Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 24 Oktoba 2024 amekutana na kuzungumza na Mapadre waungamishaji kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 24 Oktoba 2024 amekutana na kuzungumza na Mapadre waungamishaji kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.  (Vatican Media)

Sakramenti ya Upatanisho Ni Chemchemi ya Huruma na Upendo wa Mungu

Papa Francisko tarehe 24 Oktoba 2024 amekutana na Mapadre waungamishaji kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama sehemu ya kumbukizi ya miaka 240 tangu Papa Clement XIV katika Barua yake binafsi “Motu proprio, Miserator Dominus” alipowakabidhi Ndugu Wadogo Wakonventuali huduma ya maungamano kwa watu wa Mungu wanaotembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wanaokadiriwa kuwa ni arobaini elfu kwa kila siku. Toba!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho mwamini anaonja na kusikia huruma ya Mungu katika maisha yake, kwani Mungu ni mwingi wa rehema na kwa mapenzi yake makuu anampenda mwanadamu, hata pale anapokuwa mfu kutokana na dhambi zake, bado Mungu anaendelea kumpenda na kumpatia nafasi ya kutubu, kuongoka na kuanza upya hija ya maisha yake ya kiroho. Mdhambi aliyetubu na kuungama dhambi zake vyema, anarudisha mahusiano na Kristo Mfufuka na hivyo kuendeleza ile neema ya Utakaso aliyoipokea wakati wa Sakramenti ya Ubatizo. Mapadre ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika Sakramenti ya Upatanisho, ambayo wanapaswa kuiadhimisha kwa kuvaa sura ya Baba mwenye huruma! Ni katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu, mwamini anaonja huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu; ni mahali ambapo mwamini kutoka katika undani wake, anaguswa na kupyaishwa, huku akitiwa shime ya kusonga mbele katika hija ya maisha ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.

Huduma ya kuwaungamisha watu wa Mungu Kanisa kuu la Mt. Petro
Huduma ya kuwaungamisha watu wa Mungu Kanisa kuu la Mt. Petro

Sakramenti ya Upatanisho inapania kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya ndani kabisa na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ni kiini cha Injili na ni njia muafaka ya uinjilishaji mpya unaojikita katika mchakato wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji! Umefika wakati kwa waamini kujenga utamaaduni wa kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia ikiwa kama maisha yao yanaendana na utu wema sanjari na kweli za Kiinjili zinazotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na haki” anasema, huruma ya Mungu inapaswa kuendelezwa katika medani mbalimbali za maisha ya watu kama utimilifu wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu!

Upatanisho ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu
Upatanisho ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu

Idara ya Toba ya Kitume ni mahakama ya huruma ya Mungu inayogusa kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Ni mahakama inayomwezesha mwamini kupata dawa ya maisha yake ya kiroho kutoka katika huruma ya Mungu. Majiundo makini kwa waungamishaji wema ni muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa kwa nyakati hizi. Hii ni changamoto kwa wahudumu na vyombo vya huruma ya Mungu kujikita katika malezi endelevu katika maisha yao, ili huduma hii iweze kuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wao. Ni katika muktadha huu, Idara ya Toba ya Kitume kuanzia tarehe 24 hadi 25 Oktoba 2024 imeandaa semina maalum kwa ajili ya maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho kwa nyakati hizi, mwaliko maalum ni kwa waamini walei. Tema ambazo zimejadiliwa ni pamoja na: Makosa, Dhambi na Msamaha mintarafu Sakramenti za Kanisa na kwamba, baada ya toba na wongofu wa ndani kama ilivyokuwa kwa Baba mwenyehuruma, ni wakati wa kufanya sikukuu. Rej. Lk 15:32.

Sakramenti ya Upatanisho ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu
Sakramenti ya Upatanisho ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu

Haya ni majiundo yanayolenga kuwasaidia waamini walei kujiandaa na hatimaye kuweza kuungama vyema; Umuhimu wa waamini kuungama dhambi zao, ili kuonja neema na baraka za Mungu. Tema nyingine ni “Maungano na Ibada kwa Bikira Maria pamoja na shuhuda mbalimbali za toba na wongofu wa ndani. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 24 Oktoba 2024 amekutana na kuzungumza na Mapadre waungamishaji kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama sehemu ya kumbukizi ya miaka 240 tangu Papa Clement XIV katika Barua yake binafsi “Motu proprio, Miserator Dominus” alipowakabidhi Ndugu Wadogo Wakonventuali, kwa kifupi “OFM Conv.,” huduma ya maungamano kwa watu wa Mungu wanaotembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wanaokadiriwa kuwa ni arobaini elfu kwa kila siku.

Huduma ya Upatanisho: Unyenyekevu, kusikiliza kwa makini pamoja na toba
Huduma ya Upatanisho: Unyenyekevu, kusikiliza kwa makini pamoja na toba

Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia kuhusu Sakramenti ya Upatanisho kama chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu, huduma inayosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu; utamaduni wa kusikiliza kwa makini na huruma. Kuna umati mkubwa wa mahujaji wanaofanya safari kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wanaotafuta fursa ya kukutana na Kristo Yesu katika Sakramenti ya Upatanisho, kumbe, Mapadre hawa wapo kwa ajili ya huduma hii makini, kielelezo cha Kanisa kama Jumuiya ya wokovu, ya watu waliosamehewa dhambi zao na wanapendana kwa nguvu na upendo wa Mungu. Huduma hii inapaswa kutekelezwa katika hali ya unyenyekevu na kwamba, wanapaswa kuwa kweli ni waungamishi wema kwa kutambua kwamba, hata wao ni watu wanaotafuta huruma na msamaha wa Mungu.

Waungamishaji ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu
Waungamishaji ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu

Mapadre waungamishaji wajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini hasa vijana na watoto wadogo kwa kupokea maneno na ushuhuda wao kama zawadi kutoka kwa Mungu, kama sehemu muhimu sana ya toba na wongofu wao wa ndani. Kwa kuwasikiliza wao kwa makini, waungamishaji wanapata fursa pia ya kumsikiliza Kristo Yesu, huduma hii waifanye kwa upendo. Usikivu makini, faraja na msamaha wa dhambi ni muhimu sana kwa Mapadri waungamishaji. Watambue kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu; watu wakarimu, ambao wako tayari kufahamu pamoja na kumwilisha huruma na upendo wa Mungu, dawa kwa ajili ya madonda ya mwanadamu; mambo yanayoonesha ukaribu, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Mapadre waungamishaji kamwe wasiwatweze na kuwadharirisha watu wa Mungu wanaofika kwa ajili ya maungamo. Mapadre waungamishaji wamwombe Kristo Yesu neema na baraka ya kuweza kuwasamehe wote. Huduma ya kuungamisha inahitaji uvumilivu na uaminifu kwani huduma hii ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa. Kwa hakika Mungu ni upendo.

Sakramenti ya upatanisho
25 October 2024, 14:55