Papa Francisko,Sala ya Malaika wa Bwana:Utawala wa Yesu ni wa Milele!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya Misa Takatifu Baba Mtakatifu Francisko, baadaye alielekea kwenye Dirisha la Jumba la Kitume Mjini Vatican ambapo kwa kuwalekea waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 24 Novemba 2024 alitoa pia tafakari fupi. Akianza alisema “Leo Injili ya Liturujia (Yh 18,33-37) inatuonesha Yesu mbele ya Pontio Pilato: alikabidhiwa kwa mkuu wa Kirumi ili amhukumu kifo. Hata hivyo, mazungumzo mafupi huanza kati ya watu hao wawili yaani kati ya Yesu na Pilato. Kupitia maswali ya Pilato na majibu ya Bwana, maneno mawili hasa yanabadilishwa, yakipata maana mpya. Maneno mawili: neno “mfalme” na neno “ulimwengu.”
Mara ya kwanza Pilato alimwuliza Yesu: “Je, wewe ni mfalme wa Wayahudi?” (rej. Yh 18,33). Kwa kufikiria kwamba yeye ni afisa wa milki hiyo, anataka kuelewa ikiwa mtu aliye mbele yake ni tishio, na wakati yeye ndiye anafikiria kuwa mfalme mwenye mamlaka juu ya raia wake wote. Kwa hiyo hii itakuwa tishio kwake, sawa? Papa aliuliza na kuendelea. Yesu anadai kuwa mfalme, ndiyo, lakini kwa njia tofauti kabisa! Yesu ni mfalme kwa sababu yeye ni shuhuda: yeye ndiye asemaye ukweli (rej Yh 18, 37). Nguvu ya kifalme ya Yesu, Neno aliyefanyika mwili, iko katika neno lake la kweli na neno lake lenye ufanisi, ambalo linabadilisha ulimwengu.”
Baba Mtakatifu alisema kuwa “Ulimwengu ndiyo kifungu cha pili. "Dunia" ya Pontio Pilato ni mahali ambapo wenye nguvu huwashinda wanyonge, matajiri juu ya maskini, wenye jeuri juu ya wapole, yaani, ulimwengu ambao kwa bahati mbaya tunaujua vizuri. Yesu ni Mfalme, lakini ufalme wake si wa ulimwengu huo, hata si wa ulimwengu huu (Yh 18, 36).” Aidha aliendelea, “Ulimwengu wa Yesu, kiukweli, ni mpya, ule wa milele, ambao Mungu hutayarisha kwa kila mtu kwa kutoa maisha yake kwa ajili ya wokovu wetu. Ni ufalme wa mbinguni, ambao Kristo anauleta duniani kwa kumimina neema na kweli. Ulimwengu, ambao Yesu ni Mfalme wake, unakomboa uumbaji ulioharibiwa na uovu kwa nguvu ya upendo wa kimungu, Yesu anaokoa uumbaji, kwa sababu Yesu, anasamehe, Yesu anatoa amani na haki. "Lakini huyu ni baba wa kweli?" - "Ndiyo". Nafsi yako ikoje? Kuna kitu kizito hapo? Kasoro fulani ya zamani? Yesu anasamehe daima. Yesu hachoki kusamehe. Huu ni Ufalme wa Yesu Ikiwa kuna kitu kibaya ndani yako, omba msamaha. Na Yeye husamehe daima.”
Kwa njia hiyo Papa amekazia kusema kuwa “ Yesu anazungumza na Pilato kwa ukaribu sana, lakini anakaa mbali naye, kwa sababu anaishi katika ulimwengu tofauti, hata ikiwa yuko mbele yake. Atamsulubisha Yesu, na kuwaamuru waandike msalabani: “Mfalme wa Wayahudi” (Yh 19:19), lakini bila kuelewa maana ya maneno hilo la:“Mfalme wa Wayahudi.”Lakini Kristo alikuja ulimwenguni, katika ulimwengu huu: kila aliye wa kweli huisikia sauti yake ( Yohana 18:37). Ni sauti ya Mfalme wa ulimwengu, ambaye anatuokoa
Papa ameleza kwamba ,“kumsikiliza Bwana hutuangazia mioyo yetu na maisha yetu. Kwa hiyo hebu tujaribu kujiuliza - kila mtu ajiulize moyoni mwake -: Je, ninaweza kusema kwamba Yesu ni "mfalme" wangu? Au je, nina “wafalme” wengine ndani ya moyo wangu? Kwa maana gani? Je! Neno Lake ni mwongozo wangu, hakika yangu? Ninaona kwake uso wa huruma wa Mungu ambaye husamehe daima, anayesamehe daima, je, anasubiri sisi kutupa msamaha? Tusali pamoja kwa Maria, mjakazi wa Bwana, tunapongojea kwa matumaini Ufalme wa Mungu.