Umoja wa Wakristo Ni Safari ya Kisinodi na Majadiliano ya Kiekumene: Ushuhuda!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, utengano kati ya Wakristo hupingana wazi na mapenzi ya Kristo Yesu na ni kikwazo kwa ulimwengu na hudhuru tendo takatifu la kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mtakatifu Yohane Paulo II alitaka kuona kwamba, Kanisa Katoliki linaendeleza majadiliano ya kiekumene na Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali, ili siku moja wote wawe wamoja chini ya Kristo Yesu, Mchungaji mkuu. Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma. Anasema uekumene wa damu na ule wa utakatifu wa maisha ni mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo sehemu mbalimbali za dunia katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, uekumene wa damu unajikita katika: Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni chachu ya Ukristo. Uekumene wa maisha ya kiroho na utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu wa kibinadamu kati yao. Uekumene wa huduma unatekelezwa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume.
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Maadhimisho ya Awamu ya Pili ni kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 27 Oktoba 2024. Lengo kuu la Maadhimisho haya ni kwa ajili ya Mama Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Ni kusikiliza Neno la Mungu, ili kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha ya waamini. Kusikiliza ni kujenga utamaduni wa kusali pamoja na Neno la Mungu, “Lectio Divina.” Ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, kwa kuangalia matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza, ili hatimaye, kuhamasisha umoja na ushiriki wa watu wa Mungu kutoka katika ngazi mbalimbali za maisha, kama ilivyokuwa kwa Wafuasi wa Emau. Kumbe, Majadiliano ya kiekumene na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ni sawa na chanda na pete, kwani yanahitajiana na kukamilishana.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni, tarehe 11 Oktoba 2024 ameshiriki pamoja na Mababa wa Sinodi Masifu ya jioni. Katika mahubiri yake, amekazia kwamba, umoja wa Wakristo ni safari inayofumbata ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; Umoja ni safari, neema, utulivu na ushuhuda kwa ajili uinjilishaji unaopata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo, kumbe, Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Ibada ya Masifu ya Jioni, imeadhimishwa pembeni mwa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, lililojengwa kwenye masalia ya mashuhuda wa kwanza wa Injili, wanaoendelea kulienzi Kanisa kwa sala na maombi yao. Kanisa linaadhimisha kumbukizi ya Miaka 60 tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha hati ya “Unitatis redintegratio” Yaani “Kuhamasisha Urejeshaji wa Umoja wa Wakristo. Kwa maana waamini kwa kadiri wanavyokua katika ushirika na Fumbo la Utatu Mtakatifu, ndivyo watakavyoweza kukuza udugu kati yao kwa undani na kwa urahisi zaidi. Rej. UR 7.
Hii ni changamoto kwa Wakristo kumwilisha ndani mwao Sala ya Kristo Yesu, wakati wa Karamu ya Mwisho. Mkazo unaendelea kuwekwa kwenye mambo yanayowaunganisha Wakristo, kuliko yale yanayowagawa na kuwasambaratisha. Uekumene wa maisha ya kiroho na sala, umeendelezwa zaidi, kwa Wakristo kujizatiti zaidi katika ile Sala ya Yesu, ili wote wawe wamoja. Hii ni Sala ya Kikuhani inayoendelea kuwachangamotisha Wakristo kutekeleza mapenzi ya Yesu kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano. Kumbe, maadhimisho ya Sinodi imekuwa ni fursa ya kugundua tena zawadi ya umoja wa Wakristo. Umoja ni neema na zawadi kubwa kutoka juu mbinguni, changamoto kwa Wakristo ni kutoweka vizingiti katika mpango wa Mungu na utashi wa Kristo Yesu. Umoja ni safari inayojikita katika ushirikiano wa Wakristo katika nyanya mbalimbali za: huduma, majadiliano na mshikamano katika maisha, hatua kwa hatua kama ilivyokuwa kwa wale wanafunzi wa Emau walioambatana na Kristo Yesu Mfufuka njiani.
Umoja unafumbatwa katika utulivu na wala si katika usawa na kwamba, majadiliano ya kiekumene yanapaswa kujikita katika fadhila ya upendo kwa Kristo na huduma makini kwa watu wa Mungu. Shida na changamoto zitaendelea kuwepo, lakini Wakristo wanapaswa kujiaminisha kwa maongozi ya Roho Mtakatifu, mhimili mkuu wa ujenzi wa umoja wa Wakristo katika tofauti zao msingi. Kama ilivyo katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ndivyo ilivyo hata katika ujenzi wa umoja wa Wakristo unaokita mizizi yake katika ushuhuda, ili ulimwengu upate kusadiki. Rej Yn 17:21. Utengano miongoni mwa Wakristo hupingana wazi na mapenzi ya Kristo Yesu, nao ni kikwazo kwa ulimwengu na hudhuru tendo takatifu na kuhubiri na kushuhudia Injili kwa kila kiumbe. Rej. UR 1. Hii ni changamoto inayosimikwa katika ushuhuda wa pamoja. Huu ni ushuhuda wa damu unaopata chimbuko lake kutoka pale juu ya Msalaba wa Kristo Yesu. Maadhimisho ya Sinodi yalifunguliwa kwa Ibada ya toba na wongofu wa ndani. Hii imekuwa pia siku ya kuomba toba kwa Mwenyezi Mungu kutokana na utengano miongoni mwa Wakristo, changamoto na mwaliko kwa Wakristo kujikita katika msingi wa mambo yale yanayowaunganisha ili kutekeleza dhamana na wajibu wa utume wao unaopata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Hii ni changamoto ya kulijenga tena upya Kanisa la Kristo, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Msalaba wa Kristo Yesu uwaongoze hadi kufikia umoja kamili, katika amani na utulivu. “Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.” Kol 1:19-20.