Tunu Msingi za Ndoa na Familia: Talaka, Zaidi Upendo na Msamaha wa Kweli
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Wanandoa kwa kumfuasa Kristo Yesu, kwa kujikana wao wenyewe na kwa kuchukua kila mmoja Msalaba wake, watu wa Ndoa Takatifu wanaweza kupokea maana halisi ya ndoa na kuiishi kwa msaada Kristo Yesu. Neema hii ya ndoa ya Kikristo ni tunda la Msalaba wa Kristo Yesu, chemchemi ya maisha yote ya Kikristo! Ndiyo maana Mtakatifu Paulo, Mtume anakazia sana upendo kati ya wanandoa, kielelezo makini cha upendo wa Kristo Yesu kwa Kanisa lake! Rej. KKK 1613-1617. Baba Mtakatifu Francisko anasema hakuna familia ambayo hudondoka kutoka mbinguni ikiwa imeundwa kikamilifu; familia zina haja ya kukua na kupevuka katika uwezo wa kupenda. Huu ni wito endelevu na fungamani katika maisha ya wanandoa unaochota amana na utajiri wake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa linahamasika kuwatafuta na kuwasaidia wale ambao wanaogelea katika shida na mahangaiko mbalimbali ya maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu anawahimiza watu wa Mungu kufunga safari na kutembea huku wakiwa wameshikamana katika upendo bila ya kukata wala kukatishwa tamaa kwa sababu ya mapungufu yao ya kibinadamu. Kamwe wasiache kutafuta utimilifu wa upendo na ushirika wanaooneshwa na kufunuliwa na Mwenyezi Mungu. Rej. AL 325. Ndani ya familia kuna matatizo na changamoto zake, lakini waamini wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia! Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, katika maisha ya ndoa, kuna matatizo, raha na karaha zake! Huko kuna “patashika nguo kuchanika” lakini yote haya ni mambo mpito, jambo la msingi ni kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, kwani Ndoa ni Sakramenti ya Kanisa kwa ajili pamoja na Kanisa na kwamba, upendo wa dhati kabisa unawezekana hata katika ulimwengu mamboleo.
Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanadumu katika nia njema, upendo wa dhati na uaminifu endelevu na dumifu katika: taabu na raha; katika magonjwa na afya; wapendane na kuheshimiana siku zote za maisha yao! Huu ndio uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni ushuhuda wa Injili ya familia unaotangazwa katika ukimya. Ni katika muktadha wa maisha ya ndoa na familia, Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 27 ya Mwaka B wa Kanisa inarejea tena katika msingi wa upendo katika maisha ya ndoa na familia. Mk 10:2-16. Ndoa na Talaka. Mafarisayo wanamuuliza Yesu swali, huku wakitaka kumjaribu kuhusu ndoa na talaka kadiri ya Sheria ya Musa. Kristo Yesu anatumia fursa hii kukazia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zinazofumbatwa katika upendo kati ya Bwana na Bibi kadiri ya mpango wa Mungu. Katika Agano la Kale, kadiri ya Mfumo dume, mwanaume alikuwa na nguvu ya kuandika hati ya talaka na kumwacha mke wake. Ndiyo maana Kristo Yesu anakazia kwa namna ya pekee kabisa fadhila ya upendo na kwamba, mwanaume na mwanamke wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wanapoungana pamoja kwa kifungo cha upendo, wanapania kuanza ujenzi wa maisha mapya. Rej. Mk 10:7, Mwa 2:24. Na wala si mtu kufanya kadiri anavyofikiri kwa kichwa chake, kwani uhusiano huu unapania kuwa ni wa kudumu, hadi pale kifo kitakapowatenganisha. Rej. Mk 10:8; Mwa 2:24. Maisha haya mapya yanahitaji uaminifu na udumifu; ukweli na uwazi; tayari kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano; tayari kutubu, kuongoka, kusamehe na kupatana.
Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 6 Oktoba 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawakumbusha wanandoa kwamba, kukosa na kukoseana ni sehemu ya ubinadamu; kusamehe na kupatana ni mwanzo wa utakatifu wa maisha. Kumbe, wanandoa wajitahidi kupatana kabla ya kuingia kitandani kulala. Watambue kwamba, wanapaswa kuwapokea na kuwalea watoto wao kama zawadi kubwa kutoka kwa Mungu na kwamba, watoto ni matunda ya upendo wao wa dhati, baraka na chemchemi ya furaha ya maisha na matumaini kwa nyumba yao na jamii katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, fadhila ya upendo inamahitaji yake na kwamba, watu wa ndoa wanapozama katika pendo, wanaweza kugundua ile furaha. Jambo la msingi kwa waamini kujiuliza, ikiwa kama upendo wao unasimikwa katika uaminifu na ukarimu? Je, hali ya familia zao ikoje? Je, familia ziko wazi kwa ajili ya kupokea na kuwalea watoto kadiri ya mpango wa Mungu? Je, jumuiya zao zinaenzi tunu msingi za kifamilia, hasa familia changa na zile zinazoundwa na vijana wa kizazi kipya? Bikira Maria awasaidie na kuwaombea wanandoa wapya. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kujiunga kiroho na waamini waliokuwa wamekusanyika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei, kwa ajili ya kusali Rozari Takatifu, Muhtasari wa historia nzima ya ukombozi.