Tafuta

Papa Francisko kila siku anasali kwa ajili ya Ukraine Papa Francisko kila siku anasali kwa ajili ya Ukraine 

Papa amwandikia Balozi wa Vatican,Ukraine:Ni Mungu pekee chanzo cha uhai,tumaini na hekima!

Papa ametuma barua kwa Askofu Mkuu Kulbokas katika fursa ya siku 1000 tangu kuzuka kwa mzozo katika nchi ya Mashariki mwa Ulaya,akimshukuru kubaki karibu na idadi ya watu katika kipindi kirefu cha mateso.Papa anamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuibadili mioyo na kuwafanya wawe na uwezo wa kuanzisha njia za mazungumzo,upatanisho,maelewano na anatumaini.Neno Amani,linasikika katika familia,nyumba na viwanja.Mungu,atasikiliza machozi yaliyomwagika.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Siku ya Jumanne tarehe 19 Novemba 2024  ni kumbukizi ya siku 1,000 tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake kamili wa Ukraine mnamo tarehe 24 Februari 2022. Katika fursa ya kukumbuka siku hiyo ya huzuni, Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena alionesha mshikamano wake na watu wa Ukraine wanaoteseka kupitia ujumbe wake. Katika barua iliyotumwa kwa Balozi wa Vatican  nchini Ukraine, Askofu Mkuu Visvaldas Kulbokas, Papa amebainisha kiwango cha mateso wanachovumilia Watu wa Ukraine. "Ninafahamu vyema kwamba hakuna maneno ya kibinadamu yanayoweza kulinda maisha yao dhidi ya milipuko ya kila siku, kuwafariji wale wanaoomboleza wafu wao, kuponya waliojeruhiwa, kuwarudisha watoto nyumbani, wafungwa huru, au kurejesha haki na amani. Neno "amani" ndilo Baba Mtakatifu  anasali ili “siku moja litasikika tena katika nyumba, familia na mitaa ya Ukraine.”

Katika barua yake kwa mwakilishi wake nchini, Papa Francisko alikumbusha "dakika ya ukimya ya kitaifa"ya kila siku inayozingatiwa na Waukraine kila asubuhi ifikapo saa 3.00 kwa kuwaenzi waathirika wote wa vita kwamba “watoto na watu wazima, raia na askari, pamoja na wafungwa wanashikiliwa katika mazingira ya kutisha. Akiwa na watu hawa akilini,  mwake, Baba Mtakatifu aliomba  kwa kutumia maneno ya Zaburi 121, akiandika kwamba: "Msaada wangu u katika Bwana, aliyezifanya mbingu na nchi." Kwa hiyo umoja huu katika maombi, alisisitiza Papa, ni ukumbusho wenye nguvu kwamba msaada wa Mungu unafika hata katika nyakati za giza. Mungu  aifariji mioyo yetu na aimarishe tumaini kwamba, wakati akikusanya kila mchozi na kuwawajibisha wote, anabaki karibu nasi hata wakati juhudi za kibinadamu zinaonekana kutozaa matunda na vitendo havitoshi.”

Katika kipindi chote cha Upapa, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa mtetezi asiyechoka wa amani duniani kote, na mara kwa mara amekuwa akitoa wito wa maombi ya amani katika kile anachokieleza kuwa "Ukraine iliyouawa." Katika barua yake kwa Askofu Mkuu Kulbokas, Papa amepyaisha sala hii na kuomba mioyo igeuzwe ili kukuza mazungumzo na maelewano. Alisisitiza kwamba maneno anayozungumza na Balozi pamoja naye, watu wa Ukraine, si maneno ya mshikamano tu bali ni ombi la dhati la kuingilia kati kwa Mungu. Alieleza kwamba Mungu pekee ndiye chanzo pekee cha uhai, tumaini, na hekima. Baba Mtakatifu Francisko akihitimisha waraka wake huo ametoa baraka zake kwa Maaskofu na mapadre wanaoendelea kuwa imara katika utume wao wa kuwasindikiza na kuwaunga mkono waamini wa Ukraine. Hatimaye, Papa alisisitiza baraka zake kwa watu wote wa Ukraine, akionesha imani kwamba “Mungu atakuwa na neno la mwisho juu ya janga hili kubwa. Ninawabariki watu wote wa Ukraine.”

Papa ametuma ujumbe kwa Balozi wa Vatican nchini Ukraine
19 November 2024, 18:02