Tafuta

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Septemba anawakumbuka na kuwaenzi Watakatifu Malaika wakuu: Mikaeli, Gabrieli na Rafaeli ambao wametajwa kwa namna ya pekee kabisa katika Maandiko Matakatifu. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Septemba anawakumbuka na kuwaenzi Watakatifu Malaika wakuu: Mikaeli, Gabrieli na Rafaeli ambao wametajwa kwa namna ya pekee kabisa katika Maandiko Matakatifu.  (ANSA)

Sikukuu ya Malaika Wakuu: Mikaeli, Gabrieli na Rafaeli: Maisha ya Kikristo ni Mapambano

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, amewakumbusha waamini kwamba, maisha ya Kikristo ni mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi; Walinzi wa Papa wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa wema na huruma ya Mungu; amezishukuru familia zao kwa moyo wa uvumilivu kwa ndugu zao wanapokuwa katika huduma. Baba Mtakatifu anasema, maisha ya kila mwamini ni mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi na kwamba, mamlaka haya wamekabidhiwa Malaika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Septemba anawakumbuka na kuwaenzi Watakatifu Malaika wakuu: Mikaeli, Gabrieli na Rafaeli ambao wametajwa kwa namna ya pekee kabisa katika Maandiko Matakatifu na kila mmoja akitajwa kwa kazi maalum anayoifanya mbele ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anamwomba Malaika mkuu Mikaeli awasaidie waamini katika mapambano ya kazi ya ukombozi. Malaika Mkuu Gabrieli, awaletee watu wa Mungu Habari Njema ya Wokovu, Kristo Yesu, aliyemkomboa mwanadamu, awakirimie matumaini. Malaika Mkuu Rafaeli, awashike mkono na kuwasindikiza katika safari yao ya uponyaji! Mikaeli maana yake “Ni nani aliye sawa na Mungu? Huyu ni Malaika mkuu aliyepambana fika na Ibilisi, Shetani na kushinda, kiasi kwamba, yule nyoka mkubwa, aitwaye Shetani, Ibilisi audanganyaye ulimwengu wote, akatupwa hata katika nchi kama tunavyosoma kwenye Maandiko Matakatifu. Rej. Uf. 12:7.

Baba Mtakatifu amezipongeza familia za walinzi wa Vatican kwa uvumilivu
Baba Mtakatifu amezipongeza familia za walinzi wa Vatican kwa uvumilivu

Malaika mkuu Rafaeli ni mlinzi wa watu wa Mungu kwa sababu yeye ni Jemedari mkuu. Rej. Dan. 12: 1. Gabrieli maana yake ni nguvu ya Mungu. Huyu ni kati ya Malaika wakuu saba wanaokaa siku zote mbele ya Mwenyezi Mungu kama alivyosema Malaika Gabrieli alipokuwa anajibizana na Zakaria kwa kumkumbusha kwamba, yeye alikuwa ni Gabrieli anayesimama mbele ya Mungu na ametumwa kumpasha Habari Njema ya kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji. Malaika mkuu Gabrieli ndiye aliyetumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti kwa Bikira Maria, ili kumpasha Habari Njema kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu. Kwa maneno machache, Malaika wakuu ndio wanaowafunulia watu siri za Mwenyezi Mungu. Rej. Lk. 1-19; Lk. 1:26-28. Rafaeli maana yake ni dawa ya Mungu inayoponya. Rafaeli ni kati ya Malaika watakatifu saba wanaopeleka sala za watakatifu, na kuingia mbele za utukufu wake aliye Mtakatifu. Mwenyezi Mungu ndiye anayepaswa kupewa heshima, utukufu na sifa. Re. Tob. 12:15 na Ufu. 8:2. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema katika liturujia ya hapa duniani, waamini wanashiriki, wakionja liturujia ya mbinguni, iadhimishwayo katika Mji Mtakatifu Yerusalemu, wanaouelekea kama wasafari, ambako Kristo Yesu ameketi mkono wa kuume wa Mwenyezi Mungu kama mhudumu wa patakatifu na wa ile hema ya kweli. Waamini wanaungana na wapiganaji wa jeshi la mbinguni kumwimbia Mwenyezi Mungu wimbo wa utukufu. Wakiwakumbuka kwa heshima watakatifu, wanatumaini kupata ushirika nao, wanangojea kwa shauku Mkombozi, Kristo Yesu, mpaka atakapojidhihirisha, Yeye ambaye ni uzima wao, ndipo nao watakapodhihirishwa pamoja naye katika utukufu. Rej. SC. 8.

Sikukuu ya Malaika Wakuu 29 Septemba ya Kila Mwaka
Sikukuu ya Malaika Wakuu 29 Septemba ya Kila Mwaka

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 5 Oktoba 2024 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Vatican maarufu kama “Swiss Guards.” Itakumbukwa kwamba, Mikaeli maana yake “Ni nani aliye sawa na Mungu? Na ndiye Mlinzi na Mwombezi wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, amewakumbusha waamini kwamba, maisha ya Kikristo ni mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi; Walinzi wa Papa wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa wema na huruma ya Mungu; amezishukuru familia zao kwa moyo wa uvumilivu kwa ndugu zao wanapokuwa katika huduma. Baba Mtakatifu anasema, maisha ya kila mwamini ni mapambano dhidi ya Shetani, Ibilisi na kwamba, mamlaka haya wamekabidhiwa Malaika. Kumbe, kwa msaada wa Malaika waamini wajizatiti katika mapambano dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo na kwamba, katika mapambano haya, waamini wanaungwa mkono na Malaika wakuu ambao wana dhamana na kazi ya kuwalinda watu wa Mungu huku Bondeni kwenye machozi.

Malaika Mkuu Mikaeli ni Mlinzi na Mwombezi wa Vikosi vya Vatican
Malaika Mkuu Mikaeli ni Mlinzi na Mwombezi wa Vikosi vya Vatican

Baba Mtakatifu amewakumbusha walinzi hawa kwamba, kazi yao inaakisi wema na huruma ya Mungu kwa waja wake. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii pia, kuzishukuru na kuzipongeza familia zote za walinzi wa Vatican kwa moyo wao wa uvumilivu, sadaka na majitoleo pale wanapokesekana nyumbani kwa sababu ya majukumu yao ya ulinzi na usalama na hivyo kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa amani na ya Mtakatifu Mikaeli, ili aendelee kuwaunganisha katika kifungo cha umoja na upendo. Waamini wajitahidi kutafuta na kudumisha umoja na upendo. Mwenyezi Mungu awakirimie hekima, uvumilivu na ucheshi.

Malaika Wakuu 2024
06 October 2024, 15:46