Papa anaongeza Askofu mkuu wa Napoli Don Mimmo kwa makardinali wapya
Salvatore Cernuzio – Vatican.
Makadinali 21 wapya sasa watapokea kofia nyekundu kwenye Consistory ijayo tarehe 7 Desemba. Baba Mtakatifu Francisko ameongeza jina jipya katika orodha ya Makardinali wajao, lile la Askofu Mkuu Domenico Battaglia wa Napoli ambaye ameongoza Jimbo Kuu tangu Desemba 2020. Tangazo hilo lilikuja Jumatatu alasiri tarehe 4 Novemba 2024 kutoka kwa Msemaji mkuu wa vyombo vya habari katika Ofisi ya Waandishi wa Habari ya Vatican, Dk, Matteo Bruni kwamba: “Papa Francisko ametangaza kuwa amejumuisha kati ya majina ya makardinali wapya ambao wataundwa wakati wa Baraza la makardinali (Consistory) tarehe 7 Desemba 2024 Askofu Mkuu Domenico Battaglia, wa Jimbo Kuu latoliki la Napoli.”
Kama ilivyotangazwa mwishoni mwa Sala ya Malaika wa Bwana tarehe 6 Oktoba 2024, idadi ya makardinali wapya ilipungua mmoja kufuatia na ombi la kutoundwa kuwa kardinali kwa Askofu Mkuu Paskalis Bruno Syukur wa Bogor, nchini Indonesia, tarehe 22 Oktoba 2024 ambaye alionesha nia ya kuendelea na maisha yake binafsi katika ukuaji zaidi kwenye huduma kwa Kanisa na watu wa Mungu unaotokana na hamu ya kuimarisha zaidi maisha yake ya kipadre.”
Kuwasaidia wenye uhitaji
'Don Mimmo', kama Askofu Mkuu anavyojulikana sana hivyo na bado anaitwa hivyo, ana jukumu maarufu la kichungaji kusini mwa Italia, akiwa na historia kama 'kuhani wa mitaani' aliyejitolea hasa kwa vijana na wale wanaopambana na madawa ya kulevya. Papa pia alimwita kuwa miongoni mwa wajumbe wa vikao viwili vya Sinodi ya kisinodi iliyomalizika hivi karibuni. Mzaliwa wa eneo la kusini mwa Italia huko Calabria, asili yake ni Satriano, ya Catanzaro, mwenye umri wa miaka 61. Kabla ya kuteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Napoli, aliwahi kuwa Askofu wa Jimbo la Cerreto Sannita-Telese-Mtakatifu Agata de' Goti, katika jimbo la Benevento. Alimaliza masomo yake ya falsafa na taalimungu katika Seminari ya Kipapa ya Kikanda “Mtakatifu Pio X” huko Catanzaro. Alipewa daraja la Upadre tarehe 6 Februari 1988, na amekuwa padre wa parokia, Gambera, mkurugenzi wa ofisi za Jimbo kwa miaka mingi. Tarehe 24 Juni 2016 aliteuliwa na Papa Francis kuwa Askofu wa Cerreto Sannita -Telese- Mtakatifu Agata de' Goti.
Nyadhifa nyingine
Kuwekwa wakfu kwake wa kiaskofu kulifanyika tarehe 3 Septemba na kusimikwa kwake katika uongozi wa jumuiya ya Benevento tarehe 2 Oktoba 2016, akichagua kama kauli mbiu yake ya kiaskofu maneno ya Yesu kwa Bartimayo, mwana kipofu wa Timayo, ambaye alikuwa ameketi kando ya barabara akiomba.” ('Confide, surge, voat te!') yaani “Jipe moyo; inuka, anakuita!” Askofu Mkuu Battaglia amekuwa makini sana katika utunzaji mwema kwa maskini na wale walio pembezoni mwa jamii unaonekana wazi. Aliwasindikiza watu waliokuwa wakihangaika na matumizi ya dawa za kulevya kuanzia 1992 hadi 2016, akiongoza “ Kituo cha mshikamano cha Calabria”kituo kinachohusishwa na Jumuiya za Tiba za Don Mario Picchi (FICT) ambayo alikuwa rais wa kitaifa kuanzia 2006 hadi 2015. Kuanzia mwaka wa 2000 hadi 2006, pia aliwahi kuwa makamu wa rais wa Mfuko wa Betania huko Catanzaro, shirika la Jimbo linalotoa usaidizi na hisani. Huko Napoli, akisifiwa na mapadre na waamini wa mahali hapo, askofu mkuu mpya alijitambulisha katika ujumbe wake wa kwanza ‘kama kaka aendaye kati ya kaka na dada’ katika jiji aliloliita ‘hazina ya Kusini’ yenye matumaini na changamoto, akithibitisha imani yake. kujitolea kama mchungaji anayejali, jambo ambalo ataendelea kufanya kama kardinali.
Baraza la Makardinali
Katika Baraza la Makardinali inayokuja, ya kumi ya Papa Francisko, ni mmoja tu wa makardinali wa siku zijazo ambaye sio mteule (aliyekuwa Balozi Askofu Mkuu Acerbi). Pamoja na nyongeza ya Askofu Mkuu Battaglia, 11 ni Wazungu kati yao 5 ni Waitaliano; 6 wanatoka Amerika wakiwemo Wamarekani kusini 5; 3 ni Waasia; na mmoja ni Mwafrika. Hadi tarehe 7 Desemba, Baraza la Makardinali litakuwa na wajumbe 256 kati yao 141 ni wapiga kura na 115 sio wapiga kura.