Tafuta

Papa awaombea waathirika wa Indonesia na kuombea amani duniani!

Mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana Dominika Novemba 10,Papa Francisko alitoa sala na pole kwa wahanga wa mlipuko wa volkano nchini Indonesia, na wahanga wa mafuriko huko Valencia,Hispania.Alitoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo kuhusu machafuko nchini Msumbiji na kukomesha umwagaji damu nchini Ukraine,Palestina,Israel,Myanmar na Sudan.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza mara baada ya kuhitimisha sala ya Malaika wa Bwana kwa waamini na mahujaji waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Dominika tarehe 10 Novemba 2024 alionesha ukaribu wake na watu wa Kisiwa cha Flores nchini Indonesia walioathirika na mlipuko wa volkano iliyoanza takriban juma moja lililopita na inaendelea huku mamlaka za eneo hilo zikiongeza eneo la dharura na uhamishaji wa watu.

Mwonekano wa waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican 10 Novemba 2024
Mwonekano wa waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican 10 Novemba 2024

Kwa njia hiyo Papa alitoa maombi yake kwa wahanga, waliokimbia makazi na familia zao. Watu kumi wamethibitishwa kufariki na wengine kadhaa kujeruhiwa huku uokoaji wa dharura ukiendelea ili kuwahamisha wakazi mbali na maeneo hatarishi. Mlipuko wa volkano huko Lewotobi Laki-laki Januari iliyopita ulilazimisha kuhamishwa kwa wakazi 6,500 katika mojawapo ya maeneo yenye hatari kubwa ya tetemeko la ardhi nchini.

Kukumbuka Valencia,Hispania

Akikumbuka Valencia na maeneo jirani ya Hispania yaliyokumbwa na mafuriko makubwa katika majuma ya  hivi karibuni, Papa aliomba “kila mtu kuwaombea na kufikiria kutoa msaada kwa njia fulani kuwasaidia katika uokoaji na juhudi za misaada.” Mafuriko makubwa yaliathiri kusini na mashariki mwa Hispania mwishoni mwa Oktoba. Zaidi ya watu 200 wamekufa na huduma za dharura zinaendelea na msako wa kuwatafuta mamia ambao bado hawajapatikana. Maafa hayo ya asili yametajwa kuwa mabaya zaidi kuwahi kutokea nchini Hispania.

Wito kwa mazungumzo nchini Msumbiji

Papa vile vile alielendele kuelekeza  mawazo yake kwa taifa la kusini mashariki mwa Afrika huko Msumbiji ambako majuma kadhaa ya machafuko ya wenyewe kwa wenyewe yanaendelea, kufuatia uchaguzi wa Taifa mwezi uliopita ambao hadi sasa unashindaniwa,  kwa hiyo mashirika ya kutetea haki za kimataifa yanasema makumi ya watu wameuawa. Akielezea wasiwasi wake juu ya habari za kutisha zinazotoka Msumbiji, Baba Mtakatifu Francisko alihimiza “kila mtu kushiriki katika mazungumzo na majadiliano, ili kuokoa, na  katika kutafuta suluhisho la changamoto.” Aliwataka kila mmoja kuliombea “taifa hilo na hali iliyopo isiwafanye kukosa imani na njia ya demokrasia, haki na amani.”

Maombi ya amani katika ulimwengu wetu

Papa Francisko aidha alirudia kutoa wito wake kwa ajili ya amani duniani, akikumbuka hasa mateso ya Ukraine ambapo hospitali na miundo mingine ya kiraia inapigwa.” Alirudia wito wake wa maombi kwa ajili ya “Palestina, Israel, Lebanon, Myanmar, Sudan na amani duniani kote.”

Maadhimisho ya miaka mitatu ya Jukwaa la Laudato Si'

Miaka mitatu imepita tangu kuzinduliwa kwa Jukwaa la Matendo ya Laudato Si' (Laudato Si' Action Platform)ambapo  Papa alikumbuka na aliwashukuru wale wote ambao wameendeleza mpango huu muhimu. Kufanya kazi ya kulinda makazi yetu ya pamoja kwa kulinda mazingira yetu pia ndicho kilele cha hivi karibuni zaidi cha mkutano wa kilele wa kimataifa kitakachochunguza siku hizi huko Baku, Azerbaijan, wakati wa Mkutano wa COP 29 wa Mabadiliko ya Tabianchi, na Papa alionesha “matumaini yake kwamba fursa hii itatoa mchango mzuri kwa ulinzi wa nyumba yetu ya kawaida.”

Papa baada ya Sala ya Malaika 10 Novemba 2024
10 November 2024, 13:43