Tafuta

Baba Mtakatifu anawataka wanamichezo kukuza na kudumisha ndani mwao kanuni maadili na tunu msingi za michezo zinazofumbatwa katika: Udumifu, Uvumilivu, Uaminifu, Urafiki pamoja na Mshikamano. Baba Mtakatifu anawataka wanamichezo kukuza na kudumisha ndani mwao kanuni maadili na tunu msingi za michezo zinazofumbatwa katika: Udumifu, Uvumilivu, Uaminifu, Urafiki pamoja na Mshikamano.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tunu Msingi za Michezo: Nidhamu, Udumifu, Uvumilivu, Uaminifu, Urafiki na Udugu

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wanamichezo kukuza na kudumisha ndani mwao kanuni maadili na tunu msingi za michezo zinazofumbatwa katika: Udumifu, Uvumilivu, Uaminifu, Urafiki pamoja na Mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kwa jinsi hii, wanamichezo wanachangia katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, katikati ya maajabu ya asili nchini mwao; wimbo wa sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika Waraka wake wa “Dare il meglio di se” yaani “Kujitoa Kikamilifu”: Mtazamo wa Kikristo Kuhusu Michezo na Binadamu” linakazia umuhimu wa michezo katika maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, michezo ni mahali pa kuwakutanisha watu katika medani mbalimbali za maisha ili kufikia lengo linalotarajiwa. Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu na kijamii. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu na furaha kwa kuhakikisha kwamba, kila mtu anajitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaobomolea mbali kuta za tabia ya ubinafsi, uchoyo na ubaguzi na kuwakirimia watu wa Mungu ile furaha ya moyoni! Baba Mtakatifu anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Mashindano ya kuteleza kwenye theluji 2025
Mashindano ya kuteleza kwenye theluji 2025

Michezo katika nafasi mbalimbali ni jukwaa la kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa walimwengu. Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha! Ujasiri, Sadaka na Udumifu ni mambo msingi katika michezo. Mama Kanisa amekuwa akiwahimiza wanamichezo kujenga na kudumisha: umoja, upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Michezo ni shule ya maisha ya mwanadamu; mahali pa kujifunza Heri za Mlimani daima waamini wakijibidiisha kutafuta taji ya utukufu wa mbinguni.

Tunu za michezo: Nidhamu! Udumifu, Uvumilivu, Uaminifu na Udugu
Tunu za michezo: Nidhamu! Udumifu, Uvumilivu, Uaminifu na Udugu

Mababa wa Kanisa wamekuwa wakiwahimiza wanamichezo kushindana kwa kuzingatia: ukweli, haki, amani na utulivu wa ndani, kwani michezo ni furaha, ili kuwawezesha wanamichezo kuwa na afya njema. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema michezo ni shule ya kanuni maadili, utu wema na maisha ya kijamii. Hapa ni mahali pa kujifunza ukweli, usawa, sadaka, ujasiri, majitoleo ya mtu binafsi na timu katika ujumla wake. Shirikisho la Skii la Austria kwa Lugha ya Kijerumani “Österreichischer Skiverband, ÖSV” lilianzishwa kunako mwaka 1905, lakini kutoka Mwaka 2023 “Ski Austria” limekuwa ni Shirikisho la Michezo linalopania kukuza na kuendeleza michezo ya kuteleza kwenye theluji sanjari na kuratibu shughuli za ushindani nchini Austria, nchi iliyo na utamaduni mzuri wa kuteleza kwenye milima ya Alpine, katika mchezo wa kuteleza kwenye theluji huko Kaskazini.

Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu
Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu

Ni katika muktadha wa kukuza na kudumisha michezo, Wajumbe wa Shirikisho la Skii la Austria: “Österreichischer Skiverband, ÖSV” Alhamisi tarehe 10 Oktoba 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Mashindano ya Dunia yatakayofanyika mwaka 2025. Katika hotuba yake ameelezea kwa kina na mapana kuhusu uzuri wa nchi ya Austria iliyosheheni milima yenye theluji inayowawesha watu wa Mungu nchini humo kufanya michezo ya kuteleza kwenye theluji. Shirikisho hili lililonzishwa kunako mwaka 1905 limekuwa likijitahidi kuendeleza michezo ya kuteleza kwenye theluji. Hili ni Shirikisho ambalo limezalisha wanamichezo bora nchini Austria na kwa kweli wanamichezo hawa wamejisadaka kisawaswa! Baba Mtakatifu anawataka wanamichezo kukuza na kudumisha ndani mwao kanuni maadili na tunu msingi za michezo zinazofumbatwa katika: Udumifu, Uvumilivu, Uaminifu, Urafiki pamoja na Mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kwa jinsi hii, wanamichezo wanachangia katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, katikati ya maajabu ya asili nchini mwao; wimbo wa sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaombea ili Malaika walinzi wawalinde na kuwaepusha kila hatari, na mwishoni akawabariki wote, kutoka katika undani wa moyo wake!

Tunu za Michezo
10 October 2024, 14:42