Tafuta

2024.11.09 Washiriki wa Mkutano kuhusu Huduma-Elimu na Mkataba wa Elimu Kimataifa. 2024.11.09 Washiriki wa Mkutano kuhusu Huduma-Elimu na Mkataba wa Elimu Kimataifa.  (Vatican Media)

Papa:UNISERVITATE inajibu kwa njia thabiti nia za Mkataba wa Elimu Kimataifa!

Kwa kuwa hatuwezi kubadilisha ulimwengu ikiwa hatubadilishi elimu,tunahitaji kutafakari pamoja jinsi ya kuanzisha na kuongoza mabadiliko haya.Taasisi za elimu Kikatoliki huishi kulingana na jina lao.Kwa shule au chuo kikuu chochote,kuwa‘Mkatoliki’ni zaidi ya kuwa na kivumishi bainifu katika jina lake;inaashiria kujitolea kusitawisha mtindo wa kipekee wa ufundishaji na mafundisho yanayopatana na mafundisho ya Injili.Ni Maneno ya Papa kwa washiriki wa Mkutano:Mafundisho-Huduma na Mkataba wa Elimu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 9 Novemba 2024 amekutana na Washiriki wa Mkutano wa Chuo Kikuu kuhusu Huduma  ya Mafunzo na Mkataba wa Elimu Kimataifa. Katika hotuba yake amesema mkutano wao ni wa kuvutia sana kwa Kanisa, ambalo Mtakatifu Paulo VI alipenda kulielezea kama “mtaalamu wa ubinadamu”’ (Hotuba kwa Shirika la Umoja wa Mataifa, 1). Maneno hayo ni fasaha na yenye kudai; yanatupatia changamoto ya kuwaeleza waziwazi katika kazi yetu kama waelimishaji,” Papa amesema.  Kuhusiana na hili, Papa amefikiria filamu ya 'Dead Poets Society', yaani 'Jamii ya washairi waliokufa' ambayo inasimulia jinsi mwalimu wa fasihi aliyekuwa na mbinu asilia alifika katika shule maarufu ya bweni. Alianza somo lake la kwanza kwa changamoto ndogo: aliwaomba wanafunzi kusimama kwenye madawati yao na kutazama darasa kwa mtazamo mwingine. Kipindi hiki kinapendekeza elimu inavyopaswa kuwa - sio tu uwasilishaji wa yaliyomo, lakini mabadiliko ya maisha. Sio tu marudio ya mitindo, lakini mafunzo ya kuona ugumu wa ulimwengu wetu.

Papa na washiriki wa Mkutano wa Huduma-mafunzo na Mshikamano wa Elimu kimataifa
Papa na washiriki wa Mkutano wa Huduma-mafunzo na Mshikamano wa Elimu kimataifa

Katika ufundishaji wa Yesu mwenyewe, “mtindo” huu ni dhahiri kabisa: tunauona katika mojawapo ya aina zake za kufundisha kwa mifano. Kwa kusimulia historia, Bwana hakuzungumza kwa lugha dhahania ambayo inaweza kueleweka tu na wasomi, lakini kwa njia ambayo ilikuwa rahisi na kueleweka kwa wote. Baba Mtakatifu Francisko amesema kuwa “Fumbo ni historia inayowawezesha wasikilizaji kuingia katika masimulizi, wakijihusisha na kuhusika na wahusika. Yesu alilenga kuhakikisha kwamba wasikilizaji wake hawakuelewa ujumbe huo tu, bali  nao walihusika kibinafsi. Kinyume na mtindo huu, utandawazi wa leo hii unahusisha hatari kwa elimu, yaani mchakato wa kusawazisha katika mwelekeo wa programu fulani ambazo mara nyingi huzingatia maslahi ya kisiasa na kiuchumi. Mwelekeo huu wa usawa unaficha aina za hali ya kiitikadi, ambayo inapotosha kazi ya elimu, na kuifanya chombo cha maslahi tofauti kabisa na kukuza utu wa binadamu na utafutaji wa ukweli.

Papa Francisko alisema kuwa “Kwa kuwa "hatuwezi kubadilisha ulimwengu ikiwa hatubadilishi elimu", tunahitaji kutafakari pamoja jinsi ya kuanzisha na kuongoza mabadiliko haya.” Ili kukabiliana na changamoto hii, inafurahisha kuona jinsi ambavyo UNISERVITATE yaani… imeunda mbinu ya ufundishaji ya “kujifunza-huduma”, kwa kukuza hisia ya uwajibikaji wa jumuiya kwa upande wa wanafunzi kupitia mipango ya kijamii ambayo ni sehemu muhimu ya programu yao ya kitaaluma. Kwa njia hiyo, taasisi za elimu za Kikatoliki huishi kulingana na jina lao. Kwa shule au chuo kikuu chochote, kuwa ‘Mkatoliki’ ni zaidi ya kuwa na kivumishi bainifu katika jina lake; inaashiria kujitolea kusitawisha mtindo wa kipekee wa ufundishaji na mafundisho yanayopatana na mafundisho ya Injili.

