2024.11.20 Pier Giorgio Frassati  na  Carlo Acutis 2024.11.20 Pier Giorgio Frassati na Carlo Acutis 

Papa:katika siku ya watoto Papa,atatangaza kuwa mtakatifu Acutis na Giorgio Frassati katika Siku ya vijana Duniani!

Wakati wa salamu kwa mahujaji,baada ya Katekesi yake Novemba 20,Papa Francisko ametangaza kuwa katika Siku ya Watoto Duniani mwaka kesho yaani katika Mwaka Mtakatifu wa Jubilei atamtangaza Mwenyeheri Carlo Acutis kuwa Mtakatifu na wakati huo huo pia kumtangaza kuwa Mtakatifu,Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati katika Siku ya Vijana duniani.

Na Angella Rwezaula - Vatican.

Siku ambayo ilitarajiwa kwa hamu sana, imewadia ile ya kujua tarehe za kutangazwa watakatifu kwa wenyeheri vijana na ambapo katika mwaka Mtakatifu wa Jubilei bado unafunguliwa na utakatifu  wa watakatifu wapya wa Mungu. Ni katika siku ya Jumatano tarehe 20 Novemba 2024, ambapo mara baada ya Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, kwa waamini na mahujaji waliofika kutoka pande za dunia, wakati wa salamu zake kwa wanaozungumza lugha ya kitaaliano pamoja na mambo mengine aliyozungumza ya muhimu,  alisema “Ninataka kusema kwamba mwaka ujao katika Siku ya Watoto na Barubaru, nitamtangaza Mwenyeheri Carlo Acutis, kuwa Mtakatifu,  kwamba Siku ya Vijana, mwaka ujao, nitamtangaza Mwenyeheri Giorgio Frassati kuwa Mtakatifu.”

Carlo Acutis
Carlo Acutis

Mwenyeheri Carlo Acutis

Mwenyeheri Carlo Acutis, alizaliwa London, Uingereza  mnamo 1991, ambapo wazazi wake walikuwa huko kwa sababu za kazi, alikuwa na utauwa wa kina wa  mapema sana. Alipokea Komunyo yake ya Kwanza, kwa idhini maalum, akiwa na umri wa miaka saba tu. Alikuwa kijana aliyeudhuria Misa kila siku na kusali  Rozari. Aliendelea kukua na upendo wa kupendeza kwa watakatifu na kwa Ekaristi, hadi kufikia hatua ya kuanzisha maonesho ya miujiza ya Ekaristi ambayo imebaki mtandaoni hadi leo hii na imekuwa na mafanikio yasiyotarajiwa, hata nje ya nchi kwa ujumla ulimwenguni kote.

Carlo Acutis
Carlo Acutis

Carlo alifariki dunia tarehe 12 Oktoba, 2006 na kifo chake kilitokana na ugonjwa wa Saratani ya damu (Leukemia) katika Hospitali ya Mtakatifu Gerardo, mji wa Monza, Italia. Mchakato wake wa kutangazwa mtakatifu ulipata kibali tarehe 13 Mei, 2013. Papa Francisko tarehe 5 Julai, 2018 alimtangaza kuwa Mtumishi wa Mungu. Na tarehe 21 Februari 2020 Papa Francisko aliridhia mchakato wa kutangazwa kuwa MwenyeHeri. Na muuujiza unaomwinua kuwa Mwenye heri ulitokea kutokana na uponyaji wa mtoto chini Brazil aliyekuwa na shida ya kongosho hapo mwaka 2013. Jumamosi tarehe 10 Oktoba 2020 katika mji wa Assisi, Mtumishi wa Mungu Carlo Acutis alitangazwa mwenyeheri. Tangu wakati huo waamini wengi duniani kote na hasa vijana wanaenzi wito wake: kusali Rozari, kuabudu, misa na kutoa sadaka na kusaidia maskini.

