Papa Francisko amekula chakula na maskini 1300:kurudisha hadhi ya kila mtu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika Siku ya Maskini duniani inayoongoza na kaulimbiu: “Sala ya maskini huinuka kwa Mungu,” Baba Mtakatifu Francisko ameshiriki chakula cha mchana na watu wapatao 1,300 kutoka karibu jiji zima la Roma wanaohitaji msaada. Ni katika Dominika tarehe 17 Novemba 2024 mara baada ya Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican pia Sala ya Malaika wa Bwana kwa waamini na mahujaji waliounganika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro ambapo Papa Francisko alitoa shukrani zake kwa wale wote kwa majimbo na parokia duniani kote ambao wamefanya mipango ya mshikamano na watu wasio na uwezo zaidi.
Chakula hicho maalum cha mchana kwa wageni 1,300 waliokaribishwa na Papa kilitolewa na Shirika la Msalaba Mwekundu la Italia huku watu wa kujitolea wapatao 340 wakihudumia mlo huo kama ilivyokuwa imetolewa taarifa kutoka Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa Baraza hilo, Kardinali Conrad Krajewski akizungumza na vyombo vya habari Vatican, alikumbusha kuwa matukio ya leo yalitanguliwa hata hivyo na mipango mingi ya kuwahudumia maskini kama vile zahanati iliyo chini ya Nguzo ya Bernini, inayofunguliwa kila siku na ambayo inakaribisha karibu watu 150 wasio na makazi kila siku. Kila mtu anayehitaji, hata watu wasio na hati au ambao hawajui Kiitaliano, wanaweza kutegemea usaidizi kamili wa matibabu.
Katika nafasi ya kwanza, hata hivyo, kuna kusikiliza wengine, historia na mahitaji yao, kwa sababu "kurejesha heshima pia hutokea katika kusikiliza". Watu hawa wenye udhaifu hutembelewa na madaktari na kupokea dawa bure kutoka kwa Baba Mtakatifu katika duka la dawa la Vatican. Mlo huo baada ya Misa Takatifu pamoja na maskini, ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo kutolewa na Shirika la Msalaba Mwekundu la Italia. Mwishoni, kila mmoja alipokea mkoba wenye chakula na mahitaji muhimu kwa maisha ya kila siku kutoka kwa Mapadre wa Shirika la Wamisionari wa Vincent.
Kila mmoja aliyeweza kumfikia Papa alimpatia zawadi au hata kupiga picha(self)kila mmoja kuhisi kuwa na Baba wa Kanisa la Ulimwengu.