Mkutano wa Papa na washiriki wa Mkutano kuhusu Mkataba wa kielimu kimataifa
Mkutano wa Papa na washiriki wa Mkutano kuhusu Mkataba wa kielimu kimataifa

Katika suala hili, UNISERVITATE inajibu kwa njia thabiti kwa nia za Mkataba wa Elimu Kimataifa kwa kukuza michakato ya elimu inayohusisha kila mtu. Methali ya Kiafrika inasema kwamba inahitajika kijiji kizima kumfundisha mtoto. Kwa maana hiyo Papa ameongeza “Basi, tufanye kila juhudi kujenga “kijiji cha elimu,” ambapo tunaweza kufanya kazi pamoja ili kukuza mahusiano chanya na yenye kuzaa matunda kiutamaduni. Kupitia mahusiano haya ya karibu, Mkataba wa  kielimu unaweza kutokea kwa hakika kati ya wale wote wanaofanya kazi kwa ajili ya ukuaji wa kibinafsi wa watu binafsi katika nyanja zake mbalimbali za kisayansi, kisiasa, kisanii, riadha na nyinginezo. Elimu sio mchakato unaoisha mara tunapotoka darasani au maktaba tu; inaendelea maishani, katika mikutano yetu ya kila siku na wengine na kwenye njia tunazopita. Mkataba huo ambao Papa Francisko anawaalika  kukuza unapaswa kuzaa matunda ya amani, haki na kukubaliana kati ya watu wote na kupanua athari zake chanya katika aina za ushirikiano wa karibu zaidi.

Mkutano wa Papa na washiriki wa Mkutano kuhusu Mkataba wa Elimu Kimataifa
Mkutano wa Papa na washiriki wa Mkutano kuhusu Mkataba wa Elimu Kimataifa

Hali hii ya uelewa  Papa amesema, inaweza kukuza mazungumzo ya kidini na kutunza nyumba yetu ya pamoja. Sote tunajua kwamba kazi hiyo si rahisi, lakini hakika inasisimua! Katika kukabiliana na changamoto hii, shule za Kikatoliki za kila aina na ngazi  zote zinaitwa kwa ujasiri kufanya mabadiliko yoyote yanayohitajika, zikiacha shughuli zao zisukumwe na mafundisho ya Yesu, Mwalimu wetu wa kawaida.  Ili kukuza uthabiti kati ya mipango mbalimbali, Papa Francisko amewahimiza wazingatie hasa kanuni mbili zinazotolewa kutoka katika Waraka wa Kitume Evangelii Gaudium: “Mambo halisi ni muhimu zaidi kuliko Mawazo” (kifungu 231-233) na “Yote ni makubwa kuliko sehemu.” (kifungu 234-237). Papa Francisko amedadavua kuwa “Kwanza, programu za elimu zinapaswa kuwaleta wanafunzi kuwasiliana na hali halisi inayowazunguka, ili, kuanziana  uzoefu, wajifunze kubadilisha ulimwengu si kwa manufaa yao wenyewe, bali katika roho ya huduma.

Vijana kutoka sehemu mbali mbali duniani
Vijana kutoka sehemu mbali mbali duniani

Papa ameongeza “Pili, elimu ya Kikatoliki inapaswa kukuza “utamaduni wa udadisi”, ikisisitiza sanaa ya kuuliza maswali. Hebu tuwaunge mkono vijana katika uchunguzi huu wao wenyewe na ulimwengu mkubwa zaidi, bila kupunguza ujuzi kwa maarifa ya akili, lakini kuongezea ujuzi huo kwa ustadi wa mwongozo na ukarimu uliozaliwa na moyo wa shauku.” Hapa Baba Mtakatifu alisema “kuna njia nzuri ya kufanikiwa katika kazi hii ya haraka. “Katika ulimwengu wetu huu wa ‘kimiminika’, tunahitaji kuanza kuzungumza kwa mara nyingine tena kuhusu moyo”(Waraka wa kitume wa Dilexit Nos, 9), kwani “ni kwa kuanzia kutoka moyoni tu ndipo jumuiya zetu zitafaulu katika kuunganisha na kupatanisha watu tofauti, akili na lengo, ili Roho aweze kutuongoza katika umoja kama kaka na dada” (kifungu, 28). Papa ameongeza kuwa “Hapo tunaona kiini cha shughuli nzima ya elimu: kutunza moyo wa mwanadamu.” Kwa kuhitimisha amewashukuru kwa yote wanayofanya. Bwana daima aiweke shauku ya elimu ndani yenu. Na hatimaye amewabariki kutoka moyoni, na amewaomba, tafadhali wamkumbuke katika sala zao.

Papa na Mkataba wa Kielimu duniani
09 November 2024, 11:24