2024.11.17:Siku ya Maskini duniani:chakula cha mchana na maskini. 2024.11.17:Siku ya Maskini duniani:chakula cha mchana na maskini.  (Vatican Media)

Papa Fransisko katika Sala ya Malaika na kitovu cha Siku ya Maskini Duniani!

Mashahidi waliotangazwa wenyeheri huko Scutari,pia mmoja huko Freiburg im Breisgau,Siku ya Maskini duniani,kaulimbiu:“Sala ya maskini huinuka kwa Mungu,"Siku ya Maombi kwa waathirika wa nyanyaso nchini Italia,Siku ya wavuvi duniani Novemba 21 na kuombea amani,ndivyo alikumbusha Baba Mtakatifu mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana Dominika 17 Novemba 2024.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Mashahidi wawili walitangazwa kuwa wenyeheri jana huko Scutari ambao ni Luigi Palić, kuhani wa Shirika la Ndugu Wadogo, na Gjon Gazulli, Padre wa jimbo, waliokuwa waathrika wa mateso ya kidini ya karne ya XX. Na leo hii huko Freiburg im Breisgau,  shahidi mwingine alitangazwa mwenyeheri, Padre Max Josef Metzger, mwanzilishi wa Taasisi ya kiulimwengu ya Kristo Mfalme, aliyepingwa na Unazi kwa kujitolea kwake kidini kwa ajili ya amani. Hayo ni maneno ya  Baba Mtakatifu Francisko aliyoanza nayo mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 17 Novemba 2024 kwa waamini na mahujaji waliofika katika uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican.  Kwa njia hiyo Papa akielezea kuhusu hawa waliotangaza kuwa wenyeheri, aliongeza kusema: “Mfano wa mashahidi hawa uwafariji Wakristo wengi ambao katika nyakati zetu wanabaguliwa kwa ajili ya imani yao. Mzunguko wa makofi kwa Wenyeheri hawa wapya!....” Papa aliomba wapigiwe makofi.

Chakula cha mchana na maskini

Siku ya Maskini duniani

Papa Francisko aliendelea kutazama kilele cha siku kwamba: “Leo tunaadhimisha Siku ya Maskini Ulimwenguni, ambayo mada yake ni "Sala ya maskini huinuka kwa Mungu" (Sir 21:5). Ninawashukuru wale wa majimbo na Parokia ambao wamehamasisha mipango ya mshikamano kwa watu wasiojiweza. Na siku hii pia tunawakumbuka wahanga wote wa barabarani: tuwaombee, kwa ajili ya familia zao, na tujitoe katika kuzuia ajali.” Papa aliongeza hili: “Ninauliza swali, kila mtu anaweza kujiuliza swali hili mwenyewe: je, ninajinyima kitu ili kuwapatia maskini? Je, nikitoa sadaka, je, mimi hugusa mkono wa maskini na kumtazama machoni? Ndugu, tusisahau kwamba maskini hawezi kusubiri!”


Siku ya Maombi kwa waathirika wa nyanyaso Italia

Baba Mtakatifu Francisko aidha alisema kuwa “Ninajiunga na Kanisa nchini Italia ambalo kesho linapendekeza Siku ya Maombi kwa waathirika wa unyanyasaji. Kila unyanyasaji ni usaliti wa uaminifu, ni usaliti wa maisha! Maombi ni muhimu ili "kurejesha uaminifu".

Siku ya wavuvi duniani Novemba 21

Papa Francisko akiendelea na madhimisho ya siku nyingine alisema “Napenda pia kuwakumbuka wavuvi wote, katika tukio la Siku ya Uvuvi Duniani, ambalo litakuwa Alhamisi ijayo: Maria, Nyota ya Bahari, ulinde wavuvi na familia zao.”

Salamu mbalimbali

Akiendelea na salamu Papa alisema: “Na ninawasalimu ninyi nyote kwa upendo, Waroma na mahujaji. Hasa, waamini waliofika kutoka Ponta Delgada na Zagreb; Monasteri ya Mtakatifu Lorenzo wa El Escorial na jumuiya ya Ecuador ya Roma, ambayo inaadhimisha Bikira wa Quinche. Amesalimu vikundi kutoka Chioggia na Caorle; wazima moto wa Romeno (Trento) na kwaya ya Parokia ya Nesso (Como).

Kuombea amani

Papa Francisko kama kawaida yake hakusahu suala la amani: "Kaka dada, tuombe kwa ajili ya amani: katika Ukraine inayoteswa, Palestina, Israel, Lebanon, Myanmar, Sudan. Vita hutufanya kuwa wabaya, hutuongoza kuvumilia uhalifu usiokubalika. Serikali lazima zisikilize kilio cha wananchi wanaoomba amani.” Salamu kwa vijana wa mama Maria Mkingiwa. Na kwa kuhitimisha akiwatakia wote Domenika njema na tafadhali wasisahau kumuombea. Mlo mwema, mchana mwena na kwaheri ya kukuona!

Mara baada ya Angelus
17 November 2024, 15:23