Papa:Epuka unafiki na wajibika kwa unyenyekevu na huruma
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko akiwa katika dirisha la Jumba la Kitume mjini Vatican kwa kuwageukia waamini na mahujaji wengi sana waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Dominika tarehe 10 Novemba 2024, ameanza kusema: “Leo Injili ya liturujia (Mk 12,38-44) inatuambia kuhusu Yesu ambaye, katika hekalu la Yerusalemu, anashutumu mtazamo wa unafiki wa baadhi ya waandishi mbele ya watu (rej Lk 12, 38-40). Wale wa mwisho walikuwa wamekabidhiwa jukumu muhimu katika jumuiya ya Israel: walikuwa wanasoma, waliandika na kutafsiri Maandiko. Kwa hiyo waliheshimiwa sana na watu wakawaheshimu. Zaidi ya kuonekana kijujuu, hata hivyo, tabia yao mara nyingi haikupatana na yale waliyofundisha. Hawakuwa thabiti. Wengine, kiukweli, wenye nguvu katika ufahari na mamlaka waliyofurahia, waliwadharau wengine kwa kuwatazama kuanzia juu hadi chini”- Papa ameongeza kusema: “ni jambo baya sana kutazama mtu kunzia juu hadi chini,”walijionesha na, wakijificha nyuma ya sura ya heshima ya uwongo na ushikaji sheria, walijivunia mapendeleo na hata kufikia hatua ya kufanya wizi wa moja kwa moja kwa madhara ya walio dhaifu zaidi, kama vile wajane (rej Mk 12, 40).
Baba Mtakatifu ameongeza: "Badala ya kutumia jukumu walilopewa kuwatumikia wengine, walilifanya kuwa chombo cha kiburi na wizi. Na ikawa kwamba hata sala, kwao, ilihatarisha kutokuwa tena wakati wa kukutana na Bwana, lakini ikiwa fursa ya kuonesha heshima na uchaji wa uwongo, na umuhimu kwa kuvutia umakini wa watu na kupata maelewano." Kwa njia hiyo Papa amekazia kusema kuwa “Tukumbuke kile ambacho Yesu alisema katika sala ya mtoza ushuru na mfarisayo(Lk 18,9-14). Wao – lakini sio wote - walitenda kama watu wafisadi, wakichochea mfumo wa kijamii na kidini ambao ulikuwa kawaida kuchukua faida ya wengine, hasa wasio na ulinzi, kwa kutenda dhuluma na kutokujali kabisa. “kwa hiyo “Yesu alipendekeza kukaa mbali na watu hawa, “kuwa makini” (Rej Mk 12, 38), na si kuwaiga.
Papa amesisitiza kwamba "Kiukweli, kwa neno lake na kielelezo chake, kama tujuavyo, anafundisha mambo tofauti sana kuhusu mamlaka. Anazungumza juu ya hilo kwa njia ya kujitolea na huduma ya unyenyekevu (rej. Mk 10:42-45), juu ya huruma ya umama na ubaba kwa watu (rej. Lk 11:11-13), hasa wale wanaohitaji sana (Lk 10, 25-37)." Kwa njia hiyo Yesu " Anawaalika wale walio na majukumu kuwatazama wengine, kutoka katika nafasi zao za madaraka, si kuwadhalilisha, bali kuwainua, kuwapa matumaini na msaada."
Kwa kuhitimisha Papa Francisko amebainisha kuwa: “tunaweza kujiuliza: je, nina tabia gani katika maeneo yangu ya uwajibikaji? Je, ninatenda kwa unyenyekevu, au ninajivunia cheo changu? Je, mimi ni mkarimu na mwenye heshima kwa watu, au ninawatendea kwa njia isiyo na adabu na ya kimabavu? Na kwa walio dhaifu zaidi, je, niko karibu nao, je, najua jinsi ya kuinama ili kuwasaidia kuinuka? Bikira Maria atusaidie kupambana na jaribu la unafiki ndani yetu - Yesu anawaita "wanafiki", unafiki ni jaribio kubwa - na atusaidie kutenda mema bila kujionesha na kwa urahisi.