Mwenyeheri Giorgio Frassati

Kwa upande wa Goirgio Frassati ni Mwenyeheri ajulikanaye kwa vijana wengi wakatoliki nchini Italia kwa sababu alikuwa ni mmoja wa Chama cha matendo ya vijana Katoliki. Alizaliwa tarehe 6 Aprili 1901 huko Torino nchini Italia katika familia ya kitajiri. Alipokuwa mtoto, alijifunza historia za kwanza za Injili, Pier Giorgio alishangazwa nazo, wakati mwingine kwa undani sana kwamba akawa mhusika mkuu wa ishara zisizotarajiwa kwa mtoto mdogo kama huyo. Familia ya Frassati ilikuwa mojawapo ya familia mashuhuri katika jiji hilo, za uchimbaji wa hali ya juu, lakini Pier Giorgio Frassati alipendelea kuwa “mbeba mizigo” wa maskini, akiburuta mikokoteni iliyopakiwa na bidhaa za nyumbani za waliofukuzwa kupitia mitaa ya Turino na kama mshiriki wa Shirika la Mtakatifu Vincent atembelea familia zenye uhitaji zaidi ili kuleta faraja na usaidizi wa mali. Kwa ujumla alikwenda huko asubuhi, kabla ya masomo katika Chuo Kikuu, au kwenye matembezi ya jioni, akiwa amebeba vifurushi. Nguvu, yenye nguvu, iliyojaa maisha, Pier Giorgio alipenda maua na mashairi, kupanda mlima. Mara nyingi alifika Kwenye madhabahu ya Mama Maria wa Ulaya kwa miguu.

Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati
Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati

Akiwa amefika kwenye madhabahu  baada ya mwendo wa saa moja na kufunga kabisa, alizoea kuhudhuria Misa Takatifu, kisha alipokea Komunyo na alipokuwa njiani kurudi nyumbani, alisali Rozari, kwa sauti kubwa, huku akiimba Litania. Tarehe 28 Mei 1922, katika Kanisa la Torino la Mtakatifu Domeniko, alipokea Nguo za Utawa wa Tatu wa Wadomikani ambapo tangu wakati huo Pier Giorgio, akawa mfuasi mwenye bidii wa Mtakatifu Domeniko huku akisali Rozari kila siku, ambayo kila mara aliibeba kwenye mfuko wa koti lake, bila kusita kuitoa wakati wowote ili kusali, hata kwenye treni  au basi, na hata mitaani.

Pier Girogio alisema,  akionesha Rozari: “Wosia wangu mimi hubeba kila wakati mfukoni mwangu.” Mnamo tarehe 30 Juni 1925 Pier Giorgio alilalamika juu ya magonjwa ya ajabu, migraines na kupoteza hamu ya kula: haikuwa homa, lakini polio kali iliyompata kwa siku nne tu, mnamo tarehe 4 Julai kwa mshtuko na maumivu ya familia yake na marafiki wengi, akiwa na umri wa miaka 24 tu aliaga dunia. Kwenye dawati lake, karibu na maandishi ya chuo kikuu, Kulikuwa na Rosari na maisha ya Mtakatifu Catherine wa Siena ambayo yalikuwa wazi. Alizaliwa katika maisha ya Mbinguni siku ya Jumamosi, ambayo Mama Kanisa hukumbuka Bikira Maria. Alitangazwa kuwa mwenyeheri na na Mtakatifu Yohane Paulo II mnamo tarehe 20 Mei 1990.

Tarehe 13 Juni 2018, Baba Mtakatifu akiwa katika Katekesi yake alisema kuwa "Mwenye heri Pier Giorgio Frassati alikuwa ni kijana ambaye alikuwa akisema kwamba, lazima kuishi na siyo kujizeesha kwa maana watu hafifu wanazeeka, kwa maana hiyo ni kuishi kwa nguvu ya maisha. Ni lazima kuomba Baba wa mbinguni kwa ajili ya vijana leo hii  ili wapate zawadi kamili ya shauku, na uwezo wa kutokuridhika tu na maisha bila uzuri na bila rangi. Iwapo vijana hawatakuwa na njaa ya maisha ya kweli, ubinadamu utakwenda wapi? Aliuliza Baba Mtakatifu Francisko. Je ubinadamu huu na vijana wenye mashaka na mahangaiko wataishia wapi? Hivi karibuni, akikutana na watawa aliwaomba kuiga mfano wa Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati.

Frassati na Acutis
20 November 2024, 10:33