Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia Waraka Wakatoliki pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaoishi huko Mashariki ya kati kutokana na vita inayoendelea kati ya Israeli na Palestina Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia Waraka Wakatoliki pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaoishi huko Mashariki ya kati kutokana na vita inayoendelea kati ya Israeli na Palestina  (AFP or licensors)

Waraka wa Papa Francisko Kwa Watu wa Mungu Mashariki ya Kati

Damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika, kama machozi yanavyoendelea kutiririka bila kukoma! Jambo la msingi, ambacho ndicho kilio cha watu wengi ni kwa wahusika wakuu kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi; amani na maridhiano. Ikumbukwe kwamba, vita ni kielelezo cha binadamu kushindwa, silaha kamwe haziwezi kujenga na badala yake zinaendelea kuleta maafa na kwamba, kamwe vita haiwezi kuleta amani na utulivu kati ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu tarehe 7 Oktoba 2024 amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema: Kutubu na kumwongokea Mungu, kusali na kufunga na kwamba, siku hii inogeshwe kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, Mama Kanisa anapoadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu. Hii pia ni siku muhimu sana, kwa Jumuiya ya Kimataifa inapofanya kumbukizi ya mwaka mmoja tangu vita kati ya Israeli na Palestina ilipotimua vumbi, yaani tarehe 7 Oktoba 2023. Watu wengi wamepoteza maisha, wamejeruhiwa, wametekwa, kufungwa na wengine wengi wamewekwa kizuizini. Watu wanaendelea kuteseka kwa kukosekana kwa mahitaji msingi kama vile chakula, maji na makazi salama, kiasi cha kupelekea wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum huko Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu anawataka wahusika wa pande zote mbili kuhakikisha kwamba, wanawaachia huru bila masharti wafungwa na mateka wa vita. Ni wakati wa kusitisha vita kwa sababu waathirika wakuu ni raia wasiokuwa na hatia na ambao wanalazimika kuyakimbia makazi yao. Uhuru na usalama wa nchi husika lazima vipewe kipaumbele na wala kusiwepo mashambulizi dhidi ya taifa jingine au kuvamiwa. Kumbe, huu ni mwaliko wa kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli; haki na amani ili hatimaye kuachana na chuki pamoja na vita.

Papa: Waamini wasichoke kusali kwa ajili ya kuombea amani
Papa: Waamini wasichoke kusali kwa ajili ya kuombea amani

Ni katika muktadha wa kumbuziki ya Mwaka mmoja, tangu tarehe 7 Oktoba 2023 vita ilipozuka wakati wanamgambo wa Hamas waliposhambulia maeneo ya Israel huko Gaza, na kuua takribani Waisraeli 1,200 na kuwateka nyara wengine 240. Israel ilijibu mapigo katika kampeni inayoendelea hadi leo, ikigharimu maisha ya Wapalestina wapatao 40,000 na kujeruhi maelfu ya watu!Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia Waraka Wakatoliki pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaoishi huko Mashariki ya kati, ili kuwaonesha kwamba, bado yuko pamoja nao katika kipindi hiki cha mateso na mahangaiko makubwa kutokana na vita inayoendelea kati ya Palestina na Israeli. Hii ni aibu kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa na hasa kwa Mataifa makubwa kushindwa kusitisha vita hii. Damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika, kama machozi yanavyoendelea kutiririka bila kukoma! Watu wanatamani kulipiza kisasi, lakini jambo la msingi, ambalo ndicho kilio cha watu wengi ni kwa wahusika wakuu kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi; amani na maridhiano. Ikumbukwe kwamba, vita ni kielelezo cha binadamu kushindwa, silaha za vita kamwe haziwezi kujenga na badala yake zinaendelea kuwa ni chanzo cha maangamizi na kwamba, kamwe vita haiwezi kuleta amani na utulivu!

Vita ina madhara makubwa kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu
Vita ina madhara makubwa kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu

Huu ndio ukweli wa kihistoria na kwamba, katika miaka yote hii, bado binadamu hajaweza kujifunza kutokana na historia ya vita! Watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati wanaishi katika maeneo ya Biblia, lakini wanayo kiu ya amani ya kudumu. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa kuendelea kuishi katika Nchi Takatifu, kwa kuendelea kusali na kuipenda nchi yao. Watambue kwamba, wao ni mbegu pendeka kutoka kwa Mungu, itakayokuwa na hatimaye kukomaa katika matumaini na kwamba, katika mwanga wa imani, wataweza kushuhudia upendo na umoja, licha ya chuki na tabia ya kutaka kuwagawa. Baba Mtakatifu anawakumbusha kwamba, wao ni wateule wa Mungu na mashuhuda wa imani, watu wanao mwamini Kristo Yesu ambaye ni “mpole na mnyenyekevu wa moyo.” Mt 11:9.

Adui mkubwa wa binadamu ni silaha za kivita
Adui mkubwa wa binadamu ni silaha za kivita

Kristo Yesu ni chimbuko la amani ya kweli isiyobebwa na silaha za vita. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kamwe wasichoke kusali kwa ajili ya kuombea amani na kwamba, toba, sala na kufunga ni silaha za upendo zinazoweza kubadili ulimwengu! Silaha za kivita ndiye adui mkubwa wa binadamu kama alivyo Shetani, Ibilisi tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kujikita katika: toba, sala na kufunga, ili vita iweze kukoma kwenye uso wa dunia. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza na kwamba, kila siku anawakumbuka katika sala. Hawa ni watu ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao, kuacha masomo na kazi ili kukimbia mashambuzili ya kivita. Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea wanawake wanaowalilia na kuwaombolezea watoto wao, wanaopoteza maisha kutokana na vita; watoto wanaojeruhiwa, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria chini ya Msalaba. Anawakumbuka watoto ambao hawana tena fursa ya kucheza na kufurahia maisha ya utoto wao kwa sababu ya vita.

Waraka wa Papa Francisko kwa Watu wa Mashariki ya Mbali: Mshikamano!
Waraka wa Papa Francisko kwa Watu wa Mashariki ya Mbali: Mshikamano!

Baba Mtakatifu yuko pamoja na wale ambao hawana tena sauti, kwani kuna mipango mizuri inayopangwa na wakuu wa Mataifa, lakini utekelezaji wake ni “kiduchu” na badala yake vita inaendelea kusonga mbele. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha mshikamano wake na wale wote wenye kiu ya haki na amani, wasiokatishwa tamaa na “mtutu wa bunduki.” Baba Mtakatifu anawashukuru watoto wa amani na faraja; wanaoendelea kuwahudumia wagonjwa, wenye njaa na kiu ya haki; wale waliotelekezwa na kuteseka kwa umaskini; anawataka waendelee kuwahudumia na kuwafariji ndugu zao katika Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Makleri na watawa wawe ni vyombo na mashuhuda wa usalama, tayari kutangaza upendo unaovunjilia mbali uchu wa madaraka. Mwishoni mwa waraka wake kwa watu wa Mungu wanaoishi katika Nchi Takatifu, anapenda kuwapatia baraka zake za kitume na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Malkia wa amani; Mtakatifu Francisko awalinde na kuwatunza. Amina.

Waraka Kwa Watu wa Mungu
08 October 2024, 13:52