Tafuta

Papa:Kila kitu kinakufa lakini hatutapoteza chochote tulichojenga na kupenda!

Kabla ya Sala Malaika wa Bwana,Papa anatukumbusha kwamba katika dhiki,mizozo na kushindwa,tunapaswa kuangalia maisha na historia bila hofu ya kupoteza mwishoni lakini kwa furaha kwa kile kinachobaki.Maumivu yanayosababishwa na vita,jeuri na majanga ya asili yanaweza kutufundisha kutojihusisha na mambo ya ulimwengu ambayo bila shaka yamekusudiwa kufifia.

Na Angella Rwezaula – Vatican

Baba Mtakatifu Francisko  Dominika tarehe 17 Novemba 2024 wakati wa tafakari yake, kabla ya sala ya Malaika wa Bwana akiwa katika Dirisha la Jumba la Kitume kwa kuwageukia waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, ametoa mwaliko wa kushinda kushikamana na mambo ya kidunia, migogoro na kushindwa, au maumivu yanayosababishwa na vita, vurugu, majanga ya asili, hayawezi na hayapaswi kutuingiza katika ukiwa. Katika Injili ya liturujia ya leo, Yesu anaelezea dhiki kuu: "jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake" (Mk 13:24). Wakikabiliwa na mateso haya, wengi wanaweza kufikiria mwisho wa dunia, lakini Bwana anachukua fursa hiyo kutoa tafsiri tofauti, akisema: “Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe” (Mk 13:31).

Waamini na mahujaji katika sala ya Malaika wa Bwana
Waamini na mahujaji katika sala ya Malaika wa Bwana

Papa amesisitiza "Hebu tuangalie hili, basi: nini kitapita na nini kitabaki. Kwanza kabisa, nini kitapita. Katika hali zingine katika maisha yetu, tunapopitia shida au tunaposhindwa, na vile vile tunapoona karibu nasi maumivu yanayosababishwa na vita, jeuri, majanga ya asili, tuna hisia kwamba kila kitu kinakuwa mwisho, na tunahisi kwamba hata mambo mazuri zaidi yanapita. Migogoro na kushindwa, hata hivyo, ingawa ni chungu, ni muhimu, kwa sababu hutufundisha kukubaliana na kila kitu uzito wake unaostahili, sio kushikamana na mioyo yetu na hali halisi ya ulimwengu huu, kwa sababu itapita: imekusudiwa kufifia."

Papa akiendelea alisema "Wakati huohuo, Yesu anaeleza kuhusu yatakayobaki. Kila kitu kinapita, lakini maneno yake hayatapita: yatabaki milele. Hivyo anatualika tuitumainie Injili, ambayo ina ahadi ya wokovu na umilele, na sio kuishi chini ya uchungu wa kifo. Kwa maana wakati kila kitu kinapita, Kristo anabaki. Ndani Yake siku moja tutapata tena vitu na watu ambao wamepita na ambao wamefuatana nasi katika uwepo wetu hapa duniani. Katika nuru ya ahadi hii ya ufufuko, kila ukweli unakuwa na maana mpya: kila kitu kinakufa na sisi pia siku moja tutakufa, lakini hatutapoteza chochote kwa kile tulichojenga na kupenda, kwa sababu kifo kitakuwa mwanzo wa maisha mapya."

Sala ya Malaika wa Bwana
Sala ya Malaika wa Bwana

Papa amesema “hata katika dhiki, katika shida, katika kushindwa, Injili inatualika kutazama maisha na historia bila hofu ya kupoteza mwisho, lakini kwa furaha kwa kile kitakachobaki. Mungu anatuandalia mustakabali wa maisha na furaha. Na kwa hivyo, hebu tujiulize: je, tunashikamana na vitu vya kidunia, vinavyopita haraka, au kwa maneno ya Bwana, ambayo yanabaki na kutuongoza kuelekea umilele? Hebu tujiulize swali hili, tafadhali. Tumwombe Bikira Mtakatifu: Maria aliyejikabidhi kikamilifu kwa Neno la Mungu, atuombee.” Papa Francisko amehitimisha.

Papa tafakari kabla ya Angelus
17 November 2024, 13:03