Papa Francisko:Vijana wa Ureno wakabidhi Ishara za Siku ya WYD kwa vijana wa Korea Kusini
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baada ya Misa, Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 24 Novemba 2024 katika Siku Kuu ya Kristo Mfalme, sanjari na Siku ya 39 ya Vijana Duniani kwa ngazi ya Majimbo yote, na kabla ya kukabidhiana msalaba na ishara za Siku ya Vijana, aliwalekea Ujumbe wa vijana kutoka Ureno aule wa Korea ya Kusini kwamba “Ninapenda kuwasalimu ninyi nyote, vijana mliopo hapa, na vijana kutoka pande zote za dunia, hasa ujumbe kutoka Ureno, ambako Siku ya Vijana Duniani ilifanyika mwaka jana,(2023) na ujumbe kutoka Korea Kusini, ambao utaandaa inayofuata huko Seoul mnamo 2027.”
Papa Francisko alikazia kusema kuwa "Muda mfupi vijana wa Kireno watakabidhi alama za WYD - Msalaba na Picha ya Maria Salus Populi Romani (Maria Afya ya Warumi)- kwa Vijana wa Korea. Alama hizi zilikabidhiwa kwa vijana na Mtakatifu Yohane Paulo II ili kuzipeleka ulimwenguni kote.” Papa aliendelea: “Na ninyi, Wakorea wapendwa, sasa ni zamu yenu! Kwa kubeba Msalaba hadi Asia mtatangaza upendo wa Kristo kwa kila mtu. Kuweni na ujasiri! Muwe na ujasiri wa kutoa ushuhuda kuhusu tumaini tunalohitajika zaidi leo hii kuliko wakati mwingine wowote ule. Mahali, ambapo alama hizi zitapitia, basi uhakika wa upendo usioshindika wa Mungu na udugu kati ya watu ukue. Na kwa waathiriwa wote vijana wa mizozo na vita, Msalaba wa Bwana na picha ya Mtakatifu Maria iwe msaada na faraja.”