baba Mtakatifu amehutubia mjini Vatican, tarehe 17 Oktoba 2024 na jopo la Mawaziri wawakilishi wa Nchi Saba zilizoendelea kiviwanda (G7), katika fursa ya mkutano wao wa Kwanza kuhusu Ushirikishwaji na Ulemavu uliofanyika chini ya urais wa Italia na kuhitimishwa tarehe 16 Oktoba 2024 huko Umbria, baada ya siku tatu za majadiliano na mjadala. Mwishoni mwa mkutano huko, “Mkataba wa Solfagnano” ulitiwa saini, ambapo matokeo ya kazi ya mandhari za kimsingi kama vile ushirikishwaji, upatikanaji, maisha ya uhuru na ushujaa wa watu ambapo Papa amebainisha kwamba ni mandhari zinazounganishwa na “maono ambayo kwayo, Kanisa linajikita nayo kuhusu hadhi ya binadamu. “ Baba Mtakatifu alianza na salamu kwa wote na kuwashukuru kwa jitihada zao za kukuza utu na haki za watu wenye ulemavu.
Papa amesema kwamba Mkutano huo nao katika hafla ya G7, ni ushahidi thabiti wa hamu ya kujenga ulimwengu wa haki na jumuishi zaidi, ambapo kila mtu, kwa uwezo wake mwenyewe, anaweza kuishi kwa ukamilifu na kuchangia ukuaji wa jamii. Amemshukuru Waziri wa Ulemavu wa Italia, Mheshimiwa Alessandra Locatelli, kwa kuendeleza mpango huu muhimu. Papa alisema: “Jana mlitia saini ya “Mkataba wa Solfagnano,” matunda ya kazi yenu juu ya masuala ya msingi kama vile ujumuishaji, ufikiaji, maisha ya kujitegemea na uwezeshaji wa watu. Mada hizi pia zimo katika maono ya Kanisa ya hadhi ya binadamu.” Baba Mtakatifu akiendelea amesema: “Kwa hakika, kila mtu ni sehemu muhimu ya familia ya wanadamu ya ulimwenguni pote, na hakuna mtu anayepaswa kuangukia kwenye utamaduni wa kutupa ambao hutokeza ubaguzi na kuharibu jamii.”
Kwa kusisitiza Papa alisema “Kwanza, ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu lazima kutambuliwa kama kipaumbele na nchi zote. Cha kusikitisha ni kwamba hata leo katika baadhi ya nchi watu wanaona ni vigumu kutambua hadhi sawa ya watu kama hao (taz. Fratelli Tutti, 98). Kuunda ulimwengu mjumuisho kunahusisha sio kurekebisha miundo tu, bali pia kubadilisha mawazo, ili watu wenye ulemavu waweze kuchukuliwa kuwa washiriki kamili katika maisha ya kijamii. Hakuwezi kuwa na maendeleo ya kweli ya binadamu bila ushiriki wa wanajamii walio hatarini zaidi. Kwa hivyo, ufikiaji wa watu wote ni lengo kubwa la kufuatwa, ili kila kizuizi cha kimwili, kijamii, kiutamaduni na kidini kiweze kuondolewa na kila mtu aweze kuwezeshwa kuendeleza au vipaji vyake na kuchangia manufaa ya wote katika kila hatua ya maisha, tangu utoto hadi uzee. Kutoa vifaa na huduma za kutosha kwa watu wenye ulemavu sio tu suala la usaidizi wa kijamii, lakini pia haki na heshima kwa utu wao. Nchi zote zina wajibu wa kuhakikisha hali zinazohitajika kwa ajili ya maendeleo fungamani ya kila mtu ndani ya jumuiya shirikishi (taz. Fratelli Tutti, 107).
Baba Mtakatifu kwa njia hiyo alisema “basi, ni muhimu kufanya kazi pamoja katika kuwawezesha watu wenye ulemavu kuchagua njia yao wenyewe ya maisha, bila minyororo ya ubaguzi. Binadamu awe katikati ya maisha na sio wa mwisho! Hii ina maana ya kuimarisha uwezo wa kila mtu na kutoa fursa za ajira yenye heshima. Kumtenga mtu kutokana na uwezekano wa kazi ni aina kubwa ya ubaguzi (taz. Fratelli Tutti, 162). Jambo hilo hilo linaweza kusemwa kuhusiana na ushiriki katika hafla za kiutamaduni na shughuli za michezo: kuwatenga watu wenye ulemavu ni dharau kwa utu wa mwanadamu. Papa Francisko aidha amsema“Teknolojia mpya pia zinaweza kuthibitisha kuwa njia nzuri ya kuongeza ushirikishwaji na ushiriki, mradi tu zifanywe kupatikana kwa kila mtu.
Teknolojia hizi zinahitaji kuelekezwa kwenye manufaa ya wote na kuwekwa katika huduma ya utamaduni wa kukutana na mshikamano. Teknolojia inapaswa kutumiwa kwa busara, ili kuzuia kutokuwepo kwa ukosefu wa usawa zaidi na kusaidia kushinda zile ambazo tayari zipo. Hatimaye, katika kuzungumza juu ya kujumuika, ni lazima tuzingatie mahitaji ya dharura ya dunia, makao yetu ya pamoja. Hatuwezi kuwa tofauti na dharura za kibinadamu zinazohusishwa na migogoro ya hali ya tabianchi na migogoro, ambayo ina athari kubwa kwa wale walio katika hatari zaidi, ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu (taz. Laudato Si', 25). Ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba wale wenye ulemavu hawaachwi nyuma katika hali kama hizi, na wanatunzwa na kulindwa ipasavyo. Kinachohitajika ni mfumo wa kuzuia na kukabiliana na dharura ambao unazingatia mahitaji yao maalum na dhamana ya kwamba hakuna mtu anayetengwa na ulinzi na usaidizi.
Baba Mtakatifu Francisko kwa kusisitiza zaidi alibanisha kwamba anaiona kazi yao kama “ishara ya matumaini kwa ulimwengu ambao mara nyingi huwapuuza watu wenye ulemavu.” Kwa njia hiyo amewasihi “wavumilie katika juhudi zao, wakichochewa na imani na kusadiki kwamba kila mtu ni zawadi ya thamani kwa jamii. Mtakatifu Francis wa Assis, ambaye alitoa ushuhuda wa upendo usio na kikomo kwa walio hatarini zaidi, anatukumbusha kwamba utajiri wa kweli unapatikana katika kukutana kwetu na wengine, hasa kwa wale ambao wana mwelekeo wa “kutupwa na utamaduni wa ustawi Kwa pamoja tunaweza kujenga ulimwengu ambamo utu wa kila mtu unatambulika na kuheshimiwa kikamilifu. Mungu awabariki na kuwasindikiza katika shughuli hii muhimu.” Papa Francisko amehitimisha.